Siku 21, 900 za Sweden kuwepo Tanzania
-Ni saa miezi 720, miaka 60,
-Misaada ya Sweden yafikia dola bilioni 8
Exuperius Kachenje, daimatz@gmail.com
Unapozungumzia uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni huwezi kuliweka kando Taifa la Sweden.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Sweden ni moja ya mataifa ya awali kufungua ofisi zao za ubalozi hapa Tanzania.
Katika maelezo yake kuhusu uhusiano huo na maadhimisho ya miaka 60 ya Ubalozi wa Sweden hapa Tanzania Oktoba 2023, Balozi wa taifa hilo nchini, Charlota Ozaki anaeleza zaidi.
![]() |
Balozi wa Sweden nchini, Charlota Ozaki |
“Miaka 60 ya uhusiano si jambo dogo, ni kubwa la kujivunia na kupigiwa mfano,”anasema.
Kimahesabu, miaka hiyo ni sawa na siku 21,900, saa 525,600 au miezi 720 na binadamu aliyefikia umri wa miaka 60, anahesabika kufikia uzee.
Lakini balozi Ozaki anasema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Sweden na Tanzania ni wa kihistoria na kwamba hatua hiyo haikuja kwa bahati mbaya.
“Ni kutokana na msingi uliowekwa kabla ya kuzaliwa Tanzania, kwani Sweden ilikuwa na mawasiliano ya kidiplomasia na Tanganyika kabla haijapata uhuru,” anasema Balozi Ozaki.
Tukumbuke kuwa Tanzania ya leo ni zao la muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika mwaka 1964.
Tukiigeukia Sweden, historia inaonyesha kwamba Wamishonari kutoka taifa hilo moja ya nchi za Nordic, walifika Tanzania miaka ya 1930.
Balozi Ozaki anamtaja mmoja wa Wamishonari hao kutoka Sweden walioingia nchini awali kuwa ni Barbro Johansson.
“Mwanamke huyo mashuhuri anahusika katika kukuza uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili, kwani alipofika Tanzania mwaka 1946, akaanzisha shule ya wasichana huko Bukoba,” anaeleza Balozi Ozaki.
Kuhusu sera ya taifa lake kusaidia mataifa yanayoendelea ikiwamo Tanzania, balozi huyo anaeleza:
“Sera rasmi ya misaada ya Sweden ilianza mwaka 1962. Pendekezo la Serikali (1962:100) linaeleza jinsi hatua za kwanza katika uhusiano wa misaada ya Sweden na Tanzania zilivyochukuliwa mapema mwaka 1961,” anasema Balozi Ozaki na kufafanua:
“Wakati huo Kamati maalum ya Mawaziri wa Nordic ya Kuratibu Misaada kwa Nchi Zinazoendelea, ilikubali kuandaa mpango wa msaada katika elimu inayofaa ya kiafrika.”
Anasema baada ya ujumbe wa kutafuta ukweli kuhusu misaada hiyo, Agosti 1961 ambapo iliamriwa kuwa Tanzania iwemo kati ya wnufaika wa misaada ya Nordic, ndipo Sweden ilijitosa na kuanza kutoa misaada.
“Leo, mwaka 2023, Ufalme wa Sweden unaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kimaendeleo na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema Balozi Ozaki akibainisha.
Kati ya mwaka 1962 na 2023, misaada ya Sweden kwa Tanzania ilifikia takriban dola bilioni 8 sawa na takriban shilingi trilioni 20.”
Anaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazopokea misaada mikubwa kutoka Sweden, ikiwa ni nchi ya saba kwa ufadhili wa maendeleo kwa Tanzania kati ya mwaka 1962 hadi 2023.
Kwa mujibu wa Balozi Ozaki, Tanzania pia imefaidika na ushirikiano wa maendeleo na Sweden kupitia msaada kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika mengine ya kimataifa na mashirika ya kiraia ya Sweden na utawala wa taifa hilo.
