Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mkapa ataka maofisa biashara kubadilika

-Ataka watimize majukumu kwa ufanisi
-Ni katika idara mpya Biashara Viwanda na Uwekezaji

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Maofisa Biashara nchini wametakiwa kutumia elimu   waliyoipata kubadilisha mitizamo yao na kutekeleza majukumu  ya idara yao mpya ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kwa ufanisi.         

Mkurugenzi wa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Andrew Mkapa, ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya Maofisa Biashara  kuhusu  Sheria ya Leseni za Biashara na Viwanda, yaliyofanyika kwa  siku nne mkoani Singida.  

    

Mkurugenzi wa Leseni wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Andrew Mkapa, akizungumza katika mafunzo ya maofisa biashara mkoani Singida, Januari 12,2024.

"Mafunzo haya yasiishie hapa, tuendelee kuwasiliana hata busara ikatawale zaidi katika kuwasilisha namna ya kuleta mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi," amesema Mkapa na kuongeza:

"Mtakaporejea maeneo yenu ya kazi, tushauriane pale inapohitajika na  tubadilishane uzoefu  juu ya jambo lolote."

Amewashauri maofisa biashara hao kuzingatia mafunzo na maelekezo katika kuleta tija zaidi na ufanisi kwenye idara hiyo mpya ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji.

Akitoa shukrani baada ya mafunzo hayo kwa niaba ya wenzake, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Mpanda, Paul  Kahoya  ameahidi  kwenda kuyatekeleza yote waliyojifunza sanjari na kuzisoma sheria zitakazokuwa mwongozo kwenye utekelezaji majukumu yao. 

Baadhi ya maofisa biashara wakifuatilia mafunzo kuhusu  Sheria ya Leseni za Biashara na Viwanda, yaliyofanyika kwa siku nne mkoani Singida, Januari 12, 2024.


Ameongeza kuwa yote waliyopata ni nyenzo muhimu katika kutekeleza majukumu yao.

"Hivi sasa tumepewa idara, naamini uanzishwaji wa idara hiyo ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji iliyo chini ya  Wizara ya Viwanda na Biashara itatuwezesha kutekeleza majukumu yetu ipasavyo tukitambua kwamba Serikali imeona hatua hiyo itaongeza tija, hivyo tutafanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria na miongozo tuliyopewa," amesema Kahoya. 

Mafunzo hayo  kwa Maofisa Biashara kutoka mikoa ya SIngida, Dodoma, Rukwa, Simiyu, Katavi na Tanga yaliandaliwa na BRELA kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Viwanda na Biashara kwa lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kufanya kazi  kwa ufanisi zaidi.

Chapisha Maoni

0 Maoni