-Utendaji wa Bandari nchini waimarika kwa kipindi cha miezi saba (Mei-Novemba 2024) ikilinganishwa na (Mei-Novemba 2023)
![]() |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumzia kuimarika kwa utendaji wa bandari nchini. |
Utendaji Bandari Dar es Salaam Katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 hadi Novemba 2024, kiwango cha shehena kilichohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam ni tani milioni 14.4 ambayo ni zaidi ya asilimia 5.6 ya shehena milioni 13.7 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).
Shehena ya Makasha (Containers-TEUs) Idadi ya Makasha yaliyohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam katika kipindi cha Mei 2024 hadi Novemba 2024 ilifikia makasha (TEUs) 598,672 sawa na ongezeko la asimilia 0.2 ya makasha (TEUs) 597,613 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).
Shehena za nchi jirani Bandari Dar es Salaam Katika kipindi cha Mei, 2024 hadi Novemba 2024 ilihudumia shehena ya nchi jirani (Transit) tani milioni 6.3 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 19.3 ya shehena ya nchi jirani iliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023) ambayo ilikua tani milioni 5.3. ikiwa kubwa kuliko ya kipindi kama hicho mwaka 2023.
Mafanikio uwekezaji DP World Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilisaini mikataba mitatu ya uwekezaji na Kampuni ya DP World (Dubai) Oktoba 22, 2023.
Mkataba huo ulihusisha uendeshaji wa shughuli za bandari katika uhudumiaji wa makasha, mizigo mchanganyiko na shehena ya magari.
Ili kutoa huduma hizi kwa kuzingatia sheria za nchi yetu, Kampuni ya DP World ilifungua kampuni ya Tanzania inayoitwa DP World Dar es Salaam iliyokabidhiwa rasmi shughuli za uendeshaji wa bandari 15 Aprili, 2024.
Tangu kampuni hii ianze uendeshaji wa shughuli za bandari mafanikio mbalimbali yamepatikana kama ifuatavyo: Kwa mujibu wa mkataba, Kampuni ya DPW inapaswa kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 250 (Sh. Bilioni 675) katika kipindi cha miaka mitano.
Katika kipindi cha miezi mitano tayari wameshawekeza Sh.214.425 Bilioni (31%) kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa; ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA; na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa bandari.
Wastani wa muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 mwezi Mei 2024 hadi kufikia wastani wa siku saba (7) ikiwa ni siku 0 kwa meli za makasha; siku 12 kwa meli za kichele; na siku 10 kwa meli za mizingo mchanganyiko.
Kutokana na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo, muda wa kuhudumia meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3), hivyo kupunguza idadi ya meli zinazosubiri kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.
Katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni.
Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya Sh. Billioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrahaba (royalty), na Ardhia (warfage).
Kutokana na kuongezeka kwa mapato na kupungua kwa gharama za uendeshaji kufuatia maboresho yaliyofanyika, Serikali, kupitia TPA, imeanza uwekezaji katika miradi yenye thamani ya Sh. 1.922 Trilioni (USD 686.628 milioni) kwa kutumia makusanyanyo yanayopatikana.
Miradi hii ni Ujenzi wa Kituo cha Kupakulia Mafuta (SRT); Ujenzi wa Bandari ya Kisiwa Mgao (Mtwara); na Ujenzi wa Gati za Majahazi (Dhow Wharf) Dar es Salaam.
Kuunganishwa kwa mifumo ya Forodha (Tanzania Customs Integrated System - TANCIS) na ile ya bandari (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS).
Hii imewezesha kupunguzwa na kuondolewa kwa mifumo iliyokuwa inafanana, hivyo kupunguza muda wa kuondoa mizigo bandarini, kuongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano.
Mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka hadi kufikia Sh. Trilioni 1 mwezi Septemba 2024 ikilinganishwa na wastani wa Sh. 850 bilioni kwa mwezi. Hii imetokana na TRA kuweza kuchakata mizigo mingi zaidi ndani ya muda mfupi.
Kwa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa kwa DP World na kampuni nyingine kuiendesha, yanaonesha kuwepo faidi kubwa kiuchumi kwa kuchochea kuongezeka kwa biashara na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Uwekezaji huu ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa azima ya Serikali ya kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa Lango Kuu la usafirishaji mizigo katika ukanda wa Afrika. Bandar ya Tanga Kwa upande wa Bandari ya Tanga , Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi Bilioni 429 kwa awamu mbili kuboresha bandari ya Tanga hatua ambayo imeongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutokana na wingi wa shehena inayopita katika bandari hiyo.
Katika kipindi cha miezi mitatu ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha 2024/25, Bandari ya Tanga imevuka lengo kwa kukusanya mapato kiasi cha Sh. Bilioni 18.6 ambayo ni zaidi ya lengo lililowekwa la kukusanya Sh. Bilioni 11. Mapato hayo ni zaidi ya mapato yote yaliyokusanywa katika mwaka wa fedha 2019/2020 ya kiasi cha Sh. Bilioni 16.
Amesema meli zenye ukubwa tofauti zimekua zikitia nanga katika bandari hiyo, hatua inayoongeza kiwango cha bidhaa na shehena ambazo awali zilikua hazipiti katika bandari hiyo zikiwemo shaba (copper) tani 33,000, Ammonium nitrate tani 41,000 na Sulphur tani 100,004
0 Maoni