Uchaguzi TAMISEMI; Warioba aonya, ‘amgusa’ Rais Samia
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika nchini hivi karibuni, uligubikwa na kasoro alizosema zinajenga mazingira ya kuhatarisha amani ya taifa, akimtaka Rais Samia kuchukua hatua kubwa.
![]() |
Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza na wahariri wa vyombovya habari, kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), jijini Dar es Salaam Desenba 4, 2024 |
“Mwaka 2019 tuliona, badala ya Serikali kulinda wananchi wake na kuzingatia masharti na sifa za wagombea, watu walienguliwa, si sababu ya pingamizi, bali waliosimamia uchaguzi ndio waliamua. Tuliona walienguliwa na waliotakiwa kulinda haki...; hata juzi yametokea yale yale, chanzo chake ni wasimamizi wa uchaguzi,”amesema Warioba na kufafanua;
“Kama tukiendelea na hali hiyo tutakuwa tunajenga mazingira ya kuvuruga amani. Haiwezekani wagombea wanaoenguliwa ni wa vyama vingine, eti wote wamekosea kujaza fomu, wa CCM wote wanajua. Haiwezekani wananchi waamini eti wanaoenguliwa ni wagombea wa upande mmoja tu.”
Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kukukusanya Maoni kuhusu Katiba Mpya, amesema hayo leo Desemba 4, 2024 jijini Dar es Salaam, katika mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akionya kuwa kama taifa halitachukua hatua kufanya mabadiliko, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, utakuwa kama wa TAMISEMI.
![]() |
Wahariri wa vyombo habari mbalimbali, kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), wakimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba walipokutana naye, jijini Dar es Salaam Desenba 4, 2024 |
Huku akiwaomba
viongozi wa vyana vya siasa nchini, kuweka kando maslahi binafsi na ya vyama vyao,
badala yake watangulize maslahi ya taifa, amewashauri viongozi hao kukutana na kutafuta
suluhu ya matatizo yaliyojitokea katika uchaguzi wa TAMISEMI.
“Tusipochukua hatua, Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2025 utakuwa kama wa TAMISEMI, tukiendelea hiviamani tuliyonayo itakufa, mimi
naogopa kabisa... kama taifa tuangalie, moja ya mambo ya kufanyika ni Rais achukue
hatua kwa kiwango kikubwa.”
Maoni
Chapisha Maoni