Tanzania,EU zakubaliana kuunga mkono maendeleo

 

Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com 

Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) zimesaini Tamko la Makubaliano ya Kuendelea Kuunga Mkono Jitihada za Maendeleo kwa faida za pande zote mbili.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi baada ya kusainiwa kwa tamko hilo Desemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam amesema ushirikiano huo ni wa muhimu kwa pande zote.


“Majadiliano haya ya leo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Samoa, uliosainiwa mwaka 2023, ambao unaelekeza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya Umoja wa Ulaya na Nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki (ACP). “ amesema.

Amesema kuwa Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa kundi la ACP, ambayo inaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kushiriki kikamilifu kwenye majadiliano hayo muhimu kila mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Umoja wa Ulaya.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi(katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Kanda ya Afrika katika Kurugenzi ya Huduma za Nje ya Umoja wa Ulaya (Europeana External Action Service), Balozi Ritha Maria Laranjinha (kushoto) wakisaini hati za makubaliano.

Chumi amebainisha kuwa majadiliano hayo yalijielekeza zaidi katika masuala yanayogusa maslahi ya pande zote, ikiwa ni pamoja na utawala bora, demokrasia, usalama wa baharini, biashara na uwekezaji, na ulinzi na usalama kikanda na kimataifa.

Chumi ameyataja baadhi ya maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano huo ambapo alisema kuwa Tanzania na Umoja wa Ulaya zimedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili chini ya Mkataba wa Samoa. 

Ushirikiano huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020- 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambapo pande zote mbili zimekubaliana kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha matokeo chanya na yenye manufaa kwa wananchi.

Baadhi ya  wajumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) wakifuatilia hafla ya utiaji saini makubaliano baina ya umoja  huo na Tanzania.

Aidha Chumi kwa niaba ya Tanzania aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wake endelevu kupitia mfumo wa mpango wake wa maendeleo wa majirani na ushirikiano wa kimataifa ambao umeweka Euro 726 Milioni kwa Tanzania.

Amefafanua kuwa fedha hizo zimewezesha kutekeleza miradi muhimu katika sekta ya nishati, uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabia nchi na mpango wa miji kuwa ya kijani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Kanda ya Afrika katika Kurugenzi ya Huduma za Nje ya Umoja wa Ulaya (Europeana External Action Service), Balozi Ritha Maria Laranjinha amehimiza kudumishwa kwa ushirikiano huo kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi