Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Morocco Square: Alama mpya ya maisha ya kisasa Dar

-Mambo yote Dar sasa Morocco Square

-Kuingiza Shilingi Bilioni 9 kwa mwaka

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Morocco Square, moja ya miradi ya kifahari na kipekee nchini Tanzania uliotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), sasa umekamilika ukiwa ndio alama mpya ya maisha ya kisasa jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya jengo la kisasa Morocco Sqare linavyoonekana 

Alama hiyo kubwa ya aina yake, imejengwa katika makutano ya Barabara za Mwai Kibaki, Ali Hassan Mwinyi na Ursino eneo la Regent Estate, wilayani  Kinondoni, umezingatia mambo yote muhimu yanayohitajika kwa maisha ya mwanadamu anayeishi kisasa.

Kupitia mradi huo wa kipekee, NHC imejenga majengo manne kwenye msingi mmoja,  jengo moja likiwa ni hoteli, la pili ofisi mbalimbali, jengo la tatu ni la biashara na la nne ni makaziya watu.

Huu ni ukweli halisi wa mradi  huo uliozinduliwa Novemba 23 mwaka huu kwani unapotembelea eneo  hilo utashuhudia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya kibiashara, makazi na burudani. Vyote vikiwa katika eneo moja, hivyo kuvutia wawekezaji na wakazi wa jiji hilo kufika hapo, kufanya manunuzi, hata kufurahia maisha. Unaweza kusema mambo yote Dar sasa Morocco Square. 

Jengo hilo linalojulikana kwa jina la Morocco Square lililojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 137 ni alama mpya ya kazi nzuri zilizofanywa na NHC Dar es Salaam na Tanzania nzima linalobeba nyumba za makazi, ofisi, maeneo ya biashara na burudani yakiwa kwenye msingi wa jengo moja.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Ahmad Abdallah (Kushoto), akisalimiana na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu katika moja ya matukio yaliyowakutanisha. Mchechu aliwahi kuiongoza  NHC.

 Hakuna wa kubisha kwamba Morocco Square ni ishara ya maendeleo ya kisasa nchini, ikiwa ni mradi wa matumizi mchanganyiko unaojumuisha majengo manne makubwa: mawili kwa ajili ya ofisi, moja kwa ajili ya makazi na lingine kwa ajili ya hoteli.

Majengo haya yameundwa kwa viwango vya juu ili kutoa nafasi bora za kibiashara na makazi yenye huduma za hali ya juu na kisasa zaidi.

Morocco Square inajivunia majengo mawili ya ofisi yenye ghorofa 22 na 19, yanayojumuisha maduka kwenye ghorofa za chini hadi ya pili, huku nafasi za ofisi zikianzia ghorofa ya tatu na kuendelea.

Majengo hayo yanatoa mandhari ya kuvutia  yanayofaa kwa kampuni kubwa, biashara za kitaifa na kimataifa, pia kampuni zenye kuhitaji mazingira ya kazi ya kisasa na yenye miundombinu yenye ubora wa hali ya juu.

Pia kuna jengo la maduka lenye ngazi tatu, likichukua mita za mraba 28,873, likiwa na maduka mbalimbali ya vyakula, mavazi, mitindo, na maeneo ya burudani.

Ndani ya Morocco Square wateja wanaweza kufurahia sinema, vyumba vya michezo kwa watoto na huduma mbalimbali zinazoongeza mvuto wa mradi huo kwa familia na watu wa rika zote.

Kwa upande wa makazi, Morocco Square inatoa fusra tofauti za kuchagua zinazokidhi mahitaji ya makazi ya kisasa katika mradi unaojumuisha vyumba vya kulala vitatu na vinne, duplex na vyumba vya kifahari vya ghorofa ambavyo vinafaa kwa wakazi wanaotafuta maisha ya hadhi ya juu na yenye faraja jijini.

Hoteli na Huduma za ziada

Jengo la hoteli lenye ghorofa 16 na vyumba 81 vya studio linawapa wageni wa muda mfupi na mrefu mahali pa kupumzika panapotoa burudani na starehe kamili. Hoteli hii inayoendeshwa na kampuni ya Kihindi inatoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku ikichangia katika kukuza sekta ya utalii na biashara jijini Dar es Salaam.

Morocco Square pia imejengwa kwa ajili ya huduma za kisasa zaidi, ikiwemo nafasi za maegesho zinazochukua magari zaidi ya 2,000, eneo la kutua helikopta, bwawa la kuogelea, klabu ya burudani, maduka ya kahawa, likiwa pia na jenereta za dharura na mfumo wa usalama wa hali ya juu. Hizo zote ni huduma zinazofanya eneohilo kuwa na mazingira bora na salama kwa wapangaji na wateja.

Uwekezaji wenye faida kwa wawekezaji

Kwa Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC), mradi huu ni zaidi ya jengo, ni uwekezaji mkubwa utakaozalisha wastani wa mapato yanayofikia Shilingi milioni 850 kila mwezi  kila mwezi kutoka kwa wapangaji, hivyo kufikisha takribani Shilingi bilioni 9 kwa mwaka.

Mwonekano wa nje wa Moocco Square

Mapato hayo ni sehemu ya mkakati wa NHC wa kuhakikisha Serikali inarejesha fedha zake kupitia mapato yanayotokana na mradi huu.

Morocco Square pia inatoa fursa za kipekee kwa wawekezaji kutokana na kuwa eneo lake la kipekee katikati ya jiji, pia ukaribu wake na huduma muhimu za kijamii.

Eneo hilo linavutia wateja wa viwango vyote, wakiwemo wafanyabiashara, familia, hata watalii kutokana na mazingira bora ya biashara, makazi na burudani.

 Morocco Square inathibitisha jinsi Tanzania inavyoendelea kuwa na miradi ya kisasa inayofikia viwango vya kimataifa,ukiwa ni mradi wa kwanza wa aina yake nchini, unaochanganya vyema matumizi mbalimbali katika eneo moja, hivyo kuwa sehemu muhimu katika ujenzi wa jamii yenye uhai jijini Dar es Salaam.

Kwa NHC, kukamilika kwa Morocco Square ni kielelezo cha mafanikio ya utekelezaji wa sera za Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zinazolenga kuongeza thamani ya mali na kutoa huduma bora kwa Watanzania. Morocco Square inatoa mwaliko kwa wakazi na wageni kufika eneo hilo ili  kufurahia mazingira ya kisasa na fursa tele zinazopatikana hapo.

 

 


Chapisha Maoni

0 Maoni