Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
KABIDHI Wasii Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi amewataka wafungishaji ndoa wote nchini kuhakikisha wamejisajili kwenye mfumo wa kidijitali wa e-RITA ifikapo Juni 10, 2024.
Agizo hilo hilo limetolewa na Kabidhi Wasii Mkuu Juni 6,2024, Dar es Salaam, ikiwa ni siku nne, kabla ya siku ya mwisho kujisajili, sawa na saa 96 za utekelezaji kwa walengwa.
“Mfumo huu wa kidijitali utawazeshesha wahusika kutambulika katika kanzidata ya Msajili Mkuu wa Ndoa na Talaka, pia kupata leseni mpya za kidijitali za kufungisha ndoa,” amesema Kanyusi na kuongeza; "Mfumo huo utaongeza ufanisi na kuongeza udhibiti wa usajili wa ndoa."
Kanyusi amewataja walengwa katika zoezi hilo kuwa ni wafungishaji ndoa wote kutoka dini na madhehebu yote nchini, akibainisha kwamba usajili wa kundi hilo siyo utaratibu mpya bali umekuwa ukifanyika kwa miaka mingi kupitia mfumo wa analojia.
“Kuanzia Januari mwaka huu mpaka sasa tayari wafungishaji ndoa 3,635 wameshajisajili kwenye mfumo wa e-RITA. Natoa rai kwa wale ambao hawajajisajili kwenye mfumo, kufanya hivyo kwani shahada za ndoa zitatolewa kwa wale waliosajiliwa tu kwenye mfumo,” amesisitiza Kanyusi.
Kwa mujibu wa Kabidhi Wasii Mkuu huyo, zoezi hilo la usijili linawahusu wafungishaji wote hata wale ambao walishasajiliwa awali kwenye mfumo wa anajojia, ikijumuisha walio na leseni hai na ambao leseni zao zimekwisha muda wake, hivyo kuhitaji kuhuishwa.
Amebainisha kwamba kuanzia sasa wafungishaji ndoa wapya watatakiwa kutumia mfumo mpya wa kidijitali wa e-RITA na kupata leseni zinazowapa mamalaka kisheria ya kufunga ndoa.
“Ili kujisajili wafungishaji ndoa wanatakiwa kuingia kwenye tovuti ya Wakala yaani www.rita.go.tz kisha bofya kitife kilichoandikwa e-RITA na kuchagua huduma ya Ndoa na Talaka baada ya hapo utapata maelekezo,” amesema.
Akifafanua zaidi, Kanyusi amesema zoezi la usajili linahusisha ujazaji wa taarifa binafsi za mfungishaji ndoa, dini na dhehebu lake na pia atahitaji kuthibitishwa na viongozi wa dhehebu lake.
“RITA imeendelea kufanya maboresho katika utoaji wa huduma zake kwa njia ya kielekroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi sambamba na kusogeza huduma zake karibu na wananchi pamoja kufikia matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” ameongeza.
0 Maoni