-Wamo wachina, wakenya
-Wakutwa na tani Kilo 14,264.1 za nyaya za shaba
Na Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail,com
Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli linawashikilia watuhumiwa zaidi ya 15, wakiwemo raia wa China na Kenya kwa tuhuma za kuhusika na uharibifu wa miundombinu ya njia ya Reli ya Kisasa (SGR).
![]() |
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli, Gallus Hyera akiungumza na wanahabari . |
Hayo yamebainishwa jijini humo, na Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Gallus Hyera wakati akizungumza na waandishi wa habari Desemba 17/2024.
Kamanda Hyera amesema watuhumiwa hao waliwakamata wakiwa na kilo 14,264.1 (zaidi ya tani 14) za nyaya za shaba zilizokatwa kwenye njia hiyo ya SGR kwenye maeneo mbalimbali na kuuzwa kama chuma chakavu.
"Watuhumiwa hawa na nyaya za shaba, tuliwakamata kupitia misako na operesheni tulizofanya maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama," amesema Hyera na kuongeza,
"Kati ya wanaotuhumiwa kufanya vitendo hivyo, wamo mafundi walioshiriki ujenzi wa miundombinu ya SGR, fundi umeme na wafanyabishara wanaojishughulisha na uuzaji na ununuzi wa chuma chakavu,".
![]() |
Sehemu ya shehena ya nyaya za shaba waliokamatwa nazo watuhumiwa |
Hyera amebainisha kuwa Novemba 28, 2024 maeneo ya Mdaula mkoani Pwani, walikamatwa watuhumiwa wakiwa na nyaya za shaba kilo saba.
"Mmoja kati ya watuhumiwa ni fundi umeme, mwajiriwa wa kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza ujenzi wa miundombinu ya SGR. Huyu ndiye anayekata nyaya maeneo mbalimbali. Jumla ya watuhumiwa watatu wamekamatwa," amesema.
Amefafanua kuwa Novemba 30, 2024 katika eneo la Visiga mkoani Pwani kwenye kampuni ya The African Light Investment Ltd inayomilikiwa na raia wa kigeni (China na Kenya) zilikamatwa nyaya za shaba zenye uzito wa kilo 882.5.
"Desemba 2, 2024 huko maeneo ya Visiga, Pwani ulifanyika upekuzi kwenye nyumba inayomilikiwa na The African Light Investment Ltd (Raia wa China na Kenya), katika upekuzi huo, watuhumiwa walikutwa na nyaya mbalimbali za shaba zenye kilo 3687.9.
"Nyaya hizi zimetambuliwa kuwa zimetokana na uharibifu kwenye miradi ya SGR na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania). Jumla wamekutwa na nyaya kilo 4,570.4 na raw copper bars (vipande vya shaba) 44 zenye uzito wa kilo 971.5," amesema.
Kupitia taarifa za kiintelijensia, amesema eneo la Kisemvule zilikamatwa nyaya za shaba kilo 608.6 za Tanesco, kilo 37.6 (za SGR) na vipande vya shaba zilizozalishwa kwa kuyeyushwa nyaya za shaba kilo 5,517.4 kwenye kiwanda cha chuma chakavu cha Metal Chem International Co. Ltd. Watuhumiwa wawili wamekamatwa.
Desemba 5, 2024 eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti amesema walikamata kilo 65.5 za nyaya hizo kutoka kwa wanunuzi wa chuma chakavu. Pia walikamatwa watuhumiwa wakiwa na waya wa shaba kilo 6.5 wakiwa katika harakati ya kuuza.
Amesisitiza kuwa Desemba 13, 2024 mkoani Pwani walikamatwa wamiliki wa kiwanda cha Balochistan Group of Industrial (BGI) kutokana na taarifa za kiintelijensia wakiwa na waya wa shamba kilo 61, vipande vya shaba 19 vyenye uzito wa kilo 141 kutoka kwenye gari lenye namba T 141 DQG aina ya Fuso.
Amesema kuwa upekuzi ulipofanyika kiwandani zilikamatwa nyaya za shaba kilo 67 na vipande 426 vyenye uzito wa kilo 7,728 ambavyo ni zao la waya wa shaba.
Amesema shaba hiyo imetoka kwenye miundombinu ya miradi ya SGR na Tanesco na kwamba watuhumiwa wawili wamekamatwa.
Ameongeza kuwa jumla ya watuhumiwa 13 wamefikishwa mahakamani, kati yao wanane wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha kwa makosa ya uhujumu uchumi na watano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa makosa sawa na hayo.
"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa yeyote anayejipanga kufanya uhalifu huu wa kukata nyaya za shaba kwenye miradi ya SGR na Tanesco, watasakwa kwa nguvu zote, kukamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria," amesema.
Kwa upande wake,Meneja Ishara na Umeme kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Felix Mutashobya amesema uharibifu wa miundombinu unaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo hitilafu katika mfumo wa mawasiliano na umeme katika SGR.
"Matokeo yake inaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama kwa ajili ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa," amesema.
0 Maoni