Namba saba inavyoing’arisha WFC

-Makusanyo yapaa zaidi ya sh. bilioni 700
-Inatoa mafao saba, ina faida 7
-Imelipa fidia miaka 7, imetaja mafanikio saba

 

Exuperius Kachenje, daimatz@gmail.com

Ingelikuwa tunazungumzia namba ya bahati, basi tungeweza kuielezea namba saba kuwa ndiyo ya bahati kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi nchini (WCF), unaoakisi kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 700.

Makusanyo hayo ya mapato ni hadi Septemba mwaka huu, yakikua kutoka Sh. bilioni 146 miaka saba iliyopita, mwaka 2017.

Hayo yamebainika wakati Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk.John Mduma akiwasilisha taarifa ya mfuko huo mbele ya wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini Novemba 2,2023 jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kuhusu makusanyo ya michango na fidia zilizolipwa na mfuko huo kwa wafanyakazi kwa miaka saba iliyopita.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dk.John Mduma akiwasilisha maelezo kuhusu mfuko huo, mbele ya Wahariri wa Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya habari nchini Novemba 2,2023 jijini Dar es Salaam.


Katika taarifa hiyo, Mduma amebainisha mapato yaliyokusanywa na WCF kwenye miaka saba ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo akieleza: “ Hadi Septemba mwaka 2023 tumekusanya shilingi bilioni 758.78, mwaka 2022 kipindi kama hicho tulikusanya sh. bilioni 671.87, 2021 tulikusanya sh. bilioni 585.22 na 2020 sh. bilioni 478.29.”

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WCF akaitaja miaka mingine mitatu kati ya saba na makusanyo yake kuwa ni mwaka 2019 ambapo zilikusanywa sh.bilioni 371.84, mwaka 2018 sh. bilioni 262.88 na mwaka 2017 ambao WCF ilikusanya sh. bilioni 146.11.

Katika mkutano huo ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, WCF ilibainisha pia imelipa mafao kwa wafanyakazi kwa kipinzi cha miaka saba, ambayo pia yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kati ya mwaka 2017 hadi mwaka huu 2023.

“Kwa upande wa fidia kwa wafanyakazi, kwa mwaka 2017 WCF ililipa fidia ya shilingi bilioni 1.55, mwaka 2018 sh. bilioni 4.40, mwaka 2019 tulilipa sh.bilioni 9.09 na mwaka 2020 tulilipa fidia inayofikia sh.bilioni 18.18. Lakini mwaka 2021 sh.bilioni 31.38 zililipwa, mwaka 2022 fidia zililipwa sh.bilioni 44.30 na sh.bilioni 62.22 zililipwa kwa mwaka 2023 hadi kufikia Septemba,” alisema Mduma.

Katika wasilisho la Mkurugenzi huyo wa WCF, namba saba iliakisi tena wakati akieleza idadi na aina ya mafao yanayotolewa kwa wafanyakazi wanapoumia kazini na kupoteza uwezo wa kufanya kazi, au uwezo wao kupungua ambapo Mduma amesema kuna aina saba za mafao yanayotolewa na mfuko huo.

Mduma aliainisha mafao hayo saba kuwa ni;  Fao la Matibabu, Fao la Ulemavu wa Muda, Fao la Ulemavu wa Kudumu na  Fao la Kumuuguza Mgonjwa. Mengine ni  Malipo Kwa Wategemezi , Msaada wa Mazishi na Fao la Utengemao.

Akizungumzia usajili wa waajiri, Mkurugenzi Mkuu Mduma, amesema hadi kufikia Septemba30 mwaka 2023 jumla ya waajiri waliosajiliwa ni 31,469 sawa na asilimia 93.33 ya waajiri 33,680 walio katika kanzidata ya WCF.

“Katika mwaka wa fedha 2022/2023, waajiri waliosajiliwa walikuwa 30,866 sawa na asilimia 91.64, mwaka 2021/2022 walisajiliwa 27,786 ambao ni asilimia 82.50, mwaka 2020/2021 walikuwa 25,085 na mwaka 2019/2020 ni waajiri 22,802,” amesema Mduma na kuendelea:

“Mwaka 2018/2019 walisajiliwa waajiri 20,102 sawa na silimia 59.69, mwaka 2017/2018 waajiri 14,836 ambao ni asilimia 44.05,  mwaka 2016/2017 kulikuwa na asilimia 23.33 ya  waajiri ambao ni 7,857 na mwaka 2015/2016 walisajiliwa waajiri 5,178 sawa na asilimia 15.37.”

