-Ni miezi minane tangu kuteuliwa
-Atembelea mikoa tisa ya NHC
Mwandishi Wetu,
Bukoba
Kwa wafuatiliaji wa mchezo wa mpira wa miguu yaani soka, anaelewa umuhimu wa namba nane na tisa kwenye mchezo huo, kwani anayecheza
namba nane ndiye kiungo anayesukuma mpira kwa washambuliaji, huku namba tisa
akisukuma mashambulizi na kufunga magoli.
Hata hivyo, ingawa nafasi hizo za namba nane na tisa
huchezwa na watu tofauti, lakini Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Tanzania
(NHC), Hamad Abdallah ameweza kucheza nafasi hizo mbili peke yake katika
kuhakikisha anatimiza majukumu yake ya kuliongoza shirika hilo la taifa.
Mkurugenzi huyo amecheza nambari nane kwani Oktoba hii ametimiza miezi minane tangu alipoteuliwa na Rais Samia kuiongoza NHC Februari 23, mwaka huu akichukua nafasi ya Nehemia Mchechu, ambaye ameteuliwa kuwa Msajili wa Hazina.
Si hivyo tu, bali Hamad pia amehitimisha ziara ya mikoani ambapo ametoa maagizo na maelekezo nane yenye
lengo la kulisukuma mbele shirika hilo kiutendaji na kujiongezea kipato katika
kuchangia maendeleo ya taifa.
Hamad pia amecheza namba tisa kwa kuwa amefanya ziara katika
mikoa tisa ya NHC, aliyoikamilisha katika Mkoa wa Kagera mwishoni wa wiki
iliyopita, hivyo kuitia chachu mpya katika utendaji mikoa hiyo na kuipa ushindi
NHC katika kutekeleza majukumu yake kwa taifa kuhakikisha Watanzania wanakuwa
na makazi bora.
Mkurugenzi huyo amekamilisha
ziara yake katika mikoa ya Shirika, huku akiacha tabasamu, matumaini na ari
mpya kwa wafanyakazi katika mikoa hiyo.
Ziara hiyo ilimuwezesha Hamad kukutana ana kwa ana na wafanyakazi katika mikoa hiyo pamoja na kukagua miradi na rasilimali mbalimbali za NHC.
Ameihitimisha ziara yake mjini Bukoba, ambapo pamoja na kutembelea miradi iliyopo
Chato mkoani Geita, nyumba za shirika Mjini Bukoba na jengo la kibiashara
lilipo mpaka wa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula, Mkurugenzi Mkuu Hamad ameonyesha
kufurahishwa na ari na ubunifu wa hali ya juu, uliofanywa na Mkoa wa Kagera kuongeza
mapato ya mkoa huo.
Mambo hayo ni pamoja na wafanyakazi wote kufanya kazi kwa upendo, mshikamano kama familia moja ili shirika liweze kufikia malengo yake na kupata faida kubwa.
"Tuishi kwenye miiko ya shirika inayosisitiza uadilifu
na ushirikiano. Tuishi kama familia moja, ukiona mwenzio anakosea, mwambie tu
kwa nia njema, hakuna mtu ambaye ni malaika, vumilianeni," amesisistiza
Mkurugenzi Mkuu.
Ameongeza: “Wafanyakazi wote wanapaswa kuwa na upendo, kutakiana mema na kuhakikisha hakuna majungu, lakini pia muwe wepesi wa kusameheana kwa kuwa hakuna anayejua kesho yake.
Muwe ‘positive’(Mawazo mema)
wakati wote na kumtegemea Mungu kwa kila jambo, mjue kuwa kazi mbaya ukiwa nayo,
lakini ikikuponyoka utaitafuta na hutaipata kirahisi, tunzeni kazi zenu."
Amesisitiza kuwa kazi ni kipimo cha utu na kwamba kila mtu
akijibidisha vizuri NHC itapata tija na kubadilisha maisha ya kila mfanyakazi.
Mkurugenzi Mkuu amerejea kuhimiza wafanyakazi wote
kushirikiana katika kukusanya kodi na malimbikizo yaliyopo, pia kubuni mambo
yatakayoliongezea shirika mapato.
"Ukusanyaji wa
kodi ya nyumba za NHC ni kipaumbele kikubwa kwa kuwa hiki ni chanzo muhimu cha
mapato ya shirika,"amesema.
Kwa mujibu wa Hamad, mikoa ya NHC inapaswa kuwa na mikakati
ya kukusanya kodi, ikiwemo kuhakikisha kila mpangaji ana amana ya pango, pamoja
na kuhakikisha wapangaji wasiolipa kodi kwa wakati hawapewi mikataba mipya.
