Masasi sasa kumekucha, NHC yaipa sura mpya

 - Yajenga jengo la Sh2.7 bilioni, kukamilika Septemba

- Unaijua Jida? Sasa nenda Masasi

Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Masasi kumekucha, ‘Jogoo’, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limewika na kwa lugha ya wenyeji unaweza kusema ‘Masasi Kuchele’.

Ndivyo unavyoweza kuielezea Mei 18,2025 siku ambayo historia mpya imeandikwa na NHC katika Mji wa Masasi, uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.

Historia hiyo mpya iliyoandikwa ni kuzinduliwa ujenzi wa jengo jipya la Kituo cha Biashara, Masasi Commercial Complex kwa kuwekwa Jiwe la Msingi, huku aliyetimiza jukumu hilo akiwa pia kiongozi wa kihistoria kitaifa.

Hakika hakuna wa kupinga kuwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi kwani ni aghalab kiongozi wa mbio hizo kujirudia.

Kuzinduliwa kwa Masasi Commercial Complex jengo ambalo ni la kisasa zaidi Masasi, wilaya inayobeba sehemu muhimu ya historia ya Tanzania, ikikumbukwa kuwa Rais wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin Mkapa alizaliwa wilayani humo katika Kijiji cha Lupaso.

Hata hivyo, safari hii historia inalibeba eneo la Jida, jina linaloakisi eneo maarufu katika masuala ya Hijja kwa watu wa Imani ya Kiislamu wanapofanya safari au kuzungumzia Mji Mtakatifu wa Makka.

Hiyo ndio Kata lilinapojengwa jengo hilo na NHC katika Mtaa wa Madaraka, ambalo ni kitega uchumi na hapana shaka, litakapokamilika, litaibeba na kuibadili sura ya mji huo na kuifanya mpya, likiwa katika barabara kuu wilayani humo.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linajenga jengo hilo ikiwa ni sehemu ya kutimiza maono yake na Serikali kutekeleza sera ya mapinduzi ya sekta ya nyumba na makazi bora ya kisasa nchini, lakini pia kuchagiza kasi ya ukuaji uchumi wa taifa, huku likitekeleza dira yake iliyojiwekea kwa miaka 11.

Akiweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Masasi Commercial Complex, Kiongozi wa Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi (Pichani chini), analipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa kazi kubwa ya kutekeleza kwa vitendo ndoto za kuboresha huduma za jamii na wafanyabiashara nchini kupitia sekta ya nyumba.

Sauti ya Ussi inasikika akisema; “Kwa kujenga majengo bora ya kisasa, NHC inachochea kasi ya maendeleo na uchumi wa taifa.”

Sauti hiyo iliyobeba mamlaka kitaifa inaongeza: “NHC mnafanya kazi kubwa kwenye sekta ya ujenzi mkiisaidia Serikali kutimiza ndoto za kuboresha huduma ya makazi bora na maeneo bora ya biashara kwa jamii.”

Jengo hilo la kisasa lina maeneo mbalimbali ya kibiashara ikiwamo benki, maduka, migahawa na ofisi za kufanyia biashara mbalimbali.

Ussi anasema Serikali imekuwa na jitihada za makusudi kuwaletea wananchi wake maendeleo, jambo ambalo limeshuhudiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, kuweka jiwe la msingi la jengo hilo linalobadili sura ya maendeleo kwa wananchi wa Masasi.

“Leo hii tupo hapa na NHC baada ya wao kufanya utafiti na kubaini hapa Wilayani Masasi kuna uhitaji wa masuala ya fedha, benki na mahitaji mengine ya kijamii.

 Tunawashukuru NHC kwa kazi kubwa, wameutendea haki Mwenge wa Uhuru kwa sababu jengo hili litawakusanya wafanyabiashara wengi na wananchi wetu watapata huduma,hakuna  mwananchi atakayekosa huduma anayohitaji katika jengo hili,” anasema Ussi.

Amewaomba wananchi kuonyesha ushirikiano kwa NHC katika matumizi bora ya uwekezaji huo wa eneo la huduma za kijamii, akieleza pia NHC imeonyesha kwa vitendo jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea wanachi maendeleo wanayohitaji.