Akizungumzia mafanikio ya WCF, namba saba pia imehusika baada ya Mduma kunainisha mafanikio saba ambayo WCF imepata na kuyaainisha kuwa ni pamoja na kukipata Hati Safi kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, kuongezeka kwa malipo ya fidia kwa wafanyakazi (mpaka 30/09/2023, TZS bilioni 65.35) na uhai na uendelevu wa kulipa fidia bila kutetereka   kwa mujibu wa Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko ya Mwaka 2022.

 Kwa mujibu wa Mduma, mafanikio mengine ya WCF ni kuimarika uwezo wa kifedha wa Mfuko  kufikia shilingi bilioni 697.83 kwa mujibu wa hesabu za hadi tarehe 30 Septemba 2023, kuboreshwa kwa huduma kupitia usimikaji mifumo ya TEHAMA, kuboreshwa kwa kituo cha huduma kwa wateja (Call Centre) na kuboreshwa kwa tathmini za ulemavu kupitia mafunzo kwa madaktari.

Mkurugenzi huyo wa WCF ametaja mafaniko mengine kuwa ni kuongezeka  kwa wigo wa utoaji huduma kwa kuingia makubaliano na hospitali, watoa huduma mbalimbali za afya nchini na ufunguzi wa ofisi mikoani pamoja na WCF kuwa kinara hata kuzifanya nchi za Zambia, Kenya, Botswana, Afrika Kusini na Zimbabwe kujifunza kutoka mfuko huo.

Katika mkutano huo wa kawaida wa kampuni, mashirika na taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina,WCF pia imeeleza mambo iliyofanya kuboresha mchango wake katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo ni pamoja na kupunguza kwa kiwango cha uchangiaji kwa waajiri wa sekta binafsi kutoka asilimia moja ya awali hadi asilimia sifuri nukta tano.

Baadhi ya Wahariri na Waandishi wa Habari, wakifuatilia mkutano wao na Mkurugenzi Mkuu wa WCF(hayupo pichani) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023


Mengine ni kupunguzwa kwa riba kwa waajiri waliochelewesha michango kutoka asilimia 10 iliyokuwa ikitozwa kwa mwezi hadi asilimia mbili, kufitiwa riba ya malimbikizo ya michango kwa waajiri waliochelewa kulipa na kuongezwa kwa kima cha chini cha fidia kutoka utaratibu wa awali ambao haukuwa na kima cha chini cha fidia kwa mfanyakazi ambaye hakupata ulemavu wa asilimia 100 hadi kufikia sh. 275,702.83.

Kuhusu mwelekeo wa WCF ,  Mduma ametaja hatua mbalimbali yanayokusudiwa ili kutoa huduma bora zaidi ambayo ni pamoja na kupanua wigo wa huduma za utengemao kwa kulipia huduma za mafunzo ya ujuzi mbadala, kulipia huduma za utengemao wa uwezeshaji wa kijamii na kuimarisha huduma za uhakiki wa bili za matibabu kupitia ujenzi wa mifumo stahiki ya TEHAMA.

Mduma amesema, mengine ni kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwamo Jeshi la Polisi, TRA, BRELA na mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii katika kutatua changamoto za kupokea taarifa zisizo sahihi za madai na michango, kujenga jengo la Fidia House Dodoma ili kuimarisha juhudi za kuboresha makao makuu ya nchi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za WCF katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo kupitia ufunguzi na uboreshaji wa ofisi za mfuko huo mikoani.

Mduma alieleza kuwa mfuko huo ulioundwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2015, dira yake ni kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma za fidia kwa wafanyakazi barani Afrika, ukibeba dhima ya kutoa huduma za fidia za kuaminika na fanisi kwa wafanyakazi zitakazowawezesha kukabiliana na athari za kijamii na kiuchumi zitokanazo na ajali mahali pa kazi kwa kuzingatia tunu za uadilifu, ushirikiano, uwajibikaji, ubora na kujali.  

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi

Moshi mweusi watokea Vatican, moshi mweupe wasubiriwa kwa hamu