'Miaka 63 ya Uhuru na NHC inayotimizia ndoto Watanzania'


- Ni ya makazi bora, yajenga

 zaidi ya nyumba 30,000

- Awamu ya 6 pekee miradi ya zaidi ya Sh 212 bilioni

- Thamani miradi ya ubia yafikia Sh 191 bilioni

Sehemu ya Mradi wa nyumba Samia Scheme

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Tanzania Bara ilipata Uhuru wake tarehe kama ya leo Desemba 9, mwaka 1961 kutoka kwa Waingareza, ikihitimisha enzi za ukoloni, ambapo taifa lilitawaliwa na wageni hao, ambao walikabidhiwa dhamana na Umoja wa Mataifa, lakini waliondoka nchini bila kuacha mpango mkakati wowote wa makazi bora kwa wananchi.

Rais wa Kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere(Kushoto), akishuhudia uzinduzi wa nyumba za makazi ya wananchi zilizojengwa na NHC, eneo la Magomeni miaka ya 70. Picha ya Maktaba

Hata hivyo, kwa hekima, busara na kutambua mahitaji ya makazi bora kwa wananchi, mwaka mmoja baada Uhuru, Serikali iliyokuwa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilianzisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), mwaka1962 kwa Sheria ya Bunge Na. 45.

 Tangu kuanzishwa kwake wakati huo, hata sasa Tanzania inapoadhimisha miaka 63 ya Uhuru, NHC limebeba jukumu muhimu la kuleta mageuzi ya kipekee katika sekta ya nyumba nchini, likiwa na ndoto inayoendelea kuitimiza ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora.

Ushahidi wa NHC kulibeba jukumu hilo kikamilifu ni mageuzi yanayoonekana katika sekta ya nyumba nchini kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati ya shirika hilo linalotajwa kuwa kubwa zaidi barani Afrika, likiwa na  mtaji unaokadiriwa kufikia Shilingi Trilioni 5.

Awamu ya Sita

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan 

Kwa kuanzia, ushahidi wa NHC iliyo bora zaidi ikibeba majukumu yake kwa ukamilifu, unapatikana kwenye kipindi hiki cha utawala wa Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na hata miaka ya nyuma awamu zilizotangulia.

Hilo haliwezi kufichika kwani ndani ya kipindi hicho shirika limetekeleza na linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ukandarasi ambayo moja kwa moja inagusa na kuchangia maendeleo ya taifa Tanzania, mtu mmoja mmoja, wizara hata mashirika na kampuni.

Katika kipindi cha Awamu ya Sita pekee yaani mwaka 2023/24, hadi Disemba 2024, miradi mbalimbali imetekelezwa kama ifuatavyo:-

i.             Ujenzi wa Jengo la Kitengo cha Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 jijini Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 100.

 ii.           Ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Wizara nane (8) za Serikali ya Tanzania yenye             thamani ya shilingi bilioni 194 katika Mji wa Serikali Mtumba umefikia wastani wa           asilimia 85 na utakamilika Januari 31, 2025.

 iii.         Ujenzi wa jengo la Tanzanite ulio na thamani ya shilingi bilioni 5.5 katika mji wa           Mererani mkoani Manyara, ambao sasa umefikia asilimia 86, unaendelea                     kukamilishwa. 

iv.          Ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umefikia asilimia 80 yautekelezaji, ukiwa na thamani ya Shilingi Bilioni 9.8.

 v.            Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara ya                 Fedha

 vi.          Ujenzi wa Hospitali za Kanda ya Kusini (Mitengo) na Kanda ya Ziwa (Mwalimu                         Nyerere). 

Hata hivyo, utekelezaji miradi hiyo na mingine mingi isingewezekana bila NHC kufanyiwa mageuzi na kuiwekea mpango mkakati ikitazamwa historia yake na malengo yake katika sekta ya nyumba.

