Hot Posts

6/recent/ticker-posts

TRAMPA mguu sawa yapiga msasa watumishi wa umma

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mwenyekiti wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), Devotha Mrope amezindua mafunzo maalumu yanayolenga kujenga uwezo wa kitaaluma kwa wataalamu utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Devotha amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watumishi wa umma na taasisi binafsi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na uadilifu katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.

  Mwenyekiti wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania
 (TRAMPA), Devotha Mrope

"Mafunzo haya yatawakilisha juhudi za TRAMPA katika kujenga uwezo na kuimarisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka nchini Tanzania. Tunajitahidi kuhakikisha wataalamu wetu wanapata mafunzo na maarifa yanayohitajika ili kuhakikisha taarifa na nyaraka zinatunzwa kwa weledi na uadilifu,"  amesema Devota.

Mwenyekiti huyo wa TRAMPA amebainisha kuwa mafunzo hayo yamepangwa kufanyika tena Mei 6 hadi 9, 2024 mkoani Iringa na yanatarajiwa kuhudhuriwa na wataalamu wa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kutoka Tanzania bara na visiwani. 

Amesema kuwa hiyo ni fursa kwa washiriki kujifunza mbinu mpya na  bora za utunzaji wa kumbukumbu, uadilifu katika utunzaji wa siri za ofisi, na njia za kisasa za usimamizi wa nyaraka za taasisi.

Devotha amesema kwa kuzingatia thamani ya mafunzo hayo, washiriki watalazimika kulipia gharama ya ushiriki, ambayo ni shilingi laki nne tu (400,000), zitakazogharamia uendeshaji wa mafunzo kwa muda wa siku nne. 

Sambamba na hilo, Devotha ametoa wito kwa waajiri kuwawezesha watumishi wao kuhudhuria mafunzo haya na kuwalipia stahiki zao. 

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wanataaluma kuthibitisha ushiriki wao mapema ili kurahisisha maandalizi ya mafunzo hayo muhimu ambayo yatawezesha kuboresha utendaji na ufanisi katika utunzaji wa taarifa za umma na za binafsi.

“Kada hii ni miongoni mwa kada zinazoongozwa na mifumo mingi, sambamba na miongozo kulingana na wakati. Hivyo, inalazimu wataalamu wajengewe uwezo kuendana na mazingira ya wakati husika” amesisitiza Devotha.



Chapisha Maoni

0 Maoni