Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa wadau wa utalii wa vyakula kuwekeza zaidi katika kuandika vitabu vya vyakula vya kiafrika na machapisho ya kuandaa mapishi, ili kuongeza ujuzi na kupunguza woga kwa watalii wa matumizi ya vyakula wasivyovifahamu.
Dk. Mpango ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Utalii wa Vyakula Barani Afrika, unaofanyika jijini Arusha, ambapo amesema ni muhimu kutangaza vyakula vya kitamaduni vya Afrika kwa kiwango kikubwa, ili utalii wa vyakula hivyo uweze kukua na kustawi.
“Kwa sasa watalii wengi hawana ufahamu wa utajiri wa vyakula vya kitamaduni vilivyopo barani Afrika, vilevile ndani ya nchi za Afrika utalii wa vyakula umewekwa kwa kiwango kidogo kwenye mikakati ya kitaifa ya maendeleo ya utalii,” amesema Dk.Mpango.
Kwa mujibu wa Dk.Mpango katika kukuza utalii wa vyakula barani Afrika,kunahitajika utengaji wa maeneo maalum na njia za kitamaduni, ambapo bidhaa za ndani na vyakula vya kipekee vitatayarishwa kwa ajili ya watalii kufurahia.
Amesema katika njia na vituo hivyo vya chakula, ubora wa vyakula na bidhaa za asili ni lazima kudumishwa na kwamba kunahitajika ushirikiano wa karibu kati ya wapishi wa vyakula vya asili, wazalishaji wa ndani, waongozaji watalii na wadau wengine wa utalii ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa watalii ni endelevu.
![]() |
Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango (Wa pili kushoto waliokaa) na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Pindi Chana (Mwenye suti ya bluu) wakishuhudia burudani ya ngoma ya kiasili wakati wa mkutanohuo. |
Makamu wa Rais ameongeza kuwa, “Ipo haja ya kuweka utalii wa vyakula katika msingi wa utambulisho wa utalii wa Afrika ikiwemo kuimarisha mvuto wake kimataifa kwa kuweka mikakati ya kuunganisha uzalishaji wa chakula, uzoefu wa upishi, na huduma za utalii ili kuwa na athari endelevu za ndani za kiuchumi. vyakula vyetu tajiri, kupika na kula kwa ulimwengu.”
Amesema katika kuhakikisha kunakuwepo na utalii endelevu wa vyakula, Serikali ya Tanzania imeamua kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani wa kilimo ili kutekeleza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayowezesha uhusiano kati ya watalii, soko pamoja na na wazalishaji halisi wa chakula.
Makamu wa Rais amesema utalii wa vyakula una uwezo wa kuboresha hali ya lishe kwa kuwa unatoa mwongozo wa kuandaa chakula ambacho kinavutia na kinachoendana na utamaduni, huku ikihakikisha kuwa vyakula hivyo vinasaidia afya na ustawi akielezakwamba ni muhimu kubadilisha mwelekeo wa kitamaduni wa ladha na uwasilishaji wa chakula kwa afya na uendelevu katika kuoanisha uzuri wa chakula na ufahamu wa afya.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana amesema Utalii wa Chakula una nafasi kubwa ya kuvutia watalii barani Afrika kwa kuwa nchi hizo zimejaaliwa kuwa na mazao mbalimbali, viungo na ladha za kipekee.
Amesema katika kusherehekea umuhimu wa vyakula katika nyanja ya utalii, ni muhimu kuwa na mpango endelevu na jumuishi ikiwemo kuwawezesha wakulima wa ndani, wapishi na wajasiriamali wa chakula kuwa sehemu ya mpango huo.
![]() |
Awali, akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya Tamasha la Utalii wa Chakula, Mwanzilishi wa Tamasha hilo ambaye ni Mwenza wa Rais wa Zimbabwe Dk. Auxilia Mnangagwa amesema kimataifa utalii wa chakula unafahamika kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na uwezeshaji wa kijamii pamoja na kama njia ya kuondoa umasikini.
Mkutano huo wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Utalii wa Vyakula Barani Afrika, unafanyika kwa siku tatu jijini Arusha ukishirikisha wadau mbalimbali wa vyakula kutoka ndani na nje ya bara la Afrika kwa lengo la kuhamasisha fursa zilizopo katika Utalii wa Vyakula kwa maendeleo endelevu.
0 Maoni