Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Ripoti CAG: Serikali imepata hasara ya Dola milioni 147 kampuni za madini

-Wakala ununuzi mafuta yakwama uratibu wa bei

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu  za Serikali (CAG), imebainisha kuwa Serikali imepata hasara ya Dola za Marekani milioni 147 sawa  na takriban shilingi bilioni 395.14, zilizolipwa kama fidia kwa kampuni za uchimbaji madini, huku Wakala wa Ununuzi wa Mafuta ukiripotiwa haujatekeleza uratibu wa bei ya mafuta kwa Kampuni za Uuzaji wa Mafuta, hivyo kuweza kuathiri bei za mafuta nchini.

Mdhibiti na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG), Charles Kichere akizungumza katika moja ya mikutano yake na vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa  Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 iliyowasilishwa bungeni wiki hii, Serikali imepata hasara hiyo kutokana na fedha hizo kulipwa fidia kwa kampuni za uchimbaji madini zilizoathiriwa na matumizi ya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Kabla ya kuwasilishwa bungeni, CAG aliwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Dk.SamiaSuluhu Hassan, ambaye baada ya kuipokea, aliagiza kuchukuliwa kwa hatua maeneo yaliyoonyesha kasoro.   

“Kati ya kiasi hicho, Dola milioni 117 (Sh,bilioni 314.5), zimelipwa na kubaki salio la dola milioni 30(Sh. bilioni 80.6), ambazo hazijalipwa,” CAG ameeleza katika ripoti yake.

Matokeo hayo yametajwa kuashiria hatari kubwa za kifedha, ikiwemo uwezekano wa malipo yasiyo na tija yanayotokana na mchakato huo. 

Kuhusu Wakala wa Ununuzi wa Mafuta, Ripoti ya CAG imebainisha kwamba wakala hiyo  imeshindwa kukusanya michango kutoka kwa kampuni za uagizaji wa mafuta zenye gharama za chini za uingizaji au fidia kwa zile zinazoendesha katika bandari zenye gharama kubwa kama Mtwara na Tanga. 

“Matokeo yake, kampuni za uagizaji wa mafuta katika bandari hizi zinakutana na gharama kubwa bila fidia,” inaeleza ripoti hiyo.

Imefafanua kwamba, jambo hilo linaweza kupunguza faida kwa kampuni hizo, lakini pia kuzuia ushiriki wao katika biashara ya mafuta, hatimaye kuathiri ugavi wa mafuta na bei zake nchi nzima. 

 

Chapisha Maoni

0 Maoni