"Kusanyeni kodi kwa ushirikiano na hakikisheni mnakusanya malimbikizo yote. Kila
mpangaji awe na amana ya pango ifikapo Desemba 2023,” amesema.
Hamadi amerejea kauli yake kwamba ili kufikia malengo ya shirika, kila
mfanyakazi wa NHC atimize wajibu wake kwa mujibu wa ajira yake, akaagiza
Mameneja, Wakuu wa Idara na Kurugenzi kuhakikisha kuwa upimaji wa utendaji kazi
unafanyika kwa haki, kikamilifu na kuangalia majukumu ya kila mfanyakazi, ili
kila mmoja ijulikane tija anayoliingizia shirika.
"Pimeni utendaji
kazi wa kila mfanyakazi kwa haki bila kuonea mtu ili kila anayestahili
apewe motisha inayomstahili, iwe hasi au
chanya," Hamad ameasa.
Kuhusu motisha kwa
watumishi, Hamad amebainisha kuwa Menejimenti ya NHC imeanza kufuatilia uboreshaji
motisha kwa wafanyakazi, ikiwemo malipo ya mshahara wa mwezi mmoja kwa
kila likizo na kwamba nia ya menejimenti ni kuona kila mfanyakazi anafurahia
kuwa sehemu ya familia ya NHC.
"Wafanyakazi wanadanganya maeneo walikozaliwa ili wapate nauli kubwa ya kwenda likizo. Hili tunaenda kulimaliza kwa kulipa kila anayekwenda likizo mshahara wake wa mwezi mmoja;
Mazungumzo
na Msajili wa Hazina yanakamilishwa ili tuanze kutekeleza motisha ya likizo kwa
wafanyakazi. Mimi ni mtu wa haki, nikiahidi jambo natekeleza, mkichapa kazi kwa
bidii, tukapata tija, tutaongezana mishahara katika mwaka huu wa fedha," Hamad
aliahidi.
Akizungumzia miradi ya ubia iliyosimama kwa muda mrefu bila
kukamilika, Hamad amesema kuwa NHC imeanza kuchukua hatua za kurejesha miradi
hiyo chini ya shirika ili ikamilishwe.
“Tayari tuna miradi miwili tumeshairudisha mikononi mwa NHC,
iliyopo jijini Arusha na hata Mwanza tumenza kufanya mazungumzo na wabia, yenye
lengo la kuwanyang'anya miradi minne ambayo haijaendelezwa kwa muda mrefu."
"Tumieni lugha nzuri kwa wateja wetu, andikeni barua za wateja bila kuonyesha hasira wala jazba, maana maandishi yanadumu muda mrefu.
Shirikianeni katika kuwahudumia wateja na
muisemee NHC na Serikali vyema. Shirika lina sifa nzuri ni vyema tukailinda
sifa hiyo."anasema Hamad.
Kuhusu ajira mpya ndani ya NHC, Mkurugenzi Mku, Hamad amerejea
kueleza kuwa, ajira hizo zitatekelezwa hivi karibuni, lakini kwa kufuata ikama
na mahitaji ya watumishi yaliyopo, kipaumbele kikiwa kwa wafanyakazi wa
mikataba wanaolitumikia shirika hivi sasa kwa uaminifu na uzalendo mkubwa.
Hamad amewataka wafanyakazi hao kuendelea kuchapa kazi kwa
weledi na uaminifu ili ajira hizo zikitoka wawe na sifa za kuajiriwa.
Akizungumzia uuzaji wa nyumba za gharama nafuu zilizopo chini ya NHC, Hamad
ameitaka mikoa yenye nyumba hizo ukiwemo Mkoa wa Kagera, eneo la Chato na
Muleba kuanza kutafuta wanunuzi wa nyumba hizo ili kuliondolea shirika mzigo
mkubwa wa kuzitunza nyumba hizo, ambazo nyingi zimeanza kuchakaa.
"Tulijenga nyumba hizi ili tuziuze, naona zimechakaa
sana na zitatugharimu kila mara, menejimenti ya NHC inapitia bei ya kuuzia
nyumba hizi na itatolewa hivi karibuni ili muanze kuziuza,” amesema Hamad.
