NHC yakutanisha historia, maendeleo kuipaisha Tabora

-      Sh. 4 bilioni zaleta Tabora Business Complex

-   Alama mpya kuvutia uwekezaji

-    -   Yawekeza makazi, biashara, wateja wapigana vikumbo

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Katika juhudi za kuendeleza makazi bora kwa Watanzania, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limeanza kutekeleza mradi mkubwa wa jengo la kisasa la biashara na makazi katikati ya mji wa kihistoria wa Tabora.

Mwonekano wa Jengo la Tabora Commercial Complex litakapokamilika

Mkoa wa Tabora, jina linalotajwa kutokana na neno 'Matobolwa' ambalo ni viazi vitamu vilivyokaushwa, ambalo wakoloni walishindwa kulitamka na kutamka Tabora, ni mmoja wa mikoa 31 ya Tanzania,  ukijivunia kuwa na eneo kubwa zaidi kitaifa.

Una eneo la takriban kilomita za mraba 76,151. Kati ya eneo hilo, asilimia 46 ni hifadhi ya misitu (km² 34,698) huku asilimia 22 (km² 17,122) ikiwa ni hifadhi ya wanyamapori.

Tabora inapakana na Mkoa wa Shinyanga upande wa kaskazini, Singida mashariki, Mbeya na Songwe kusini, na Katavi, Kigoma pamoja na Geita upande wa magharibi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mkoa huu ulikuwa na wakazi 3,391,679 wanaoishi katika wilaya nane: Tabora Mjini (308,741), Nzega Vijijini (574,498), Nzega Mjini (125,193), Igunga (546,204), Uyui (562,588), Urambo (260,322), Sikonge (335,686) na Kaliua (678,447). Wakazi wengi wa Tabora ni jamii ya Wanyamwezi, wakijishughulisha zaidi na kilimo na ufugaji.

Mkoa wa Tabora una historia ndefu, ukijulikana kwa watawala wa jadi kama Mtemi Milambo, ambaye jina lake bado linaishi kupitia shule, mitaa na taasisi mbalimbali. Aidha, Tabora imekuwa na mchango mkubwa katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika na pia kwenye siasa za vyama vingi nchini.

Hata hivyo, pamoja na umaarufu na ukubwa wake, mkoa huu haukuwa na jengo la kisasa la biashara linaloendana na hadhi yake. Lakini sasa ni kama NHC inahuisha utemi wa Milambo. Inafanya hivyo, kwa kuiondoa Tabora katika unyonge wa kukosa jengo la kisasa linaoendana na historia na hadhi ya mkoa huo baada kuanzisha mradi wa Tabora Commercial Complex, ambalo ni la kwanza la aina yake mkoani humo.

Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 4 na unatarajiwa kukamilika mwaka ujao ifikapo Aprili 2026. Tayari ujenzi umeanza mwezi Mei mwaka huu na wananchi wa kada mbalimbali wameanza kunufaika kiuchumi, huku maombi ya nafasi za biashara na makazi yakiwa yamefurika.

Meneja wa NHC Mkoa wa Tabora, Eminick Sanga, amesema:

“Hadi sasa tumezipokea zaidi ya maombi 200 kutoka kwa watu wanaotaka kupangisha sehemu za biashara, ofisi na makazi. Mwitikio ni mkubwa sana na tunaamini jengo hili litaleta mageuzi makubwa mkoani Tabora."

Ameongeza kuwa mradi huo si tu utaongeza makusanyo ya kodi za serikali, bali pia umefungua fursa za ajira kwa wananchi na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi.

“Wananchi wamepata ajira kwenye ujenzi, akina mama ntilie wanaingiza kipato kwa kuuza chakula kwa mafundi, na hata kabla ya kukamilika, tayari tunaanza kupokea wapangaji,” amesema Sanga.

Mkazi wa Tabora, Regina Mikongo, amesema:“Jengo hili litavutia wawekezaji na wageni kutoka nje ya mkoa wetu. Linaongeza hadhi ya mji wetu na kufungua fursa mpya za kiuchumi.”

Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi huo, Remigius Chrisostoms, amesema kuwa jengo hilo la ghorofa nne litawezesha uwepo wa zaidi ya maduka 50, migahawa, benki, ofisi na makazi.

“Ghorofa ya kwanza itakuwa kwa ajili ya ofisi, huku ghorofa ya pili hadi ya nne zikiwa ni za makazi. Ujenzi ulianza Mei 2025 na utakamilika Aprili 2026,” amesema.

Mkazi mwingine wa Tabora, Sebedia Jonas, amesema: “Mradi huu ni wa kipekee. NHC imetuletea maendeleo halisi. Ni matumaini yangu kuwa mradi huu utaibadilisha Tabora kuwa jiji kamili.”

Mradi wa Tabora Commercial Complex ni zaidi ya jengo – ni dira mpya ya maendeleo kwa Mkoa wa Tabora. Kupitia uwekezaji huu wa kimkakati, NHC imethibitisha dhamira yake ya kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Watanzania katika kila kona ya nchi.


 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi