Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Waziri Aweso: Ongezeni nguvu tafiti Dodoma wapate maji salama

-Aagiza kuongezwa mitambo zaidi ya uchimbaji visima Dodoma

-Akagua miradi ya maji Nala na Nkuhungu

▪️Miradi ya visima vinavyochimbwa kuzalisha maji lita 32m

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wataalamu wa wizara hiyo kuhakikisha wanaongeza nguvu na kufanya utafiti wa kina wa maji katika Jiji la Dodoma ili kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Jiji la Dodoma.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akipanda katika moja ya matenki ya kuhifadhia maji jijini Dodoma, kufanya ukaguzi katika ziara yake Nara jijini Dooma leo.  

Waziri Aweso ameyasema hayo leo, wakati akikagua miradi ya maji wa Nala unaogharimu Tsh 3.8 bilioni na Uchimbaji wa Visima katika Kata ya Nkuhungu na maeneo mengine ya jiji hilo katika mradi unatoekelezwa ukiwa  na thamani ya Tsh 41 bilioni.

“Ni maelekezo ya Mh. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji jijini Dodoma.Ndio maana zimetolewa fedha zaidi ya Tsh 45 bilioni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa maji. Ninaelekeza wataalamu wa wizara kuhakikisha unafanyika utafiti wa kina wa upatikanaji wa maji Dodoma Jiji kwa kuchimba visima virefu maeneo mbalimbali.

Pia ninaelekeza mitambo ya uchimbaji visima iongezwe hapa Dodoma na ile timu ya wataalamu waliokuwa kwenye usimamizi wa mradi wa Same Mwanga sasa kuhamia Dodoma mpaka tuhakikishe tunaongeza vyanzo vya kutosha vya maji,” alisema Aweso.

Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ameshukuru hatua zinachukuliwa na Serikali kukabiliana na upungufu wa maji na kusema miradi hiyo miwili ikikamilika, itaongeza uzalishaji maji kufikia lita 121 milioni kwa siku, hivyo kubakisha lita 28 milioni kufikia mahitaji ya maji kwa siku.

Akitoa taarifa ya awali, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph,amesema kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa kwa wananchi zaidi ya 184,642 katika maeneo ya Nkuhungu, Mkonze, Miganga, Chidachi, Michese,Iyumbu, Mahungu, Ndachi, Njedengwa, Ng’ong’ona, Mlimwa C na Ntyuka kwa awamu ya kwanza.

Chapisha Maoni

0 Maoni