-'Asikia' kilio cha Jukwaa la Wahariri kwa Jerry Slaa
-Awapa Prof Kabudi na Msigwa, TEF wapongeza
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan pichani‘ametoa’ zawadi za Krismasi mapema. Ndivyo unavyoweza kueleza baada ya kiongozi huyo kutangaza uteuzi na mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na viongozi mbalimbali wa Serikali anayoiongoza.
![]() |
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan |
Katika mabadiliko hayo, yaliyotangazwa leo Desemba 8,2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, Rais Samia ameihamisha sekta ya Habari kutoka ka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo sasa Sekta hiyo itaongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi.
Uamuzi huo wa Rais kuihamisha Sekta ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyokuwa chini ya Jerry Silaa ni kama amesikia kilio cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kulalamika kwamba Waziri huyo amekuwa akikacha mialiko ya wadau wa Habari, lakini pia waliomba ihamishwe kwa walichodai kuona inamezwa na shughuli nyingine za wizara..
Madai hayo ya TEF yalitolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile katika ufunguzi wa Mkutano wake Mkuu wa Mwaka jijini Dar es Salaam, Novemba 9, 2024, ambapo Waziri Jerry Silaa alialikwa pia kuwa mgeni rasmi, lakini hakutokea, aliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara yake,
Tayari TEF kupitia Mwenyekiti wake imetoa salam za pongezi kwa hatua hiyo ya Rais Samia, ikiwapongeza pia Waziri mpya wa Sekta ya Habari Profesa Kabudi na Katibu Mkuu Mpya aliyeteuliwa, Gerson Msigwa.
“Sisi, Jukwaa la Wahariri Tanzania, tumepokea mabadiliko haya kwa moyo mmoja.
Awali tuliomba sekta ya habari ihamishwe katika wizara hii kutokana na kwamba ilionekana kumezwa na sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo mawaziri wengi waliipa kisogo sekta ya Habari.
Mheshimiwa Rais imempendeza kuirejesha huko, tunaamini waliopewa dhamana hawataiweka kando sekta ya Habari kama ilivyokuwa awali.
Faraja tuliyoipata ni kwamba viongozi wakuu wote walioteuliwa kuongoza wizara hii mpya ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo — Waziri na Katibu Mkuu — wote ni waandishi wa habari kitaaluma. Tunaamini hawataipa kisogo sekta ya Habari,”ilielezaTEF katikantaarifa iliyosainiwa na Balile nakuongeza:
“Tunawapongeza Waziri Prof. Palamagamba Kabudi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hii mpya na Gerson Msigwa aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii mpya ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.”
Katika mabadiliko hayo Rais Samia amemrejesha Msigwa kuwa Mmsemaji wa Serikali, nafasi aliyoishika enzi za utawala wa Awamu ya Tano,huku aliyekuwa Msemaji wa Serikali Thobias Makoba akiteuliwa kuwa balozi na kusubiri kupangiwa kituo cha Kazi.
Rais Samia pia amemteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuchukua nafasi ya Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira}.
Katika uteuzi huo Aballah Ulega anakuwa Waziri wa Ujenzi, Damas Numbalo anakuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Ashatu Kijaji ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, huku Jerry Silaa akiwa Waziri wa Mawasiliano naTeknolojia ya Habari.
Ikulu imesema uapisho wa wateulie hao utafanyika Ikulu Ndogo Tunguu Zanzibar, Desemba 10, 2024.
Majina na uteuzi soma zaidi kwenye
viambatanisho hapa chini.;
0 Maoni