- Majengo mapya yaota kama uyoga
- Wazawa wawekeza
- Kitabu cha zama mpya kinaandiwa
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Kila zama ina kitabu chake; hayo si maneno yangu, bali ni msemo wa lugha adhimu ya Kiswahili, linaloweza kutafsiriwa kwamba, kila jambo lina historia yake. Ndivyo ilivyo kwenye maisha ya binadamu anapotekeleza mipango na malengo yake binafsi au ya jamii inayomzunguka, ili kupata manufaa au tija tarajiwa.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa namna ya pekee katika historia yake liliingia katika zama za ubia Novemba 16, 2022, kwa kumwalika Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), aliyeizindua sera yake ya ubia iliyoboreshwa, ikilenga kufungua milango kwa wawekezaji binafsi kushirikiana na shirika hilo kuendeleza maeneo ya mijini kwa kujenga makazi bora na ya kisasa ya watu, pia majengo ya biashara.
Hata hivyo, Sera ya Ubia si mpya sana kwa NHC kwani kati ya mwaka 1993 hadi 2010, shirika hilo lilitekeleza mirai 194 likishirikiana na wawekezaji binafsi. Lakini, tofauti iliyopo sasa na mwaka1993 hadi 2010 ni namna ya utekelezaji ubia.
Hakuna ubishi kwamba utekelezaji sera ya ubia kwa sasa unalenga kuhakikisha wananchi wa kawaida na taifa kwa ujumla linanufaika, kukiwa pia na usimamizi thabiti zaidi na uwazi zaidi, huku eneo la Kariakoo lililo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, likichaguliwa kama moja ya maeneo muhimu ya utekelezaji Sera ya Ubia.
Zipo sababu nyingi za uamuzi huo wa NHC kuchagua eneo la Kariakoo. Lakini kwa uchache, hakuna wa kupinga kwamba Kariakoo imebeba historia kubwa kwa Jiji la Dar es Salaam, hata Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwani ndilo eneo kubwa la kibiashara.
Ukweli huo unapambwa sio tu na eneo hilo kuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam, bali pia linafikika kirahisi likikutanisha wafanyabiashara na wanunuzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mazingira hayo, hakuna shaka kwamba ardhi ya Kariakoo ina thamani kubwa, pia ni kitovu cha kibiashara chenye mvuto zaidi Afrika Mashariki.
Hali hiyo pia ndiyo inayovutia wawekezaji wa ndani na nje, ikiwamo NHC kuthubutu kuwekeza Kariakoo bila hofu, ambapo sasa shirika hilo linamiliki majengo mbalimbali yenye thamani kubwa na ndogo, yakiwa na ubora mkubwa uliowapa fursa watu wa kada tofauti kuishi na kufanyabiashara kwa kulipa kodi NHC.
Hatua hiyo pia huiwezesha NHC kulipa kodi mbalimbali za Serikali, hata kuchangia katika pato la taifa kwa kulipa gawio serikalini.
![]() |
Baadhi ya majengo mapya yanayojengwa na NHC Kariakoo. |
Hakuna wa kupinga kwamba Kariakoo inasimama kipekee kuwa eneo muhimu kwa jamii kiuchumi, ambapo maelfu ya watu hutimiza ndoto zao za kimaisha kupitia ukazi au biashara wanazofanya.
Lakini pia sasa mvuto kwa Kariakoo umeongezeka na kufanya eneo hilo kung’ara sababu kubwa ikiwa uwekezaji wa ubia kati ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambalo ni la umma linalojiendesha kibiashara. Ikumbukwe kuwa NHC lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge.
Uthubutu wa NHC
Shirika la Nyumba la Taifa, sasa linalipitisha eneo la Kariakoo katika mabadiliko makubwa yanayolenga kulipa hadhi ya kisasa, kuimarisha shughuli za biashara na kuboresha maisha ya watu.
Hili linafanyika kupitia utekelezaji wa Sera ya Ubia, ambayo ni ushirikiano kati ya NHC na sekta binafsi kwa lengo la kujenga majengo ya biashara na makazi.
Si jambo la kushangaza kwamba kwa inachofanya Kariakoo, NHC inajenga taswira ya kitaifa na kulifanya eneo hilo kuongeza heshima na thamani yake ndani na nje ya Tanzania.
![]() |
Kariakoo inavyoonekana kutoka juu. |
Mwonekano wa sasa wa Kariakoo ambayo kiutawala ni Kata ndani ya Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam unavutia watu wa kada mbalimbali, ukujumuisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya eneo hilo, hata kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, watalii wanaofuata historia na wawekezaji wanaotafuta fursa yenye sifa za kipekee.
Kariakoo sasa inakuwa mpya kila kukicha kutokana na kuchomoza kwa maghorofa mapya yenye urefu zaidi kuliko yaliyojengwa awali. Si hivyo tu, bali maghorofa ya sasa hasa yaliyojengwa na NHC, yamebuniwa na kujengwa kisasa zaidi yakibeba mandhari ya kuvutia yanayojumuisha hadhi tofauti katika jengo moja.
Pia viwango vya juu vilivyobeba nakshi za kuvutia, yakiwa na makazi ya watu, ofisi za biashara, maduka na maegesho ya chini ya ardhi, yakiwa pia na lifti za kisasa na mifumo ya usalama wa uhakika.