Mpango Mkakati wa Maendeleo

Kwa kuangalia mambo hayo mawili pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo, Mwaka 2010, Serikali ilianza awamu mpya ya kuimarisha Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuboresha Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti. Lengo kufanya hivyo lilikuwa kuongeza ufanisi, kujenga nyumba zaidi na kufanikisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Katika mazingira hayo Mpango Mkakati wa Miaka 10 kuanzia mwaka 2015/16–2024 hadi 2025 uliandaliwa. Mpango huu ulilenga ujenzi wa nyumba 10,000, usimamizi wa miradi mikubwa na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na taasisi za kifedha.

Pia unatoa dira ya ukuaji wa sekta ya nyumba nchini, ikizingatiwa mahitaji ya sasa, ongezeko la idadi ya watu na mustakabali wa taifa kwenye sera ya Ardhi na Makazi.

Mafanikio

Licha ya machache yaliyotajwa kutekelezwa katika Awamu ya Sita, tangu Uhuru hadi sasa imefanikiwa kutekeleza na kukamilisha miradi mikubwa ya maendeleo, ambayo ni ushahidi mwingine wa mafanikio ya NHC kwa kipindi chote cha uhai wake wa miaka 62, tangu lilipoanzishwa mwaka 1962.

Sehemu ya mradi wa majengo ya wizara nane za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

 Miradi iliyotekelezwa na kukamilishwa na NHC tangu Uhuru inajumuisha:

Ujenzi wa nyumba 887 za makazi za kawaida katika eneo la Iyumbu na Chamwino Mkoani Dodoma (404), Wilaya ya Makete Mkoa wa Njombe (50), Chartur Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga (10) na Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi (24).
  1. Ujenzi wa nyumba 521 kwa ajili ya biashara katika eneo la Mtukula mkoani Kagera (45), Medeli mkoani Dodoma (42), Dar Es Salaam (380) na Mwanza (54).  
  2. Ujenzi wa nyumba 1,187 kwa ajili ya makazi na biashara katika eneo la Morocco Square (1,100) na miradi ya ubia (87) katika Jiji la Dar es Salaam.
  3. Shirika limeongeza rasilimali zake kwa kununua nyumba 896 zikiwemo nyumba za makazi 389 na nyumba 497 za biashara katika eneo la Urafiki Mkoa wa Dar es Salaam.

Mbali na miradi hiyo iliyokamilishwa, Shirika la Nyumba la Taifa, linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi iliyo katika hatua tofauti za ujenzi.

Miradi hiyo inajumuisha; Ujenzi wa nyumba 560 katika mradi wa “Samia Housing Scheme” Awamu ya Kwanza katika eneo la Kawe jijini Dar es Salaam ambao umefikia asilimia 54, unaotarajiwa kukamilika Januari 2025. Mradi huu utawezesha ujenzi wa nyumba 5,000 nchini zitakazogharimu takriban shilingi bilioni 466.

Mauzo ya nyumba hizo za Kawe yameshakamilika, hii inatokana na Awamu ya Sita kufungua milango ya uchumi na uwezeshaji wa mapato kwa wananchi.

Pia kuna ujenzi wa nyumba 1,533 za makazi na biashara. Katika mradi wa Kawe 711 zinajengwa nyumba (422) na umefikia asilimia 45 ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2026. Aidha, pia kuna ujenzi wa nyumba 532 kupitia mradi wa Golden Premier Residence.

NHC na Sekta ya Fedha

Shirika la Nyumba la Taifa pia limekuwa kiunganishi muhimu kati ya wananchi na taasisi za kifedha nchini na tayari zaidi ya benki 22 zimeungana na NHC kuwezesha mikopo ya nyumba ya muda mrefu.

NHC na Sekta Binafsi

Kupitia sera ya ubia, NHC imefungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa nyumba na majengo ya kisasa. Ushirikiano huo umeongeza ushindani, ubora na kupanua fursa za uwekezaji katika sekta ya nyumba nchini.

