- Awataka kupunguza kero kwa wananchi
-Mkurugenzi BRELA awataka kubadili mtazamo
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Maofisa Biashara nchini, wameonywa wakitakiwa kuepuka rushwa, badala yake kutoa elimu kwa wananchi sanjari na kupunguza kero zinazojitokeza, ikiwemo gharama zisizo halali za urasimishaji biashara.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba leo Januari 9, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Maofisa Biashara kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga, yanayofanyika mkoani Singida.
"Nitoe rai kwenu, mjiepushe na vishawishi vya kuomba au kupokea rushwa katika utoaji huduma zenu, mafunzo haya yakawezeshe kutoa huduma saidizi kwa wananchi kwa weledi na uaminifu, ili yakaonyeshe matokeo chanya kama ilivyokusudiwa na Serikali," amesema Serukamba.
![]() |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akifungua mafunzo ya Maofisa Biashara wa mikoa sita ya Tanzania Bara mkoani Singida leo Januari 9,2024.. |
Amebainisha kuwa Serikali imekuwa ikilipigia kelele mara kwa mara kero zinazojitokeza zikiwagusa wananchi na kutaka zipatiwe ufumbuzi.
“Mafunzo haya ni muhimu, ukizingatia kwamba hivi sasa masuala ya uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo utoaji wa huduma za Leseni za Biashara na Viwanda yanafanyika kwa njia ya mtandao kupitia Mifumo ya Kielektroniki au mifumo ya TEHAMA hivyo muwe sehemu ya kufanikisha haya,” amesema Serukamba.
Amesema ni matumaini yake kuwa, mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa maofisa biashara, kuboresha utoaji huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
"Mafunzo haya ni nyenzo ya kupunguza kero na gharama za urasimishaji biashara, ikiwa ni utekelezaji wa uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini," amesema Serukamba.
Kwa mujibu wa Serukamba, mpango huo wa mafunzo umezingatia umuhimu wa Maofisa Biashara kuwa karibu na wanancha kwa kutoa huduma bora, saidizi na elimishi kwao ili kipato chao kikue, hatimaye Serikali ipate kodi na uchumi wa nchi uweze kuimarika.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida kufungua mafunzo hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, alisema Maofisa Biashara wanatakiwa kubadilisha mtazamo na kutambua majukumu ya idara na kada yao, pia kuachana na mtazamo wa kuwa wakusanya mapato pekee na kufunga biashara.
Amewataka kuwatambua wafanyabiashara katika maeneo yao na kusikiliza kero zao zinazosababisha wafunge biashara na kuzitafutia majawabu ili biashara zao ziendelee kuwepo na kuimarika.
Nyaisa pia amewakumbusha maofisa hao kutambua malengo na majukumu ya idara yao ambayo ni mpya, kuainisha fursa za uwekezaji na kuweka mazingira wezeshi ya kukuza biashara na kuinua uchumi wa halmashauri na mkoa husika.
"Kama mnavyofahamu, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara nchini, ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na viwanda," amesema Nyaisa na kuongeza:
"Hayo yote ni kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya jamii, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP)."
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na BRELA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda na Biashara, yana lengo la kuwajengea uwezo Maofisa Biashara wote nchini.
Tayari mafunzo hayo endelevu, yameshafanyika kwa Maofisa Biashara katika mikoa yote ya Tanzania Bara na yataendelea kutolewa kwa Maofisa Biashara ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo kama haya katika mikoa yote.
0 Maoni