Umaridadi na usasa wa Kariakoo, umeongeza umaarufu wa eneo hilo, likivutia zaidi mithili ya Dubai ndogo, inayokutanisha watu kutoka kona mbalimbali za Dunia ambao hufika kutafuta biashara, kutalii hata kuwekeza.
Hapana shaka NHC inazidi kuifanya Kariakoo kuwa mpya na kuvutia zaidi wawekezaji, wafanyabiashara hata watalii kwani ni mahali pa kisasa, salama panapobeba funguo za ndoto za maisha za watu wa nyanja tofauti.
Miradi hiyo inayotekelezwa na NHC ni sehemu ya mchango wa shirika hilo katika kutekeleza Dira ya Taifa 2025 na maelekezo mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Sita, ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, (Deo Ndejembi).
NHC na Wazawa
Kwa uhakika, NHC ni maneno kidogo na kazi zaidi. Ndivyo ilivyo, kwani pamoja na majengo mengine madogo inaweka hadharani miradi mitano mikubwa ya majengo inayotekelezwa Kariakoo. Unaweza kusema Kariakoo majengo yanaota kama uyoga.
Mfano wa majeno hayo ambayo pia yanahusisha wawekezaji wazawa kuwa ni pamoja na Mwigomelo Co Ltd ambao sasa ghorofa ya 11 imekamilika, huku umaliziaji ukiendelea. Jengo la ITEL East Africa Ltd ni la pili, ambalo sasa liko kwenye ghorofa ya sita, huku upigaji plasta na uwekaji milango ukiendelea.
Tatu ni jengo la Salala Solution Ltd la ghorofa nane ambalo limekamilika na sasa linaendelea kupakwa rangi, kuwekwa vigae, huku wateja hasa wafanyabiashara wakiwa tayari wameanza kufanyia biashara zao.
Jengo la nne ni la Tanzanite Forever Lapidary Ltd. Tayari msingi wa jengo hilo umekamilika, huku zinaendelea kazi mbalimbali hadi ghorofa ya nne na jengo la mwisho ni la Baba’s Electronics Co Ltd, uliofikia ghorofa ya nane, huku ghorofa za chini zikiwa zimekamilika.
Majengo yaota kama uyoga
Kwa mujibu wa NHC, miradi 16 kati ya 20 iliyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa NHC imetekelezwa Kariakoo, ikuhusisha wapangaji 172 wa zamani, huku miradi 61 ikiidhinishwa awamu ya pili.
Kati ya hiyo, miradi 44 ipo Kariakoo, jambo linalodhihirisha Kariakoo kuvutia wawekezaji. Takwimu hizo zinaonyesha jinsi majengo yanavyoota kama uyoga Kariakoo, NHC ikibeba dhima kuifanya Kariakoo kama Dubai ndogo, ambapo wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali za kiuchumi hukutana na kunufaika kimaslahi, huku pia shirika na taifa vikinufaika kiuchumi.
![]() |
Wataalam husema picha inaongea maneno elfu moja, ndivyo ilivyo. Hapa picha ikionyesha ushuhuda wa wingi wa majengo mapya eneo la Kariakoo. |
NHC na Wapangaji
Shirika la Nyumba la Taifa limekuwa likitekeleza miradi hii kwa kujali maslahi ya wapangaji wa zamani. Ingawa sheria inaruhusu kutoa notisi ya siku 30 kwa wapangaji kuondoka, NHC inatoa notisi ya siku 90 na kwa baadhi ya wapangaji imeongeza hadi mwaka mmoja ili kuwapa muda wa kujipanga.
Zaidi ya hapo, wapangaji wamehakikishiwa kipaumbele cha kurejea kwenye majengo mapya, pindi ujenzi unapokamilika. Hii inaonesha kuwa NHC inazingatia utu, haki na uhusiano mzuri na jamii.
Faida
Miradi ya ubia ya NHC inaleta faida mbalimbali kwa ngazi zote, ikiwamo wananchi wa kawaia kupata fursa ya kufurahia makazi bora yenye usalama wa kuaminika, maeneo ya huduma za kisasa, sehemu za biashara, maegesho, lifti, pia miundombinu bora.
Kutokana na miradi hiyo, Serikali inakusanya kodi ya ardhi, majengo huku pia wananchi hasa vijana wakinufaika na ajira kupitia sekta ya ujenzi.
Miradi hiyo imewapa wawekezaji faida ya kupata ushirikiano wa haki na NHC, uhakika wa faida kwao, mazingira bora ya kutumia vyema mitaji.
![]() |
Sehemu ya majengo ya biashara Kariakoo yanayotoa tumaini jipya la makazi bora. |
Hii ndiyo Kariakoo Mpya inayochomoza upya kama Dubai kwa uwekezaji wa pamoja kati ya NHC na watu binafsi, inayoandika kitabu kipya cha zama zake katika NHC kuwapatia watanzania pambazuko jipya kwa kupata makazi bora ya kisasa.
Katika Kariakoo ya sasa ndipo wajasiriamali na wasomi hata wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, wanapoweza kukutana hata kupanga na kutekeleza mipango yao, bila kusahau familia zilizopata makazi ya kuishi eneo hilo.
Kwako wewe unayetaka kuwekeza au kushirikiana na shirika hilo, fursa bado zipo, la kuzingatia ni kuwasiliana na Shirika la Nyumba la Taifa, ili kuendelea kuwa sehemu ya historia nzuri inayojengwa na NHC nchini.
0 Maoni