Jumanne, 28 Novemba 2023

Msajili Hazina kuwa Mfuko wa Uwekezaji

 -Lengo kuongeza tija

-Yasiyo faida kuchukuliwa hatua 

 Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Msajili wa Hazina (TR),  Nehemiah Mchechu amesema, Ofisi yake ipo mbioni kufanyiwa marekebisho kisheria na kuwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (PIA), lengo likiwa kuongeza tija kwenye  Taasisi za Umma inazozisimamia.

Amesema kutokana na mabadiliko hayo, taasisi hizo zinapaswa kuzalisha kwa ajili kugharamia mipango binafsi iliyonayo na ile ya Serikali, akionya kwamba mashirika yasiyofanya vizuri itabidi yachukuliwe hatua.

 Mchechu amebainisha hayo leo Novemba 28, 2023, katika Kikao Kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Msajili huyo wa Hazina, matarajio ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuona taasisi hasa za kibiashara, zinazalisha faida na kuingizwa Serikalini au kujiendesha bila kutegemea Serikali Kuu.

"Kwa hali hiyo ni lazima kuwepo mabadiliko, ili kuziongezea tija na ufanisi taasisi hizo" amesema Mchechu na kufafanua:

"Katika mabadiliko hayo, tutaangalia kwa nini haya yanafanya vizuri. Yale yasiyofanya vizuri itabidi tuchukue hatua." 

Msajili huyo wa Hazina ameeleza kwamba yapo mashirika ya kimkakati yasiyofanya vizuri na kwamba pamoja na hali hiyo, Serikali haitayaacha, bali itaendelea kuyasimamia na kufanyia kazi mapungufu husika.

“Tutaanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma, kazi yake itakuwa kuzisaidia taasisi kuimarisha mtaji,lengo ni kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi  duniani," amesema Mchechu.

Ameeleza kwamba kwa sasa Msajili wa Hazina anawajibika kusimamia utendaji wa taasisi zote za umma, pia amepewa mamlaka ya kuwekeza na kusimamia uwekezaji katika taasisi, lakini wigo uliopo ni finyu.

Mchechu amesema, kuna mambo manne ambayo lazima yazingatiwe ili kuongeza ufanisi katika taasisi hizo.

"Mambo hayo ni pamoja na taasisi kuwa na uongozi bora, kuwa na rasilimali za kutosha, kutoingiliwa mambo yake na nne ni kupima utendaji," amesema.

Akitoa mfano Mchechu amesema: "Sasa tuna vigezo vipya, zamani kulikuwa na vigezo ambavyo havikuzingatia sekta. Sasa unapoisimamia Tanesco au Muhimbili, kazi zao ni tofauti hata vigezo, lazima vigezo na asili ya taasisi inayofanya kazi viendane na sekta husika.” 

Amesema mabadiliko ya kimfumo tayari yameanza ndani ya ofisi yake na kuwataka watendaji wa taasisi zilicho chini ya ofisi hiyo kujiweka tayari kwa kujipanga.

Amedokeza kuwa kutokana na mabadiliko hayo yaliyokwishaanza, yatawagusa watendaji wakuu wa taasisi na bodi, ambapo si ajabu mtendaji wa taasisi binafsi akahamishiwa taasisi ya umma.

Ofisi ya Msajili wa Hazina ina taasisi za umma 298, zilizo chini yake, ambapo kwa mujibu wa Mchechu 248 ni taasisi, wakala wa Serikali, mashirika ya umma, huku 50 zikiwa kampuni zenye hisa chache za Serikali ndani na nje ya Tanzania.

Msajili wa Hazina,  Nehemiah Mchechu, akizungumza wakati wa Kikao Kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari, jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2023.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza kwenye mkutano wa Msajili wa Hazina,  Nehemiah Mchechu na Wahariri wa Vyombo vya Habari, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wakifuatilia mkutano na wahariri

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari, wakifuatilia Kikao Kazi kati ya Wahariri na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchecu, jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2023.

Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, wakiwa pamoja na Wahariri wa Vyombo vya Habari, kwenye Kikao Kazi baina ya Wahariri na Msajili wa Hazina,  jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023.


Katibu Mkuu Chongolo yupo, hayupo?

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana amefungua semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, leo Novemba 28 jijini Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana akifungua semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, leo Novemba 28 jijini Dar es Salaam. 


Wakati Kinana akifungua semina hiyo, kitendawili kinabaki ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo yupo au hayupo kwenye nafasi yake, kufuatia kuenea kwa taarifa kwamba ameandika barua ya kujiuzulu.