Akizungumzia uadilifu na uaminifu katika kusimamia miradi na
mali za shirika, Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema jambo hilo ni kipaumbele cha
kila mfanyakazi wa NHC, akawataka kuhakikisha kuwa usimamizi wa miradi na
rasilimali za NHC vikiwemo vifaa vya ujenzi katika miradi vinalindwa na kila
mfanyakazi ili shirika lipate faida iliyokusudiwa.
"Kila mfanyakazi ana wajibu wa kuhoji mwenendo wa
usimamizi wa miradi, utunzanji wa mali za NHC na kuelezana ukweli pale
tunapoona kuna ufujaji wa mali za shirika," amesema Mkurugenzi Mkuu na kusisitiza: “Hili siyo
suala la Makao Makuu pekee, bali kila mmoja awe mlinzi wa mali za shirika.”
Katika ziara hiyo
Mkurugenzi Mkuu Hamad ameupongeza Mkoa wa Kagera kwa kuwa kinara katika kujua
kila kinachoendelea kwenye miradi ya shirika iliyopo Chato akieleza kwamba huo
ni mfano wa kuigwa na kila mkoa wa NHC.
Ameusifu pia kwa kuwa
na ubunifu wa kuongeza mapato na kuwa na kiu kubwa ya kuendeleza maeneo muhimu
yanayomilikiwa na shirika katika mkoa huo.
"Mmenipa
uchambuzi mzuri wa uanzishwaji wa miradi na namna miradi hiyo itakavyorudisha
fedha za shirika zitakaxowekezwa hapa, nimependa sana ubunifu wenu wa
kibiashara," amehitimisha Mkurugenzi Mkuu Hamad.
NAMBA NANE ALIYOCHEZA
1-Kwa kusisitiza upendo, umoja na kuzingatia maadili ya msingi ya
shirika.
2-Kwa kuhimiza uadilifu na uaminifu ili kuongeza tija
3-Kuhimiza kipaumbele makusanyo
ya kodi, ubunifu kwa kuongeza mapato ya NHC
4- Usimamizi miradi ya ujenzi kikamilifu kwa uzalendo
5- Ataka kila mfanyakazi kuwa mlinzi wa mali za shirika
6- Ataka huduma bora kwa wateja izingatiwe
7- Atangaza miradi ya ubia isiyoendelezwa kutwaliwa
8- Aahidi bonasi, nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi
NAMBA TISA ALIYOCHEZA
Kutembelea mikoa tisa ya NHC ziara iliyotia chachu mpya ya utendaji katika kutimiza majukumu ya NHC
Awali, akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Kagera, Meneja wa NHC
Mkoa huo, Deogratius Batakanwa
amemshukuru Mkurugenzi Mkuu Hamad kwa
ubunifu wake wa kupeleka rangi katika mikoa yote ambayo wameanza kuutumia
kutengeneza nyumba na kupendezesha nyumba hizo.
Ameelezea kuwa siri ya mafanikio ya mkoa huo ni mshikamano na kuwa na mikakati ya kuwajengea umoja na uwajibikaji ikiwemo kuwa na timu ya michezo, kuwa na ‘breakfast meeting’, kuwa na ‘checkpoint’ katika tarehe za mwezi za kutathmini ukusanyaji wa mapato kwa asilimia na kuwa na ‘champion of the month’, ambaye huwa kama kiranja wa zamu wa mwezi husika, anayeratibu utekelezaji wa kila jambo katika mkoa na kukumbusha kwa anayejisahau kutekeleza wajibu wake, kupitia "breakfast meeting".
Batakanwa amesema wilayani Ngara kuna fursa ya ujenzi wa
nyumba kutokana na uwepo wa mradi wa ‘Nickel’
na kwamba mkoa wake utahakikisha kuwa kila fursa inayojitokeza wataitumia ili
kuongeza mapato ya NHC.
Katika ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu alifuatana na Mkurugenzi
wa Rasilimali Watu na Utawala Fatma Chillo, ambaye aliwaeleza wafanyakazi namna
NHC inatakavyoondoa uhaba wa wafanyakazi katika ikama ya shirika kwa mfumo wa ‘job enrichment na job enlargement’, ambapo alizungumzia upandishwaji wa madaraja kwa
mserereko akisema ni jambo litakalotekelezwa na NHC yenyewe bila kupitia
utumishi.
Mkurugenzi Mkuu na ujumbe wake wamerejea jijini Dar es
Salaam, akiwa ameacha furaha na matumaini mapya kwa wafanyakazi wa NHC, ambao
walimpokea kwa bashasha na kuelezea kwa uwazi changamoto zinazoikabili mikoa
hiyo na kuahidi kuzipatia ufumbuzi.
0 Maoni