-Akutwa na kesi ya kujibu
Mwandishi Wetu,daimatzanews@gmail.com
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imemkuta na kesi ya kujibu mfanyakazi wa Benki ya CRDB, Ibrahim Masahi, anayetuhumiwa kumjeruhi kwa nyundo jirani yake, Deogratus Minja kwa madai kuwa alikwenda kumshitaki Serikali za Mitaa kwa kutiririsha maji machafu mbele ya nyumba yake.
Akitoa uamuzi huo leo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Amos Rweikiza amesema mahakama baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wote imeridhika kwamba mshitakiwa ana kesi ya kujibu kwa hiyo atatakiwa kujitetea.
Hakimu Rweikiza alimueleza mshitakiwa: "Pamoja na kukutwa na kesi ya kujibu, una haki ya kuleta mashahidi na vielelezo wakati wa kujitetea, pia unaweza kutoa ushahidi wako chini ya kiapo au ukitaka, anaweza kukaa kimya," amesema Hakimu.
Baada ya hakimu kusema hayo, wakili wa mshitakiwa alidai kuwa mteja wake atajitetea chini ya kiapo, pia hatokuwa na shahidi wala vielelezo vyovyote na kwamba atajitetea mwenyewe.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 24, mwaka huu kwa ajili ya mshitakiwa kujitetea.
Masahi anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 11, 2023, ikielezwa alimpiga Deogratus Minja kwa nyundo na kumsababishia madhara kwa mwili mwake akiwa eneo la Mbezi Msakuzi, ndani ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake, Minja alidai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake huyo (Masahi), alimkuta kijana wa jirani huyo, ambaye baada ya kumuona alizungumza kwa sauti kubwa kwa lugha ambayo yeye hakuielewa.
"Ghafla kijana alikuja mbele yangu akanizuia nisipite, mara geti likafunguliwa akatoka Masahi, akanihoji kwamba mimi ni kama nani nimekwenda kumshitaki Serikali za Mitaa, sikumjibu chochote, kijana wake akanipiga ngumi," alidai na kuongeza:
"Nilimgeukia jirani yangu ili amuonye kijana wake, lakini na yeye aliinua shati lake, akatoa nyundo, akanipiga nayo kichwani. Baada ya kupata maumivu makali, nilianza kukimbia huku nikipiga kelele za kuomba msaada."
Alidai kuwa hakufika mbali, akaanguka chini, ndipo Masahi akaanza tena kumshambulia kwa nyundo mgongoni, maumivu yalipomzidi aligeuka, akampigwa tena na nyundo kwenye mkono wa kulia na katika bega.
"Jirani mmoja alifungua geti na kunisaidia kwa sababu nilikuwa navuja damu nyingi, ambapo yeye na wenzake walinipeleka Hospitali ya Bochi iliyopo Kimara kwa Musuguri kwa matibabu," amesimulia Minja.
0 Maoni