Tayari, barua inayodaiwa kuandikwa na Chongolo jana Novemba 27, 2023 kwenda kwa mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, imeonekana kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, CCM bado ipo kimya kuhusu taarifa hizo, hata Kinana hakueleza chochote kuhusu mtendaji huyo mkuu wa Sekretarieti wakati akifungua semina hiyo, aliyoielezea kwamba itawafundisha mada tofauti kuhusu uongozi, maadili na uwajibikaji kwa chama na Serikali.

Iwapo taarifa hizo za kujiuzulu Chongolo ni za kweli, CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itakuwa na kibarua cha kumteua Katibu Mkuu mpya wa chama hicho tawala na kikongwe barani Afrika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa(wa pili kulia), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla(wa tatu) na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko (wa nne) na wajumbe wengine, wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, leo Novemba 28 jijini Dar es Salaam.


Wakati hayo yakiendelea, majina ya makada mbalimbali wa CCM yanatajwa kwamba huenda mmoja akarithi mikoba ya Chongolo.

Baadhi ya wanaotajwa ni Balozi Dk.Emmanuel Nchimbi, Ali Happy, Abdallah Bulembo na Amos Makala.



Jumatatu, 27 Novemba 2023

Wasanii 10 wenye 'maokoto' zaidi Afrika Mashariki 2023

-Diamond, Harmonize, Kiba watajwa

-Profesa Jay, Lady Jay Dee waibuka, Tanzania ikizoa nafasi tano,

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waswahili husema, biashara asubuhi, jioni ni mahesabu. Usemi huu unaweza kuulinganisha na matokeo ya kufunga mwaka ya viwango vya maokoto kwa wasanii wa muziki Afrika Mashariki katika mwaka 2023 unaoishia, yakibainisha wasanii kumi bora, huku Mtanzania Diamond Platnumz, akitajwa kushika nafasi ya pili.

Katika matokeo hayo yaliyotolewa na Jarida maarufu la Forbes, leo Novemba 27, mwaka 2023, pamoja na Diamond Plutnumz, wametajwa pia wengine wanne, wakiwemo wakongwe Professor Jay  na Lady Jay Dee kuwa miongoni mwa wasanii wanaoongoza kwa utajiri Afrika Mashariki kwa mwaka 2023.

Msanii Diamond Platnumz (Picha zote kwa hisani ya Mtandao)

Diamond ametajwa na jarida hilo kushika nafasi ya pili kwa utajiri Afrika Mashariki katika mwaka 2023, kwa kumiliki ukwasi unaofikia Dola za Marekani milioni 9.1. Fedha hizo ni sawa na takriban shilingi bilioni 21.84, akiongoza pia kwa utajiri mbele ya Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa kwenye orodha hiyo.

Matokeo hayo yaliyotajwa kuhusisha pia mtandao wa Ugwire.com, yamemtaja  Diamond Plutnumz kuwa ndiye msanii anayetafutwa na kufuatiliwa zaidi kupitia mtandao wa Google, kuwa na wafuasi wengi zaidi, akiwa pia maarufu zaidi kwenye ukanda huo.

Diamond anatanguliwa na Msanii Bobi Wine wa Uganda, ambaye pia ni mwanasiasa na kiongozi wa upinzani nchini Uganda, aliyewahi kumtikisa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni wakati alipowania urais nchini humo uchaguzi uliopita mwaka 2021.

Msanii Bobi Wine

Wine anamiliki utajiri unaofikia Dola 9.2 (shilingi bilioni 22.08), akimzidi Diamond kwa takriban shilini milioni 240 pekee.

Katika orodha hiyo, anayeshika nafasi ya tatu ni Mwimbaji Akothee wa Kenya anayetajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola milioni 9, sawa na wastani wa shilingi bilioni 21.60, huku wa nne akiwa Jose Chameleon wa Uganda ambaye kwa mwaka 2023 ametajwa kumiliki utajiri wa Dola milioni 8 (shilingi bilioni 19.2).

Msanii Professor Jay

Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa na Forbes ni pamoja na Profesa Jay anayeelezwa kusika nafasi ya tano, ambapo anamiliki utajiri unaofikia Dola milioni 7.5 kwa mwaka huu, ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 18.

Profesa Jay, amefuatiwa na  Msanii Ali Kiba aliyeshika nafasi ya sita, ambaye kwa mujibu wa Forbes, hadi leo Novemba 27, mwaka 2023 ana utajiri wenye thamani ya Dola milioni 7.2, sawa na takriban shilingi bilioni 17.28.