Muungano Saguya ni Meneja Uhusiano na Habari wa NHC, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah kwenye ghafla ya uwekaji Jiwe la Msingi la ujenzi wa Masasi Commercia Complex, pamoja na mikakati mingine inayotekelezwa na shirika hilo, anazungumzia mradi huo katika mahojiano.

Muungano Saguya, Meneja Uhusiano na Habari wa NHC akizungumza katika mahojiano.

“Leo tumepata fursa, Mwenge wa Uhuru kuweka Jiwe la Msingi katika jengo hili la kisasa, Masasi Commercial Complex,” anasema Saguya.

Anasema kuwekwa jiwe la msingi kwa ujenzi huo kunafungua fursa mpya kwa watanzania na wafanyabiashara wa kada mbalimbali ambao watapata fursa ya kuwekeza na kufanya shughuli zao katika jengo jipya la kisasa.

“Jengo hili litagharimu Shilingi bilioni 2.7, limeshafikia zaidi ya asilimia 75 na tunatarajia litakamilika ifikapo Septemba mwaka huu 2025.

Kwenye miji karibu yote inayokua kwa kasi kubwa, NHC imejenga majengo makubwa. Kahama tumeweka jengo kama hili, leo tupo Masasi,” anasema na kufafanua; “Tumeweza kuweka majengo haya kwa ajili ya kuruhusu watanzania kuwekeza biashara zao. Hii itaweza kusaidia Serikali kuweza kukusanya mapato makubwa kutokana na kodi kutoka kwa wafanyabiashara.”

 Saguya anasema jengo hilo litaiongezea fedha zaidi  Shirika la Nyumba la Taifa, ambazo zitalisaidia kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya watanzania.

Anabainisha kwamba kwenye hotuba ya uzinduzi wa Masasi Commercial Complex, NHC imeombwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi, iende maeneo mbalimbali nchini kuwekeza majengo kama lilivyo Masasi Commercial Complex.

Saguya anasema kauli ya kiongozi huyo ni maelekezo kwa shirika kwani anafanya kazi kwa niaba ya Serikali.

“Kujenga majengo kama haya, kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa Serikali, hiyo ipo  kwenye mipango ya NHC, kuhakikisha tunafika kila halmashauri ya mji na wilaya kuona fursa zilizopo. Tukikubaliana na halmashauri hizo, tutaweza kwenda kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma,” anasema Saguya.

Akizungumzia matarajio ya shirika hilo Meneja huyo wa Uhusiano na Habari anasema, NHC inatarajia kukuza uchumi kwenye  miji inayokua kwa kasi.

Anaweka wazi kuwa kabla ya kutekeleza mradi wowote wa ujenzi, shirika hilo hufanya utafiti ili kujua mahitaji katika miji husika.

“Tulifanya utafiti katika Mji wa Masasi na miji mingine hapa nchini, tumejiridhisha kwamba tutapata wateja wa kutosha na kweli. Mpaka sasa jengo hili la Masasi Commercial Complex limeshajaa. Wateja wameshajiorodhesha wakihitaji kupangisha na hakuna tena nafasi,” anasema Saguya.

Furaha baada ya kuwekwa Jiwe la Msingi

Kwa mujibu wa Saguya, NHC ina uhakika kwamba baada ya jengo hilo kukamilika, wateja watajaa kwa asilimia 100, hivyo kuweza kuanza kurejesha fedha zilizotumika kwa ujenzi, lakini pia kuliwezesha  shirika kujenga majengo mengine kwa ajili  ya watanzania maeneo mbalimbali nchini.

Saguya anasema ujenzi wa nyumba unaofanywa na NHC ni endelevu na unafanywa kwa kuzingatia mahitaji ya watanzania.

Tuna kitengo ndani ya shirika huwa kinafanya utafiti na kuishauri menejmenti ya shirika kwamba eneo fulani lina mahitaji makubwa ya nyumba;

Kwa kweli tuna mahitaji makubwa za makazi na ndio maana NHC imeanza kubadili miji yetu kwa kushirikiana na  sekta binafsi, kwa kubomoa majengo makuukuu katikati ya miji ili kujenga majengo ya ghorofa;

Hayo yatatoa nafasi kubwa zaidi kwa wananchi kupata maeneo ya kufanyia biashara na maeneo ya kuishi. Mfano eneo la Kariakoo, tumeshabomoa majengo 21, miradi ikikamilika kujengwa thamani yake ni zaidi ya Shilingi bilioni 271, kabla ya kujengwa upya ilikuwa na thamani ya chini karibu Shilingi bilioni 70,” anasema Saguya.

