Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mnigeria wa dawa za kulevya waachiwa huru

 DPP asema hana nia kuendeleza kesi 

Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP) ameiomba Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imwachie huru raia wa Nigeria Emmanuel Chiabo na mwenzake wanaoshtakiwa kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine Kilogramu 29.71 sababu hawana nia ya kuendelea na shauri hilo.


Mahakama mbele ya Jaji Godfrey Isaya imepokea maombi hayo na kukubali kuondoa shtaka dhidi ya Chiabo na Goodness Remy.

Wakili wa Serikali Glory Kilawe akiwakilisha Jamhuri aliwataja washtakiwa kuwa ni Chiabo na Goodness Remy ambao walishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.

"Mheshimiwa shauri lilikuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa mashtaka na usikilizwaji wa awali lakini Jamhuri tunaomba kuondoka shtaka chini ya kifungu namba 91(1) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022,"alidai.

Alidai kuwa washtakiwa wanadaiwa Aprili 19 mwaka 2023 maeneo ya Salasala, Mtaa wa Upendo wilayani Kinondoni walisafirisha heroine kilogramu 29.71.

Wakili Glory aliomba Mahakama ikubali kuondoka shtaka kama walivyoomba.

 Wakili wa utetezi Hardson Mchau akijibu alidai hana pingamizi isipokuwa anaomba endapo Serikali itaamua kuwashtaki tena iwarudishwe mahakamani mapema.

Jaji Isaya baada ya kusikiliza maombi ya Jamhuri na majibu ya upande wa utetezi alikubali kuwaachia huru washtakiwa.

"Mahakama inawaachia huru washtakiwa wote wawili , tunawajulisha kuachiliwa kwenu  huru chini ya kifungu cha 91(1) hakuzuii kushtakiwa tena kwa kosa mliloachiwa,"alisema Jaji Isaya.

Washtakiwa wote wamwachiwa huru.

Chapisha Maoni

0 Maoni