Msanii Ali Kiba

Nafasi ya saba katika orodha hiyo amewekwa Msanii Jaguar kutoka Kenya, anayetajwa kuwa na ukwasi wenye thamani  ya Dola milioni 6.9, takriban shilingi bilioni 16.56 na nafasi ya nane pia imeshikwa na Saut Sol wa nchini humo, wenye umiliki wa Dola milioni 6.8(shilingi bilioni 16.32)

Jarida hilo la Forbes, limemtaja Mtanzania mwingine, Harmonize kushika nafasi ya tisa kwa utajiri Afrika Mashariki katika mwaka huu wa 2023, akimiliki ukwasi wenye thamani ya Dola milioni 6.6 ambazo zikibadilishwa kwa fedha za kitanzania, zitakuwa sawa na takriban shilingi bilioni 15.84.

Msanii Harmonize

Msanii Lady Jay Dee, maarufu kama Binti Machozi  au Komando ndiye aliyefunga ndimba la wasanii 10 matajiri zaidi Afrika Masharikikwa mwaka 2023, akielezwa kumiliki utajiri unaofikia Dola 6.5 ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15.60.

Lady Jay Dee ndiye msanii pekee wa kike aliyeingia kwenye orodha hiyo, akiwa pia miongoni mwa wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

Msanii Lady Jay Dee


 

 

 

Ruto Rais tajiri zaidi Afrika Mashariki 2023

 -Yumo kati ya 10 matajiri zadi Afrika
-Awaacha mbali King Mswati, Ramaphosa
-Kagame amfuatia

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wakati zimesalia takriban siku 34 kuumaliza mwaka 2023, sawa na mwezi mmoja na siku tatu, orodha ya marais 10 wanaoongoza kwa utajiri barani Afrika imewekwa hadharani, ikimtaja Rais William Ruto wa Kenya kuwa kinara wa utajiri ukanda wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2023.
Orodha hiyo imechapwa na Jarida la Forbes mtandaoni leo tarehe 27 Novemba 2023, likimtaja Ruto kumiliki utajiri unaofikia Dola za Marekani  milioni 510, sawa na takriban shilingi trilioni 1.22.

Rais William Ruto wa Kenya (Kushoto), akisalimiana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Nairobi wakati Dk Samia alipofanya ziara nchini Kenya mapema Juni mwaka huu 2023.



Kutokana na utajiri huo, jarida hilo limemtaja Ruto kushika nafasi ya nne kati ya marais kumi matajiri zaidi Afrika katika mwaka 2023.

Katika orodha hiyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda anatajwa kushika nafasi ya sita kwa utajiri barani Afrika kwa kumiliki Dola milioni 460(Sh. Trilioni 1.10), akiwa pia wa pili ukanda wa Afrika Mashariki, huku yeye na Ruto wakiwa pekee walioingia katika orodha hiyo ya marais 10 wanaoongoza kwa utajiri Afrika.
Rais Paul Kagame(Kulia) na Cyril Ramaphosa. Wawili hao
walikutana katika mkutano wa Russia na viongozi wa nchi za Afrika.


Kwa mujibu wa orodha hiyo ya marais matajiri zaidi Afrika kwa mwaka 2023, Ruto amemzidi Mfalme Mswati  III, anayetajwa kushika nafasi ya tano, akitajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 500 sawa na takriban shilingi trilioni 1.2.

Orodha hiyo inaonyesha kuwa Mfalme Mswati III, ndiye anayeongoza kwa utajiri ukanda wa Kusini mwa Afrika, akifuatiwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrikakusini, anayemiliki ukwasi unaofikia Dola milioni 450, sawa na takriban shilingi trilioni 1.08.
Mfalme Mswati III

Forbes imemtaja Ramaphosa kushika nafasi ya saba kwa utajiri barani Afrika kwa mwaka 2023.
Jarida hilo maarufu Afrika, limemtaja Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco kushika nafasi ya kwanza kwa utajiri barani humo akimiliki utajiri unaofikia Dola za Marekani bilioni 5.9 (Sh. trilioni 1,416), akiongoza pia kwa utajiri ukanda wa Afrika Kaskazini.

Hata hivyo, Forbes limeeleza kuwa orodha hiyo iliyoitoa haijumuishi marais wote tajiri Afrika kwa mwaka 2023 badla yake ni viashiria vya udhaifu na nguvu ya uzalishaji ndani ya nchi husika.