Anabainisha kwamba majengo hayo, awali yalikuwa na wapangaji wasiozidi 172, lakini baada ya kubomolewa na kujengwa upya yatakuwa na wapangaji zaidi ya 2,150.

“Hapo unaweza kuona jinsi NHC inavyotumia mbinu mbalimbali kufanya utafiti na kushirikisha sekta binafsi kufahamu maeneo yenye masoko na kuwajengea watanzania kwa ajili ya makazi, masoko na matumizi mengine ya kijamii,” anasema Saguya.

Anabainisha kuwa katika Wilaya ya Masasi, NHC imejenga jengo jingine maeneo ya Chilungutwa, ambalo ni ghala, likisaidia wakulima kuhifadhi mazao yao.

Anasema jengo hilo limejengwa baada ya kufanyika utafiti na kujiridhisha kuwepo kwa mahitaji.

Saguya anasema NHC ina sera ya uwekezaji, ambayo huliwezesha shirika kupima na kutoa mwongozo kwamba majengo mangapi yanaweza kujengwa na ya aina gani.

Kwa mujibu wa Saguya, kwa sasa NHC ina majengo na nyumba zaidi ya 3,000 inayomiliki yenye sehemu za nyumba zaidi ya 18,000 nchini zilizojengwa kwa miaka tofauti.

“Mpango Mkakati wa shirika wa miaka 11, unatuelekeza namna ya kufanya uwekezaji wenye tija kwa NHC na taifa. Uwekezaji huo ni endelevu na tunaendelea kuufanya kwa Kadiri tunavyoendelea kupata mahitaji hayo,” anahitimisha Saguya.  

Neno la Meneja wa Mradi

Jiwe la Msingi la jengo la Masasi  Commercial Complex linavyosomeka.

Awali, akitoa historia ya ujenzi wa mradi wa kituo hicho mbele ya mgeni rasmi, meneja wa mradi huo, Gofrey Mkumbo kupitia risala aliyoisoma, ameeleza ulianza kutekelezwa Julai 25 mwaka 2024, baada ya NHC kukamilisha taratibu zote za ujenzi katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

“Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika, Septemba 14, mwaka 2025, ukiwa na maeneo mbalimbali ya biashara kama vile benki, ofisi, migahawa na maduka ya biashara mbalimbali,” anasema Mkumbo akiongeza:

“Ukamilifu wa ujenzi huu mpaka hapa ulipo ni asilimia 76. Hii ikijumuisha na taratibu zote za manunuzi ambazo zimeshakamilisha kwa vifaa vyote vya ujenzi ambavyo havijafika hapa kutokana na changamoto ya ubovu wa barabara za ukanda wa kusini.”

Hata hivyo, Mkumbo amesema vifaa hivyo vitaanza kuwasili ndani ya siku saba kuanzia Mei 18, 2025 hivyo kuendelea kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha biashara. 

Kuhusu lengo la mradi huo, Mkumbo ameyataja ni kuboresha huduma za kijamii na wafanyabiashara wa  ndani na na nje ya Masasi.

Kwa niaba ya NHC, Mkumbo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayofanya kazi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na mipango thabiti na kuinua uchumi wa taifa.

Akitoa maelezo kuhusu jengo hilo, Mshauri Elekezi wa mradi huo wa Kituo cha Biashara Masasi, Noel Mihanjo anasema kupitia mradi anaousimamia, kuna faida mbalimbali kwa wananchi wa Masasi.

Amezitaja kuwa ni pamoja na kutoa ajira za muda kwa wananchi wakati na baada ya ujenzi, kukuza uchumi kwa wafanyabiashara na kuleta mwonekano mzuri kwa mji wa Masasi.

“Pia kukuza uchumi wa wafanyabiashara wa eneo la Masasi, kuleta mwonekano mzuri wa Masasi hasa eneo hili, kandokando ya barabara kuu,” amesema.

Amebainisha kuwa hadi ulipofikia, mradi huo fedha ambazo zimeshatumika ni Shilingi 1,450,718,159.94. 


      

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi