Hot Posts

6/recent/ticker-posts

'Kocha wa makipa Simba', wenzake wakana mashtaka dawa zakulevya

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MSHTAKIWA Saidi Matwiko na mkewe Sarah Joseph wamekana kukutwa na dawa za kulevya wakati upekuzi ulipofanyika nyumbani kwao Kivule katika Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.


Matwiko na Sarah wamekana maelezo hayo waliposomewa mashtaka na maelezo ya awali katika mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya na wenzao wanne pamoja na aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Timu ya Simba Muharami Sultani.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu mbele ya Jaji Godfrey Isaya  Februari 5,2025.

Watuhumiwa hao wanashtakiwa wakidaiwa kuongoza genge la uhalifu, kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 34.89.

Pia mmiliki wa Ktuo cha Michezo cha Cambianso, kilichoko Tuangoma, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Kambi Zubery anashtajiwa kwa kutakatisha fedha ambapo anadaiwa kujipatia magari matano aina ya Tata huku akijua Mali hiyo inatokana na zao la kuongoza genge la Uhalifu.

 Akiwasomea mashtaka watuhumiwa hao, Wakili wa Serikali Tully Helela amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka nane ambapo inadaiwa, wote kati ya Mwaka 2016 na Novemba 2022 maeneo ya Dar es Salaam na Mkuranga waliongoza genge la Uhalifu na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.

Imeadaiwa mahakamani hapo kwamba Oktoba 27, 2022  maeneo ya Kivule , Ilala mkoani  Dar es Salaam, washtakiwa wote walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilogramu 27.10. 

Pia ilidaiwa kwamba Novemba 4, 2022, eneo la Kamegele Mkuranga, wote kwa pamoja walikutwa wakisafirisha kilogramu 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroine.

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo Kambi anakabiliwa na mashtaka  matano ya kutakatisha fedha, alijipatia magari matano aina ya Tata wakati akijua mali hizo zimetokana na mazalia ya kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Kambi, Sultani, Maulid Mzungu, maarufu Mbonde, Said Matwiko, John Andrew maarufu Chipanda ambaye ni mfanyakazi wa Cambiasso na Sara Joseph ambaye ni mke wa Matwiko. 

Katika usikilizwaji wa awali  wa shauri  hilo, Wakili Tully alidai maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya wakiwa kwenye doria maeneo ya Kivule walipata taarifa ya watu wanasafirisha dawa za kulevya.

Alidai maofisa walikwenda  nyumbani kwa mshtakiwa Saidi Matwiko na kundi lingine lilielekea Kitunda Magole kwa mshtakiwa John.

Ilidaiwa katika upekuzi nyumbani kwa Saidi walikuta pakiti 27 zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya, mshtakiwa Saidi na Sarah walikamatwa na vielelezo vilipelekwa kwa mkemia kwa ajili ya uchunguzi ambako ilibainika ni dawa za kulevya aina ya heroine.

Ilidaiwa pia upekuzi ulifanyika nyumbani kwa washtakiwa wengine wote na nyumbani kwa Maulid walikuta pakiti nane za dawa za kulevya.

Akijibu, mshtakiwa Kambi alidai upekuzi ulipoanyika nyumbani kwake hakuwepo na zilichukuliwa Sh milioni tisa na gari.

Alidai hakukamatwa katika mpaka wa Horohoro Tanga akitaka kukimbilia Kenya, bali alikamatwa maeneo karibu na Horohoro.

Naye mshtakiwa Kambi alikana kuwafahamu washtakiwa wengine wote, lakini mshtakiwa wa pili na watatu walikubali kwamba wao ni ndugu na mshtakiwa wa nne alikubali kwamba mshtakiwa wa sita ni mke wake.

Mshtakiwa wa nne katikashauri hilo Saidi alidai upekuzi ulipofanyija nyumbani kwake hawakukuta kitu chochote.

Kwaupande mwingine mke wa Saidi, Sara alidai wakati wa upekuzi hakuwepo nyumbani na kwamba alikamatwa mchana, wala hakukamatwa pamoja na mumewe kama inavyodaiwa.

Upande wa Jamhuri una jumla ya mashahidi  30 na vielelezo 90 kwa ajili ya kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni