Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji tuzo za waandishi wa habari zinazofahamika kwa jina la "Samia Kalamu Awards", itakayofanyika Aprili 29, mwaka huu jijini Dodoma.
![]() |
Mkurugenzi wa TAMWA,Dk.Rose Reuben (Katikati),akizungumza nawanahabariDar es Salaam.Wengine pichani ni wajumbe wa kamati ya tuzo za wanahabari za kuandika habari za maeneleo. |
Hayo yamesmwa leo Aprili 15, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Dk. Rose Reuben alipozungumza na waandishi wa habari.
Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na TAMWA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni Tuzo Maalum za Kutambua Mchango wao katika kuandika Habari za Maendeleo.
Dk. Reuben amesema tuzo hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuhamasisha na kuthamini kazi za waandishi wanaojikita katika uandishi unaoleta uelewa, hamasa na mabadiliko chanya katika jamii.
Amebainisha kuwa Samia Kalamu Awards ni matokeo ya mafunzo yaliyotolewa kwa wanahabari mwaka 2024, kwa lengo la kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.
“Tunataka kuona habari zinazoibua changamoto lakini pia zikitafuta suluhisho. Hii ni njia mojawapo ya kuonyesha kuwa uandishi wa habari una nafasi muhimu katika maendeleo ya taifa letu,” amesema Dk. Reuben.
Amebainisha kwamba tuzo hizo zimegawanywa katika makundi makuu matatu, la kwanza linahusisha umahiri wa kitaifa pamoja na tuzo maalum kwa waandishi wanawake, maafisa habari wa Serikali na wachapishaji wa mitandaoni.
Kundi la pili linajumuisha vyombo vya habari kama redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii huku kundi la tatu ni tuzo za kisekta zinazohusu maeneo kama afya, maji, elimu, kilimo, mazingira, TEHAMA, uchumi wa buluu, vijana, sanaa, michezo, utalii, na uwekezaji.
Amewataka waandishi wote nchini kushiriki kikamilifu katika tukio hilo, akisisitiza kuwa ni jukwaa muhimu la kutangaza mchango wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ameweka wazi kuwa hafla hiyo itarushwa mubashara kupitia vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii, ili kuwapa wananchi nafasi ya kushuhudia mchango wa wanahabari waliobobea katika kuelimisha na kuleta mabadiliko.
0 Maoni