Mwandishi Wetu, WHMTH, Kagera
Katika kuhakikisha mikoa iliyo pembezoni inaungwanishwa na Tanzania ya Kidigitali, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ((UCSAF), unatarajia kutumia takriban shilingi bilioni 6,6 kujenga minara 45 katika Kata 44 mkoani Kagera.
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba mebainisha hayo leo Julai 16, wakati akitoa taarifa ya utendaji wa mfuko huo katika Mkoa wa Kagera, mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya waziri huyo Mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya Simu.
"Minara 45 ya Kagera ni sehemu ya minara 758 inayofadhiliwa na Serikali kwa kipindi cha miaka miwili, kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024 hadi 2024/2025, Katika Mkoa wa Kagera tunatarajia wananchi 801,961 watanufaika mara itakapokamilika minara hiyo mwanzoni mwa mwaka 2025," amesema Mashiba.
Kwa mujibu wa Mashiba, Mkoa wa Kagera ni kati ya mikoa 26 Tanzania Bara itakayonufaika ambapo ameainisha wilaya za mkoa huo inakojengwa minara 45 akiitaja kuwa ni Biharamulo minara 13, Bukoba DC (1), Karagwe (14), Missenyi (3), Kyerwa (4), Muleba (8), na Ngara (2).
Amesema hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2024, jumla ya minara kumi (10) imeshawashwa na Watoa Huduma za Mawasiliano.
Mtendaji Mkuu huyo wa UCSAF amesema, kupitia minara 10 iliyowashwa, vijiji kadhaa vya wilaya hizo vimenufaika na mradi huo, katika kata 44 zikiwemo Kaniha, Nyakahura, Nyantakara, Nyarubungo, Igurwa, Kihanga, Kakunyu, Karambi na Ngenge.
Tangu mwaka 2009 jumla ya minara 80 imejengwa katika wilaya saba za Mkoa wa Kagera, kutokana na makubaliano kati ya Serikali, kupitia UCSAF na watoa huduma za mawasiliano.
Mashiba amesema, minara hiyo iliyojengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G na 4G, kwa ruzuku iliyotolewa na UCSAF, imegharimu jumla ya Shilingi Bilioni 10.89, na inawanufaisha Watanzania 1,248,911.
Ametaja wilaya saba zinazofaidika na minara hiyo na idadi ya minara iliyojengwa, kwenye mabano, kuwa ni Biharamulo (15), Bukoba DC (5), Karagwe (22), Missenyi (14), Kyerwa (6), Muleba (4), na Ngara (14).
0 Maoni