Hot Posts

6/recent/ticker-posts

DCEA yakamata kilo 4500 za dawa za kulevya

-Yazuia tani 14 za kemikali hatari kuingia nchini, ingeweza kuua watu bilioni 4   

- Yateketeza ekari 178 za mashamba ya bangi 

Hussein Ndubikile,daimatznews@gmail.com
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola nchini, imekamata kilogramu 4,568 za dawa za kulevya, magari saba, pikipiki tano na bajaji moja kwa kuhusika katika shughuli za usafirishaji wa dawa hizo pamoja na kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akizungumza na wanahabari Dar es Salaam Aprili 25, 2025.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amebainisha hayo alipozungumza na wanahabari Dar es Salaam Aprili 25, 2025, ambapo ameeleza kuwa walifanya ukamataji huo baada ya kufanya oparesheni kubwa katika mikoa kadhaa ya Tanzania ambapo wamefanikisha kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha dawa za kulevya, kemikali bashirifu, magari na watuhumiwa waliokuwa wakijihusisha na biashara hiyo haramu.

"Kwamba watuhumiwa 35 wamekamatwa kutokana na matukio hayo na hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao," amesema KamishnaLyimo.

Amefafanua kuwa operesheni hizo zilifanyika kati ya Machi na Aprili mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha.

Katika hatua nyingine,  Kamishna Lyimo amesema DCEA kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB), imefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu kuingia nchini kinyume cha sheria. 

Amesema kemikali hizo ni pamoja na kilogramu 4,000 za 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za acetic anhydride, zilizotakiwa kuingizwa kutoka Bara la Asia bila kuwa na vielelezo halali vya matumizi.

Lyimo amesema kiasi hicho cha kemikali kingeweza kutumika kuzalisha kilogramu 8,000 za dawa aina ya fentanyl, ambayo kiasi kidogo tu cha miligramu mbili kinaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja. 

"Fentanyl ambayo ingezalishwa, ingeweza kusababisha vifo vya watu bilioni 4. Acetic anhydride nayo ingeweza kutumika kutengeneza kilo 3,704 za heroin au kemikali nyingine hatari kama methamphetamine na mandrax,"amesema.

Amesema katika tukio jingine mkoani Mbeya, raia wa Uganda Herbert Kawalya amekamatwa akiwa na pakiti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu aina ya THC. 

Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo, gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa ikisafirisha pipi hizo kutoka Afrika Kusini nalo limekamatwa,huku mkoani humo pia zikikamatwa kilo 1,658 za bangi aina ya skanka na kilo 128.7 zilizokuwa zikiingizwa kutoka Malawi.

Kwa upande wa Dar es Salaam, Kamishna Lyimo amesema operesheni iliyoendeshwa katika Kata ya Chanika ilikamata kilo 220.67 za bangi aina ya skanka zilizofichwa chooni na kilo 11 nyingine zilipatikana katika eneo la ukaguzi wa mizigo bandarini kuelekea Zanzibar.

Amesema katika mikoa ya Arusha, Tanga, na Manyara zilikamatwa kilo 733.74 za methamphetamine, kilo 91.62 za heroin, kilo 692.84 za mirungi kutoka Kenya na kilo 115.05 za bangi, pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi. 

"Mkoani Tabora katika Wilaya za Uyui na Nzega, kilo 845 za bangi zilipatikana na ekari 176 za mashamba ya bangi ziliharibiwa. Shinyanga na Kahama tulikamata watuhumiwa wakiwa na kilo 98.35 za bangi," amesema Kamishna Lyimo.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu na taasisi za ndani na nje ya nchi, hivyo kuzuia athari kubwa kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira ambazo zingeletwa na dawa hizo mitaani. 

"Hapo unaweza kuona kwamba tumeokoa maisha ya mamilioni ya vijana ambao wangepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo," ameongza.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa mapema kuhusu shughuli za uzalishaji au biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga simu bure namba 119, huku akiwataka wazazi na walezi kuwa makini na mienendo ya watoto wao na kuwapa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Kwa upande mwingine, kampuni zinazotumia kemikali za viwandani na kilimo zimekumbushwa kuzingatia sheria na kuepuka kushirikiana na magenge ya kihalifu yanayochepusha kemikali hizo kwa ajili ya kutengeneza dawa za kulevya


Chapisha Maoni

0 Maoni