Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Waziri Mazrui azindua Zanzibar Afya Week 2025

-Linalenga kuhamasisha utalii wa afya na kukuza sekta ya afya

Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com


Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Mazrui amezindua Zanzibar Afya "Week" 2025 Zanzibar Afya Week 2025 itakayofanyika Unguja na Pemba na kubainisha kuwa ni fursa adhimu ya kuimarisha mfumo wa afya, kukuza ubunifu katika sekta ya tiba, na kuhamasisha Utalii wa Afya Visiwani Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Mazrui

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo Aprili 12, 2025, Waziri Mazrui amewapongeza wadau wote wa sekta ya afya na washirika wa maendeleo wanaoshirikiana nasi kuhakikisha mafanikio ya Zanzibar Afya Week 2025.

"Waheshimiwa viongozi na wageni waalikwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua kwamba afya bora ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Zanzibar Afya Week 2025 inahusiana moja kwa moja na vipaumbele vya Serikali vilivyobainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 pamoja na Mpango wa Mkakati wa Afya wa Zanzibar III," amesema Waziri Mazrui na kuongeza:

"Katika wiki hii muhimu ya afya, tunatarajia kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha malengo makuu yafuatayo, kuongeza uelewa wa afya kwa Jamii kupitia kampeni za elimu, kambi za afya na huduma za uchunguzi wa magonjwa bure, tutahamasisha wananchi kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa."

Malengo mengine ameyataja ku wa ni kukuza utalii wa Afya na kwamba Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha utalii wa afya na wellness tourism jambo ambalo litaongeza mapato ya nchi na kutoa ajira kwa vijana nchini.

Kadhalika kuboresha ubunifu na teknolojia katika sekta ya afya, kongamano la siku saba ambalo litawapa wadau fursa ya kujadili matumizi ya telemedicine, mifumo ya kidijitali ya afya na mbinu nyingine za kisasa katika utoaji wa huduma za afya.

Ameongeza kuwa lengo lingine ni kuhamasisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP), kwamba watatumia jukwaa hilo kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya, kujenga miundombinu bora ya hospitali, na kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa.

Vile vile kuimarisha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa afya kwani wanatambua changamoto wanazokumbana nazo wahudumu wa afya na ndiyo maana Zanzibar Afya Week 2025 itaweka mkazo kwenye afya ya akili na ustawi wa wafanyakazi wa sekta ya afya.


Ameeleza kuwa kwa Pemba, shughuli zitaanza kwa siku mbili za matukio makuu matatu ambayo ni matembezi ya Afya, Kliniki ya Afya ya Siku Mbili na Kongamano la Fursa za Sekta ya Afya.

Kwa upande wa Unguja, shughuli zitadumu kwa siku saba kuanzia Mei 4 hadi Mei 10, 2025, ambapo kila siku kutakuwa na mada maalum na mijadala kuhusu uboreshaji wa sekta ya afya Zanzibar.

Waziri Mazrui ameongeza kuwa, zaidi ya hayo, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa na huduma za afya, Upimaji wa bure wa magonjwa katika eneo la tukio Nyamanzi, Unguja, kampeni za uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii kuelekea kilele cha wiki hii.


Amefafanua  kuwa uzinduzi wa pili wa Zanzibar Afya Week jijini Dar es Salaam, wakishirikiana na Wizara ya Afya Tanzania Bara, hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Zanzibar kuwa hub ya afya kwa wageni.

"Kwa kweli, Zanzibar Afya Week 2025 itakuwa ya kipekee na yenye historia kubwa kwa Zanzibar. Hatutakiwi kukosa fursa hii! Kwa heshima kubwa, pia tutatoa tuzo maalum kwa watu waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya afya siku ya kilele cha tukio," ameongeza Waziri Mazrui.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wote wa afya, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, vyombo vya habari, na wananchi kwa ujumla kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha Zanzibar inakuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora za afya.

Pia amesema Zanzibar Afya Week 2025 itakuwa hatua muhimu ya mageuzi katika sekta ya afya na itaendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi.

Chapisha Maoni

0 Maoni