-Awapa Sh 445 bilioni kutekeleza mradi
-Lita 20 mil kuzlishwa kwa siku
-Maji yamweka Waziri Awesoi Dodoma
-Mbunge Mavunde apongeza Serikali
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameelekeza utekelezaji wa miradi ya maji wenye thamani ya Shlingi Bilioni 445 jijini Dodoma ili kutatua changamoto ya maji jijini humo.
![]() |
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba wa mradi wa maji jijini Dodoma. |
Aweso ameeleza kuwa Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati Jiji la Dodoma likisubiri utekelezaji wa miradi ya kuleta maji kupitia Ziwa Victoria na mradi wa Bwawa la Farkwa.
Ameyasema hayo leo Aprili 15, 2025 wakati akishuhudia utiaji wa saini wa Mkataba wa Mradi wa Kusambaza Maji kupitia visima vya maji vya Nzuguni A, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 5, unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi 123,095.
“Mbunge wenu alileta maombi kwa Mh. Rais Samia juu ya uchimbwaji wa visima virefu wakati wa mkutano wa Mh. Rais pale Mpunguzi na sisi wizara tukapata maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi," amesema Aweso na kuongeza;
"Tunamshukuru Mh. Rais Samia kwa kulivalia njuga suala la maji hapa jijini Dodoma na kuelekeza tutekeleze miradi ya maji ya zaidi Shilingi Bilioni 445 ambayo itasaidia sana kupunguza tatizo la mgao wa maji katika maeneo mbalimbali."
DUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine kama vile Nala (3.8bn), UDOM,(1.2bn), Mji wa Serikali Mtumba (35.6bn).
Wizara ya Maji kwa kushirikiana na taasisi zake (DUWASA na RUWASA) imeunda timu zinazoendelea na utafiti wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa visima katika maeneo ya Mzakwe, Nzuguni, Kisasa, Nkuhungu, Miganga, Zuzu, Msalato na Ihumwa.
"Nipo hapa jijini Dodoma, kesho ntaanza ziara maalum, kukagua utekelezaji wa miradi hii ili wananchi wa Dodoma wapate maji ya uhakika," amesema Aweso.
Naye Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amesema utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji kupitia Nzunguni utasaidia kupunguza adha ya mgao wa maji kwa wananchi wa maeneo ya Nkuhungu, Miganga, Chidachi, Nzuguni, Kisasa-Bwawani, and Mwangaza, Ipagala, Ilazo, na Swaswa, Mpamaa na Njedengwa.
Akitoa taarifa yake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Eng. Aron Joseph amesema mradi huo unalenga kuhudumia watu 123,095 jijini humo.
Kukamilika kwa mradi huo kutaleta ongezeko la uzalishaji maji kutoka lita milioni 81 hadi 91 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 30 kutoka chanzo cha Nzuguni.chenye visima 10, vinavyoweza kuzalisha lita milioni 20 kwa siku.
0 Maoni