Akizungumzia kuhusu biashara kati ya Sweden na Tanzania, Balozi Ozaki anasema imeongezeka, kutoka kiwango cha chini hadi takriban dola milioni 80 mwaka 2022, sawa na takriban shilingi bilioni 200.
“Lengo la sera ya misaada ya Sweden ni kuinua hali ya maisha ya maskini, yaani, kupunguza umaskini, lengo ambalo lina matokea chanya,” anasema.
Balozi Ozaki anasema ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden unahusisha takriban sekta zote za jamii, ikiwemo elimu, afya, utamaduni maji, mazingira na nishati, miundombinu, maliasili, sekta binafsi na msaada wa bajeti.
![]() |
Balozi wa Sweden nchini Charlota Ozaki (Wa kwanza kushoto), akishiriki moja ya shughuli za kijamii nchini zilizofadhiliwa na ubalozi huo kuadhimisha miaka 60 ya kuwepo nchini. |
Anasema Sweden na Tanzania pia zimekuwa zikishirikiana katika maeneo mengi kimataifa, kuanzia kuunga mkono harakati za ukombozi katika kupigania uhuru pia kufanya utafiti katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.
Anaongeza:
“Idadi kubwa ya Watanzania wamesoma nchini Sweden au kushiriki katika Mpango wa
Kimataifa wa Mafunzo (ITP).” Anasema katika kipindi
cha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Sweden na Tanzania, mafanikio kadhaa
yamedhihirisha ushirikiano huo akitoa mfano wa
eneo la afya, ambapo Sweden imeunga mkono mipango ya kuboresha
miundombinu ya matibabu na huduma, pia kuchangia maendeleo katika afya ya umma.
Balozi huyo anataja pia sekta ya elimu ambapo Sweden pia imekuwa ikisaidia kukuza taasisi na programu za elimu.
“Hii
imesababisha kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa elimu bora kwa
Watanzania,” anaeleza.
Anabainisha
kwamba, Sweden pia imesaidia kuanzisha mfumo wa utafiti unaofanya kazi katika
vyuo vikuu vitatu ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba Muhimbili(MUHAS), na Chuo Kikuu cha Ardhi, akikitaja MUHAS kuwa
kwa sasa ni mojawapo ya vyuo vikuu vitatu bora vya utafiti barani Afrika.
Kwa upande wa maendeleo endelevu, Balozi Ozaki anasema ushirikiano baina ya Tanzania na Sweden umesaidia miradi inayokuza ulinzi wa mazingira, nishati mbadala na maendeleo endelevu kwa ujumla.
Anasema
juhudi hizo zinaendana na malengo ya dunia na kuchangia katika ustawi wa muda
mrefu wa mazingira na uchumi wa Tanzania.
“Ushirikiano
kati ya Sweden na Tanzania katika sekta ya nishati ulianza kwa ujenzi wa mtambo
wa kufua umeme wa Kidatu na kufuatiwa na mitambo mingine ya kuzalisha umeme kwa
maji,” anadokeza.
Ozaki anasema kwa miaka mingi, misaada ya Sweden imewekezwa katika upanuzi wa mitambo, uzalishaji wa umeme, usambazaji wa umeme, kujenga uwezo na usaidizi wa kitaasisi.
Balozi huyo anabainisha kwamba kanuni ya msingi ya ushirikiano wa Sweden na Tanzania ni utawala bora wa kidemokrasia na haki za binadamu na kwamba Sweden inaunga mkono maendeleo ya sekta binafsi, kwa kuzingatia zaidi viwanda vidogo na sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Kwa
mujibu wa balozi huyo, ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi hizo mbili,
umefungua njia za biashara na uwekezaji.
“Ili kusherehekea miaka 60 ya ushirikiano wa maendeleo, Ubalozi wa Sweden hapa Tanzania umeandaa na utaendelea kuandaa matukio na shughuli kwa mwaka mzima, zinazoangazia mambo mbalimbali ya ushirikiano wetu wa muda mrefu, kwa kuzingatia mustakabali wa ushirikiano huo,” anahitimisha balozi Ozaki.
Maoni
Chapisha Maoni