-DC awataka kuzingatia maadili, miiko ya kazi
MwandishiWetu, daimatznews@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, ametoa rai kwa watumishi wa umma Hospitali ya Rufaa Mwananyamala kuzingatia maadili na miiko yao ya kazi wanapotekeleza majukumu yao hususani kwenye upatikanaji wa ushahidi kwenye matukio ya ukatili wa ubakaji na ulawiti.
 |
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule akizungumzana watumishi wa Hospitali ya Rufaa Mwananyamala, Dar es Salaam kuhusu kuzingatia maadili na miiko yao ya kazi wakati warsha iliyoanaliwa na TAKUKURU Desemba 11, 2024. |
Ameitoa Jijini Dar es Salaam Desemba 11, 2024 kwenye warsha kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, kuhusu umuhimu wa maadili na madhara ya rushwa ya ngono na ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni katika kuadhimisha siku ya maadili na haki za Binadamu.
Aidha amewaomba watumishi wa afya kutokuwa sehemu ya kufanikisha uhalifu na ukatili wanaotendewa watoto hususani ubakaji na ulawiti Kwa kutoa ushahidi katika kujaza fomu ya Polisi ya PF3 Ili mtuhumiwa atiwe hatiani na kuwaondoa mtaani wasiendelee kutekeleza Matukio hayo ya kikatili ndani ya Jamii
Amewasisitiza kuharakisha uchunguzi wa kweli na ushahidi kurudishwa Polisi ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati kwa mtenda na mtendewa hivyo wasimame kama wataalamu kwenye sekta ya Afya kwa kukataa Rushwa na kusimamia kwa mujibu wa Sheria Ili kuendelea kulinda haki za Binadamu
Amesema Mmomonyoko wa maadili Kinondoni upo sana hususani maeneo ya Mwananyamala, Makumbusho, na Tandale Matukio ya ubakaji na ulawiti ni mengi hivyo wanaendelea kuwasihi viongozi wa Dini na watu wa haki Jinai kuangalia jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia ambapo hospital pia ni Moja ya wahusika katika kuangalia kama tendo hilo limetokea ili mtuhumiwa atiwe hatiani.
Hata hivyo amesema Hospitali ya rufaa ya mwananyamala ndio kimbilio ya watu wengi wazee, wazazi kutokana na unafuu wa gharama hivyo ili kuendelea kuwa kimbilio waendelee kuishi na kutoa huduma kwa Msingi na miiko ya Utumishi wa umma kwani hawataweza kuzungumza kuhusu rushwa, uzembe na maadili mabovu.
Ameongeza kuwa siku ya maadhimisho ya Haki za Binadamu inayoadhimishwa Desemba 10 ya kila mwaka pamoja na siku ya mapambano dhidi ya rushwa ambayo huadhimishwa kila Desemba 9 ya kila mwaka serikali iliamua kuunganisha siku hizo mbili kufanya maadhimisho hayo Desemba 10 na kuwa siku ya maadili na Haki za Binadamu.
“ Nasisitiza kuishi na kutenda kazi Kwa kuzingatia miiko ya Utumishi wa umma ambayo ni uadilifu, uzalendo, utaratibu wa kuwasiliana, kuongea matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa, mavazi kulingana na miiko ya kazi” DC Mtambule.
Katika miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika wana kila sababu ya kujivunia kwa kuwa na tunu ya amani na utulivu wa nchi na Jitihada za kutokomeza maadui watatu maradhi, ujinga na umaskini hivyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhakikisha kuwa sekta ya Afya inaimarika hususani miundombinu ambayo ni pamoja na ujenzi wa hospitali mpya za serikali na binafsi na uwepo wa vifaa tiba na madawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Christian Nyakizee amesema lengo la warsha hiyo ni kuwakumbusha watumishi wa Umma kutekeleza majukumu ya bila kujihusisha na vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki na inaenda nje ya utaratibu na kunyima haki hivyo ni vyema kila mmoja kupambana na rushwa na kuishi kwa misingi ya maadili ya Utumishi wa umma.
Amesema warsha hiyo ni muendelezo wa jukumu la TAKUKURU Kinondoni kutoa elimu kwa umma kwa taasisi na makundi mbalimbali ambapo leo wametoa elimu kwa umma kuhusu matatizo ya ukatili wa kijinsia na watoto ambalo ni jambo kubwa ndani ya Jamii hususani Wilaya ya Kinondoni.
Ameongeza kuwa wameshatoa Elimu hiyo kwa viongozi wa serikali za Miata, Polisi Dawati la Jinsia na Ustawi wa Jamii Ili kuwezesha kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya Jamii.
Nae, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Dkt. Zavery Benela, ameishukuru TAKUKURU Kinondoni Kwa kutoa warsha hiyo kuhusu maadili, ukatili wa kijinsia ambayo itawezesha pia watumishi kupata Elimu jisnsi ya kutokupokea rushwa kutoka kwa wateja wao.
Amesema Rushwa ni adui wa haki ambayo inasababisha wateja wao kukosa haki yao ya matibabu katika hospitali yao hivyo kuwakumbusha viongozi kusimamia maadili na watumishi wa sekta ya Afya kuzingatia uadilifu.
Maoni
Chapisha Maoni