Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wafanyabiashara wa ng'ombe wamuunga mkono Rais Samia

-Kufanya maonyesho Juni 14 Chalinze

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com 

CHAMA cha Wafanyabiashra wa Ng'ombe Tanzania (TCCS), kimesema kinaendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha sekta ufugaji nchini inazidi kuboreshwa kufikia ufugaji wa kisasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kibiashara wa Ng'ombe(TCCS), Naweed Mulla (aliyevaa kofia),wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya mifugo na mnada, unaotarajiwa kufanyika Juni 14 -15, 2024 maeneo ya Ubena Estate Chalinze.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Kibiashara wa Ng'ombe nchini (TCCS), Naweed Mulla ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, kuhusu maonesho ya mifugo na mnada unaotarajiwa kufanyika Juni 14 -15, 2024 maeneo ya Ubena Estate Chalinze.

"Lengo la kuanzisha programu hizo ni kusaidia wakulima na wafugaji kujikwamua kiuchumi wao wenyewe na kuongeza  Pato la Taifa kupitia ufugaji," amesema Mulla.

Amebainisha kuwa takribani washiriki 300 wanatarajiwa kushiriki maonesho hayo yatakayofanyika kwa siku tatu, huku akitoa wito kwa vijana na wafugaji wapya wanaotamani kuingia katika shughuli za ufugaji kushiriki katika maonesho hayo, ili waweze kujifunza mambo mbalimbali ya ufugaji na kuona namna watakavyoweza kufanya biashara hizo za kilimo.

Mulla amesema maonesho hayo yana nia ya kuwezesha Jukwaa Madhubuti la Kitaifa la Wafugaji, wasindikaji na wadau katika mnyororo wa thamani ya mifugo, kutambulika kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo kwa mbinu bora, endelevu za kiuchumi na kimazingira.

''Tamasha hilo lilianzishwa na kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2022, ambapo kwa mwaka huu linatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa yatakayoenda sanjari na utoaji wa elimu, ili kutoa msaada kwa jamii namna ya kufuga kwa tija,''amesema Mulla na kuongeza;

''Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora, rafiki na wezeshi kuhakikisha sekta ya mifugo inawakwamua wakulima na wafugaji kimaisha na kuhakikisha wanaongeza tija na ubunifu katika shughuli za kilimo.''

Naye Kaimu Mkurugezi Idara ya Mipango, Ushauri na Uhusiano wa Benki ya Kilimo, Mkani Waziri amesema kazi yao kubwa ni kusaidia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi vinapata maendeleo, hivyo wameamua kushirikiana na TCCS kuona namna wanavyoweza kuleta mageuzi katika tasnia ya ufugaji.

Amesema Benki ya kilimo wamekuwa washiriki wakuu katika sekta ya ufugaji ili kuhakikisha  Watanzania wanafuga kwa tija na kuweza  kupata kipato cha  kuboresha maisha yao.

''Tunatoa  mikopo ya moja kwa moja kwa wafugaji katika kuwawezesha wafugaji na hadi sasa benki imetoa jumla ya Sh.bilioni 38 ya mikopo kwa wafugaji  kwa wanufaika wapatao 8688 katika mikoa 21,''amesema na kuongeza;

''Tumekuwa tunashirikiana na taasisi nyingine za fedha katika kuchangiza  taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kutoa dhamana ya asilimia 50 hadi 70 kwa mikopo mfugaji anaochukua lengo ikiwa ni kuwainua wafugaji wakitanzania,''alisema.

 Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoani Pwani, Ngobere Msamau amesema kupitia maonesho hayo wanatarajia kupata  elimu ya kufanya wazidi kuongeza tija katika ufugaji wa kisasa na kuondokana na ule wa kienyeji.


Chapisha Maoni

0 Maoni