-Makomredi 10 wamtangulia
-WanaCCM matumaini mapya
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Hahika siku hazigandi, Balozi Emmanuel Nchimbi (52), ametangazwa
kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM leo Januari 15,2024 ikiwa zimetimia saa 1,200 sawa na siku 50, tangu kujiuzulu kwa Daniel
Chongolo katika wadhifa huo Novemba 2023.
Mapema leo akili, macho na masikio ya wanaCCM yalielekezwa
Zanzibar, kusubiri mrithi wa nafasi hiyo nyeti ya utendaji ndani ya CCM.
Lakini, taarifa iliyotolewa na CCM kupitia Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda baada ya mkutano huo, pamoja na mambo mengine imeeleza:
"Kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kimepokea pendekezo la Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuhusu jina la Katibu Mkuu wa CCM, Wajumbe wa Halmauri Kuu ya CCM ya Taifa wameridhia kwa kauli moja pendekezo hilo na kumchagua Ndugu Balozi(mst) Dkt. Emmanuel John Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa CCM."
![]() |
Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi. |
Pamoja na Dk. Nchimbi, wengine waliotajwa ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM), Mkuu wa Wilaya na sasa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella akiwemo
pia aliyewahi kuwa Mweka Hazina wa CCM, Amos Makalla, ambaye sasa Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza na aliyekuwa kampeni meneja wa Hayati John Magufuli, Abdallah
Bulembo.
Katika Mkutano huo uliotanguliwa na Mkutano wa Kamati Kuu ya
CCM, sio tu WanaCCM walioelekeza akili, macho na masikio visiwani humo, bali
pia wanasiasa wa vyama vya upinzani, kila mmoja alitamani kujua na kusikia jina
la mtu atakayekabidhiwa mikoba ya ukatibu mkuu wa CCM, kurithi nafasi ya
Chongolo.
Hakuna ubishi kwamba sasa mtu huyo ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi
na ndiye watachuana naye katika kutangaza, kuuza na kutekeleza sera na ilani za
vyama siasa, hasa ikizingatiwa kwamba mwaka huu 2024, kutafanyika uchanguzi wa
Serikali za Mitaa, CCM kikiwa chama tawala huku kikishikilia asilimia kubwa ya
viti katika Serikali za Mitaa nchini.
Wanaomfahamu Dk. Nchimbi wanaeleza kuwa ni tumaini jipya kwa
CCM, wakimuelezea kuwa mtu mwenye uthubutu katika jambo analoliamini, akiwa pia
na ushawishi.
Dk. Nchimbi ambaye ni mwanasiasa mkongwe, anatajwa pia kuwa mwanaCCM mwenye msimamo, ikikumbukwa alipotangaza kujitenga na uamuzi wa CCM kupitia Kamati Kuu yake wakati wa uteuzi wa wagombea urais, ambapo jina la hayati John Magufuli lilipitishwa kuwania urais.
Balozi Nchimbi 'anavaa jezi na 11' ya kuiletea CCM ushindi, kwa kuwa Katibu Mkuu 11 wa chama hicho tangu kuasisiwa kwake tarehe 5, Februari mwaka 1977, kutokana na muungano wa vyama vya
TANU kilichokuwa Tanzania Bara na Afro Shirazi, Zanzibar.
Waliomtangulia ni pamoja na Daniel Chongolo,(2021-2023), Dk.
Bashiru Ally Kakurwa (2018-2021) na Abdulrahman Kinana (2012-2018).
Wengine ni Wilson Mukama (2011-2012), Yusuph Makamba
(2007-2011), Philip Mangula (1997-2007) na Lawrenc Gama (1995-1997).
Wamo pia marehemu
Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa tatu wa CCM (1990-1995), hayati Rashid
Kawawa aliyekuwa Katibu Mkuu wa pili, (1982-1990) na Pius Msekwa katibu Mkuu wa
Kwanza wa CCM (1977-1982).
Taarifa za kihistoria zinaonyesha kuwa Balozi Nchimbi aliyezaliwa Desemba 24, 1971 ni mwanasiasa aliyelelewa na kukulia ndani ya CCM, akianzia Umoja wa Vijana (UVCCM), ambapo aliwahi kuwa mwenyekiti wa Umoja huo.
Mbali na nafasi hiyo, amewahi kuhudumu kwenye serikali akishika
nafasi ya naibu waziri, uwaziri kamili katika Serikali ya Awamu ya Nne,
iliyoongozwa na Jakaya Mrisho Kikwete.
Katibu Mkuu huyo mpya wa CCM, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Habari
mwaka 2006, akitangulia kuwa Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini mwaka 2005 na kuwa
mbunge hadi mwaka 2015.
Mwaka 2006 hadi 2008 alikuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo
ya Vijana, kabla ya mwaka 2008 hiyo hiyo kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 hadi mwaka 2012, Balozi nchimbi aliteuliwa kuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Vijana, ambapo alihudumu hadi mwaka
2012 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani hadi mwaka 2012/2013.
Kuwajibika
Nchimbi alionyesha kuwajibika baada ya kujiuzulu nafasi hiyo ya
Uwaziri wa Mambo ya Ndani, Desemba 2013 kufuatia shinikizo lililoelezwa kutoka
ndani ya vikao vya CCM, ambalo lilitanguliwa na Ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Kamati hiyo ilikuwa chini ya Mbunge wa Kahama wa wakati huo,
James Lembeli, ambapo ilichunguza kuhusu ‘Opeseheni Tokomeza’ iliyotekelezwa
wakati huo.
Mwaka 1998 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM ambapo kabla
alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM (NEC).
Ikumbukwe kuwa Chongolo alijiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu wa
CCM kwa kuandika barua kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan,
Novemba 27, mwaka 2023, kwa kile kilichodaiwa ni kuchafuliwa kwenye mitandao ya
kijamii, akihusishwa na tuhuma mbalimbali.
Rais Samia aliridhia hatua hiyo ya Chongolo na kuwatangazia
wajumbe wa NEC, huku akiagiza vyombo vya dola kuchunguza tuhuma hizo.
0 Maoni