Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wananchi ipeni thamani miradi ya minara- Waziri Nape

-Aitaka Vodacom kukopesha zaidi simu kwa wananchi

Mwandishi Wetu, WHMTH, Kagera

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye(pichani), amewataka wananchi wa vijijini waliofikishiwa huduma za mawasiliano kuipa thamani miradi hiyo kwa kuitumia.

Amesema wananchi wasipoitumia ipasavyo miradi hiyo, uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa ku5shirikiana na Sekta binafsi hautakuwa na maana, huku  akiitaka Kampuni ya Vodacom kuongeza nguvu ya kukopesha wanavijiji simu, ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hizo. 

Waziri Nape ametoa kauli hiyo leo Julia 16, 2024, baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika Kijiji cha Kisharara, Kata ya Karambi wilayani Muleba, mkoani Kagera akiwa katika siku ya pili ya ziara yake kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

""Wito wangu kwa wananchi watumie hizi huduma, kwa sababu kadri idadi yao inavyoongezeka inatusaidia kuona namna gharama zitakavyopungua, lakini pia tunaupa thamani mradi huu, fedha iliyolazwa hapa (zaidi ya milioni 300), kama watumiaji watakuwa hawaongezeki inakuwa hasara kwa watoa huduma na kwa Serikali," amesema Nape na kuongeza:

 "Niwahakikishie tu utayari wa Serikali kuendelea kufanya kazi na Sekta Binafsi, kwenye hili la mawasiliano nadhani tumefanikiwa sana, .... sekta binafsi inaleta fedha zake inafanya biashara, lakini Serikali inaongeza fedha miradi itekelezwe ili wananchi ambao katika hali ya kawaida wasingefikiwa, waweze kupata mawasiliano."

Awali, akizungumza na viongozi wa mkoa, wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara take na watoa huduma katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Nape amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi mkoani humo, kusimamia ipasavyo kodi ya pango katika maeneo yote yaliyojengwa minara, kwenye ardhi ya vijiji ili iwe na matokeo chanya na wananchi wanufaike na ardhi yao.

Akitoa taarifa ya mnara huo wa Mkuu wa Vodacom Kanda ya Ziwa Ezekiel Nungwi, amesema tangu mnara huo uwashwe Juni 21 mwaka huu, tayari vijana saba wamejiari kutoa huduma za Uwakala wa Mpesa na wengine kuuza line, wakati  jumla ya wanufaika wa mawasiliano ni watu 20,000.

"...Mnara huu umeshatoa ajira kwa mawakala saba na mzunguko wake tangu tumewasha mnara ni shilingi milioni 25 hadi 50, vilevile tumetoa ajira za muda mfupi kwa wajenzi,  ambao ni watu wanaotoka hapa kijijini na ajira ya muda mrefu kwa mlinzi,"

Waziri Nape pia amekagua minara katika Kijiji cha Kasharara Kata ya Karambi Wilaya ya Muleba na kijiji cha Katahoka Kata ya Katahoka Wilaya ya Biharamulo alikowasisitiza pia wananchi kutumia vizuri mitandao ili isivunje ndoa zao bali kuziimarisha.

Chapisha Maoni

0 Maoni