Kupitia Sera ya Ubia iliyohuishwa mwaka 2022, NHC inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ubia, ambapo jumla ya miradi 20 yenye thamani ya Shilingi bilioni 191 iko tatika hatua mbalimbali za ujenzi.

Katika eneo hilo, majengo makubwa ya kibiashara katikati ya miji ni ushahidi wa mchango wa NHC katika kuboresha mandhari ya miji. Miradi kama vile ya nyumba za makazi na ofisi, zimekuwa chanzo kikuu cha ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.

 NHC historia na maono

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah(Kushoto), akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, Augustino Vumu(Mwenye mavazi meupe),wakiwaongoza wabunge wajumbe wa kamati hiyo kutembelea mradi wa ujenzi wa wizara nane katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma hivi karibuni.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), lilianzishwa kwa sheria ya Bunge, mwaka mmoja tu baada ya Uhuru wa Tanganyika, likiwa ni sehemu ya maono ya Mwalimu Nyerere kuhakikisha mahitaji ya msingi ya mwanadamu kama makazi, chakula na mavazi yanapatikana kwa kila mwananchi.

NHC miaka ya mwanzo lilitekeleza majukumu yake kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba na majengo ya umma. Hata hivyo, changamoto za kiuchumi na kisheria ziliathiri utendaji wa Shirika.

Sheria ya Zuio la Kodi ya Mwaka 1984 ilikuwa moja ya sheria zilizosababisha NHC na sekta ya nyumba kusuasua kwa kuzuia uwekezaji wa sekta binafsi, kutokana na masharti magumu kwa wamiliki wa nyumba.

Hata hivyo mwaka 1990 mageuzi yalifanyika, ambapo NHC liliunganishwa nailiyokuwa Msajili wa Majumba. Hili lilifanyika kupitia Sheria Na. 2, na NHC likapewa mamlaka mapya ya kusimamia nyumba zilizotwaliwa na Serikali mwaka 1971.

Hatua nyingine muhimu ilikuja mwaka 2005, pale Bunge lilipoondoa sheria zisizokuwa rafiki na kuweka mazingira bora kwa uwekezaji, ikiwemo kuboresha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 iliyounda upya Shirika la Nyumba la Taifa.

NHC leo na kesho

Shirika linaendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia utaalamu wa ndani na teknolojia za kisasa, lengo ni kuimarisha utendaji, kuongeza ufanisi wa miradi, na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika miaka ijayo, NHC ina mpango wa kuanzisha miradi mingi zaidi ya makazi, kuimarisha uhusiano wa kimataifa, pia kutoa ushauri wa kitaalamu katika miradi mbalimbali.

Mradi wa Morocco Square unavyoonekana 

NHC inaendelea kushirikiana na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) katika kuimarisha maendeleo ya nyumba ukanda wa Afrika Mashariki. Ikumbukwe kuwa NHC ilishiriki kuasisiwa kwa ZHC mwaka 2014, ambapo ilitoa mafunzo mbalimbali ya namna Shirika la Nyumba linavyotakiwa kujiendesha.

Mafunzo ya kitaalam na kwa wataalam wa ZHC kuja Tanzania Bara na kujifunza mambo ya nyumba, ikiwemo mafunzo ya utayarishaji wa Sheria za Shirika la Nyumba Zanzibar. Ziara mbalimbali za kubadilishana uzoefu kwa Bodi na Menejimenti ya pande mbili za Muungano pia zimefanyika.

Kwa zaidi ya miaka 61, NHC limekuwa kiungo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea makazi bora. Kutoka kwenye changamoto za awali hadi mafanikio ya sasa, Shirika linaonyesha mfano wa jinsi taasisi za umma zinavyoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mustakabali wa Shirika ni mzuri na kupitia mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya nyumba nchini Tanzania, ikihakikisha kila Mtanzania anafurahia haki ya makazi bora.

 


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi

Moshi mweusi watokea Vatican, moshi mweupe wasubiriwa kwa hamu