Hot Posts

6/recent/ticker-posts

'Serikali kuboresha mazingira ya biashara'

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amesema Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na viwanda lengo likiwa kuleta maendeleo endelevu ya jamii.

Waziri wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji 

Dk. Kijaji amesema hayo  Aprili 6, 2024 alipokuwa akifungua kikao cha Wizara hiyo na Wakuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika mkoani Morogoro.

"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendeleza jitihada zake katika kujenga uhusiano mzuri na wafanyabiashara ili kukuza uchimi wa Taifa," amesema.

Ameongeza: “Dunia imeshaingia katika mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo yanajikita katika matumizi makubwa ya teknolojia na utoaji wa huduma kwa haraka, watu kukutana kidigitali na uwepo wa maarifa ya kutosha na bila mipaka kwa jamii ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa njia za kidigitali."

Dk. Kijaji amezitaka wizara na maofisa biashara wa mikoa na wakuu wa idara za biashara, viwanda na uwekezaji kukaa pamoja na kujadili mustakabali wa idara zao kiutendaji pia kukumbushana wajibu wao kutekeleza sera, sheria, kanuni pamoja na taratibu zinazohusu biashara na viwanda katika halmashauri zao.

“Nimewaiteni nikitambua kwamba ndiyo mlioaminiwa kuongoza sehemu na idara za viwanda biashara na uwekezaji katika mamlaka zenu, ili tuyatafsiri na kuyaelewa kwa pamoja majukumu mliyonayo, matarajio na matokeo tarajiwa ya uanzishwaji wa sehemu na idara hizo katika maeneo yenu,” amesema Dk. Kijaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -TAMISEMI, Adolph Ndunguru amesema kuwa mpango wa maendeleo wa Serikali ni kulifikisha taifa katika uchumi shindani na kuboresha masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

 “Kuhakikisha tunachokizalisha kinauzwa, lakini pia kuongeza tija katika uwekezaji ili mpango wetu wa kutengeneza uchumi shindani ufanikiwe kwa kiwango kikubwa,” amesema Ndunguru

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa

Awali, akitoa neno la utangulizi, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amewapongeza Wakuu wa Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushiriki katika mkutano huo.

“Kikao kazi hiki kina lengo la kuwajengea uelewa Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kinahusu Sheria, Kanuni na Taratibu za sajili na utoaji wa leseni zinazosimamiwa na BRELA na namna ambavyo tunaweza shirikiana katika kutekeleza majukumu ya kukuza sekta ya biashara na uwekezaji nchini,"amesema Nyaisa

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda Biashara na Uwekezaji katika Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za mtaa wapatao 200, wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 7 Aprili, 2024 mkoani Morogoro.

Chapisha Maoni

0 Maoni