-Awekeza trilioni 4 Dongo Kundu
-Ni katika gesi asilia, apambana na bilionea wa Mombasa
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Bilionea Mtanzania, Rostam Aziz, ameanza ujenzi wa kituo cha gesi asilia ya kupikia (LPG) na eneo la kuhifadhia gesi hiyo katika mji wa Mombasa nchini Kenya, wenye thamani Dola za Marekani bilioni 1.9 sawa na takriban shilingi trilioni 4.55.
Taarifa zinaeleza kuwa, mradi huo ni mwendelezo wa Kampuni ya Taifa Gas inayomilikiwa na Rostam (pichani chini), kutanua wigo wa shughuli zake katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kusini, mbali na Tanzania.
![]() |
Mwenyekiti wa Kampuni za Taifa Group, Rostam Aziz |
Uwekezaji wa sasa nchini Kenya, unatajwa pia kumuweka Rostam katika ushindani wa kibiashara na Mohamed Jaffer anayetajwa kuwa tajiri zaidi mjini Mombasa, akimiliki Kampuni ya Africa Gas and Oil ltd, inayohodhi asilimia 90 ya biashara ya gesi ya kupikia inayoagizwa katika soko la Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapwa na Mtandao wa billionaires.africa za hivi karibuni, , mradi huo wa Rostam nchini Kenya, unatekelezwa katika ukanda maalum wa uwekezaji uchumi wa Dongo Kundu huko Mombasa, huku eneo la kuhifadhia likijengwa Bandari ya Mombasa.
Mtandao huo umemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa Taifa Gas SEZ Kenya, Veneranda Masoum, akieleza kuwa mradi huo unalenga kuleta matokeo chanya ndani ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Mradi huu ni alama muhimu ya uwekezaji kwa Kampuni ya Taifa Gas kutoka ndani ya Tanzania na kusambaa katika Jumuia ya Afrika Mashariki,” amesema Masoum.
Ujenzi wa mradi huo wa LPG unafuatia Serikali ya Kenya kutoa kibali kwa Rostam kufanya uwekezaji huo wa gesi ya kupikia katika Bandari ya Mombasa, ukifuatia makubaliano ya kibiashara yaliyosainiwa Aprili 2022 na Rais wa Kenya wa wakati huo, Uhuru Kenyatta na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Makubaliano hayo yanalenga kupunguza gharama za upakuaji wa gesi asilia ya kupikia kutoka kwenye meli kwenda nchi kavu ili kusaidia kupunguza bei ya gesi hiyo kwa wananchi wa Kenya, ambao asilimia 23.9 wanategemea gesi ya kupikia.
Hatua hiyo ya Rostam kuwekeza Mombasa inaashiria mabadiliko makubwa Afrika Mashariki kwenye sekta hiyo ya gesi ya kupikia, huku ikichagiza ushindani wa kibiashara kati yake na kampuni nyingine kubwa zilizowekeza kwenye sekta hiyo nchini Kenya za Rubis, Total na Vivo zenye wateja wapatao milioni 2.87.
0 Maoni