Hot Posts

6/recent/ticker-posts

FinScope: Asilimia 36 ya Wazanzibar ni tegemezi

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Zaidi ya theluthi ya wananchi wa Zanzibar ni tegemezi, huku asilimia 23 ya wakazi hao wakiishi kwa kutegemea vibarua, matokeo ya utafiti wa FinScope Tanzania 2023 kwa Zanzibar  yamebainisha.

FinScope Tanzania ni utafiti wa kina wa mahitaji ya sekta ya fedha kwa watu wazima Tanzania, walio na umri wa kuanzia miaka 16 na kuendelea.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, katika kipengere cha vyanzo vya mapato, asilimia 17 ya Wazanzibar ni wafanyabiashara,  wanaopokea mishahara ni asilimia tisa, wakulima asilimia nane na makundi mengine asilimia sita.

Dk. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango
 wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Hali hiyo inaweza kutafsiriwa kwamba licha ya juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendeleza wananchi wake, juhudi zaidi zinahitajia katika kupanga, kusimamia na kutekeleza mipango ya kiuchumi na maendeleo inayowahusu moja kwa moja wananchi wa Zanzibar, ili kuondokana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, unaopatikana katika mtandao wa Ofisi wa Taifa ya Takwimu (NBS), idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia nne, kutoka asilimia 30 mwaka 2017 hadi asilimia 36.

Utafiti huo uliogusa maeneo mbalimbali ya Zanzibar kitaifa ikizingatia demografia, umebainisha kwamba Wazanzibar waoishi kwa mishahara ni asilimia 9, wakulima asilimia 8 na makundi mengine wakiwa asilimia 6.

Mkoa wa Kusini Pemba umetajwa na utafiti huo kuongoza kwa kuwa na watengemezi wengi zaidi wanaofikia asilimia 43, vibarua wakiwa asilimia 17, wafanyabiashara wakiwa asilimia 12, wanaopokea mishahara asilimia 12, makundi mengine wakiwa asilimia 9 huku wakulima na wavuvi wakiwa asilimia 6.

Mjini Magharibi unaufuatia Mkoa wa Kusini Pemba kwa kuwa na wategemezi asilimia 42, wafanyabiashara asilimia 21, vibarua asilimia 16,  wenye mishahara kutoka sekta rasmi ni asilimia kumi na moja, makundi mengine asilimia 7 , ambapo wakulima na wafugaji ni asilimia nne pekee.

FinScope katika utafiti wake huo, imeutaja mkoa wa tatu kuwa ni Kaskazini Pemba wenye asilimia 41 na wategemezi, vibarua asilimia 31, wakulima na wavuvi asilimia 16, wafanyabiashara asilimia 12 na wengineo ni asilimia 4.

Mkoa wa Kaskazini Unguja wenyewe umetajwa nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia 33 ya wategemezi, vibarua asilimia 30, wafanyabiashara asilimia 16, wenye mishahara asilimia 4 na makundi mengine asilimia nne.

Mkoa wa tano kati ya mikoa yote ya Zanzibar ni Kusini Unguja, ulio na asilimia 17 ya wategemezi, asilimia 15 ya wakulima na wavuvi, asilimia kama hiyo ya wafanyabiashara, asilimia 10 ya wanaopokea mishahara na asilimia nne ni makundi mengine.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, mwaka 2017 Zanzibar kitaifa ilikuwa na asilimia 27 ya vibarua, wafanyabiashara asilimia 21, wakulima na wavuvi asilimia 10, wenye mishahara asilimia nane na makundi mengine asilimia mbili.

 

  

Chapisha Maoni

0 Maoni