Polisi yawaonjesha 'shubiri' madereva walevi mwaka mpya 2025

  -Yawafungia leseni miezi 6

 - 30 wakamatwa Krismasi na Mwaka Mpya Dar, wengine 2 wahukumiwa jela maisha


Na Hussein Ndubikile, daimatnews@gmail.com
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewafungia leseni za udereva kwa kipindi cha miezi sita, madereva waliokamatwa  wakiendesha magari huku wakiwa na kiwango kikubwa cha ulevi kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro (Pichani juu),amebainisha hayo Januari 3,2 025 alipozungumza na wanahabari jijini humo, ambapo ameeleza hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu 28 (3) (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura 168 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeuanza Mwaka 2025 vizuri na sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zilikuwa za amani na utulivu. Hata hivyo usimamizi wa Sheria na kanuni mbalimbali zikiwemo za usalama barabarani zilisimamiwa kikamilifu ili kudhibiti ajali za barabarani," amesema SACP Muliro na kuongeza;

"Katika kipindi hicho cha sikukuu, makosa hatarishi ambayo yangesababisha ajali yalidhibitiwa na hatua kuchukiliwa kwa wahusika. Jumla ya madereva 179 walituhumiwa na kupimwa ulevi, kati yao madereva 30 walikutwa na ulevi wa kiwango cha zaidi ya milligramu 80,"

Muliro amesema kati yao madereva 22 walitokea Wilaya ya Kinondoni, sita (6) Wilaya ya Ilala na madereva wawili (2) Wilaya ya Temeke.

Katika hatua nyingine SACP Muliro ameeleza kuwa katika kipindi cha Novemba hadi Desemba 2024, Jeshi hilo lilifanikiwa kupata matokeo mahakamani ya watuhumiwa mbalimbali.

Ametaja miongoni mwao kuwa ni Sadick Foreni (30) mkazi wa Mbagala ambaye Mahakama ya Wilaya ya Temeke ilimuhukumu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.

Mahakama hiyo pia ilimuhukumu Joseph Ferdinand (35) mkazi wa Mbagala Kibonde Maji kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.

SACP Muliro amebainisha kuwa naye Ayub Hatibu (32) mkazi wa Tabata alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kinyerezi  kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka, huku Salmin Athuman (30) makazi wa Kitunda akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Ameongeza kuwa Henry Peter (36) mkazi wa Mbezi wa Dar es Salaam alhukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kubaka, huku Ramadhan Amir (30) mkazi wa Kawe akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro jumla ya watuhumiwa 250 walikamatwa kwa kuhusika na kuuza, kusafirisha na kutumia Dawa za Kulevya.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi

Moshi mweusi watokea Vatican, moshi mweupe wasubiriwa kwa hamu