Anayemfuatia Mfalme Mohammed wa Sita ni Rais Ali Bongo wa Gabon anayemiliki utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni mbili (Sh. Trilioni 4.8), huku wa tatu akitajwa kuwa ni Rais Teodoro Nguema wa Guinea ya Ikweta akishikilia utajiri wa Dola za Marekani Milioni 700 (Sh. Trilioni 1.68).
Mfalme Mohammed wa Sita


Kwa kiwango hicho cha ukwasi, Nguema pia anaongoza miongoni mwa marais tajiri ukanda wa Afrika Magharibi, akifuatiwa na Rais Paul Biya wa Cameron aliye na utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 210 (Sh. Bilioni 504).

Forbes,limemtaja Rais Biya kushika nafasi ya nane katika orodha ya marais tajiri zaidi Afrika mwaka 2023, huku nafasi ya tisa ikishikiliwa na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ambaye ametajwa kumiliki ukwasi unafikia Dola za Marekani milioni 200 (Sh.bilioni 480).

Katika orodha hiyo inayofunga mwaka huu wa 2023,kiongozi wa Eritrea, Isaias Afwerki anatajwa kushika nafasi ya kumi, akitajwa kumiliki utajiri unaothaminishwa kuwa sawa na Dola za Marekani milioni 120 (Sh.bilioni 288).

Kwa mujibu wa Jarida la Forbes katika miongo kadhaa, Afrika imekuwa ikijulikana kuwa bara tajiri kutokana na kujaliwa wingi wa maliasili duniani, lakini mara nyingi wanufaika wakubwa wa rasilimali hizo ni viongozi wake.

IFUATAO NI MTIRIRIKO WA MARAIS 10 MATAJIRI

ZAIDI AFRIKA KWA MUJIBU WA FORBES

1.       Mfalme Mohammed VI, Morocco- Dola bilioni 5.9

2.       Rais Ali Bongo, Gabon- Dola bilioni 2

3.       Rais Teodoro Nguema, Guinea ya Ikweta- Dola Milioni 700

4.       Rais William Ruto, Kenya- Dola milioni 510

5.       Mfalme Mswati, Swaziland-Dola milioni 500

6.       Rais Paul Kagame, Rwanda- Dola milioni 460

7.       Rais Cyril Ramaphosa, Afrikakusini-Dola milioni 450

8.       Rais Paul Biya, Cameron-Dola milioni 210

9.       Rais Abdel Fattah el-Sisi, Misri- Dola milioni 200

10.   Isaias Afwerki, Eritrea-Dola milioni 120

Jumanne, 14 Novemba 2023

Kumbe watoto huugua kisukari

-Ni wa umri kuanzia mwaka mmoja
Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com
Wakati dunia leo imeungana kuadhimisha Siku ya Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kisukari, inayoadhimishwa Novemba 14 ya kila mwaka, bado yapo maswali kuhusu ugonjwa huo, moja likiwa: je watoto huugua kisukari?
Jibu la swali hilo kitaaluma ni ndiyo na kwamba ugonjwa huo umegawanyika katika makundi matatu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Afya, Viashiria na Malaria, watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi miezi 23, wapo hatarini kupata ugonjwa wa kisukari.
Hali hiyo inatajwa kusababishwa na kubadilika kwa mtindo wa maisha na malezi, lakini pia kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi.
Ripoti hiyo ya mwaka 2022 iliyoandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) nchini inaonyesha kuwa kundi hilo lipo katika hatari kupatwa na kisukari pamoja na kuongeza uzito uliopitiliza.
Aina tatu za Kisukari
Aina ya kwanza
Aina hii huwapata watoto kati ya mwaka mmoja na 24.
Watoto hupatwa na aina hii kutokana na tatizo la kongosho kutoa insulini kidogo au kukoma kutoa jimeng'enya hicho. 
Dalili za mtoto kuugua aina ya kwanza ya kisukari ni pamoja na kuongezeka kwa kiu, kukojoa mara kwa mara, njaa, kupungua uzito ghafla na udhaifu.
Kisukari aina ya kwanza ni huanza wakati seli zinazotengeneza insulini (seli za beta) zinapoharibiwa kwa kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. 
Ikumbukwe kuwa Insulini ni homoni inayohitajika kwa seli kutumia sukari ya damu kwa ajili ya kuzalisha nishati, ikiwa na kazi ya kudhibiti kiwango cha sukari katika mzunguko wa damu.
Kwa aina hii ya kisukari, kuna dalili za ziada ambazo ni uoni hafifu, uchovu na majeraha kuchukua muda mrefu kupona.
Kisukari aina ya pili
Aina hii hjwapata watu wazima kati ya miaka 25 - 70 au zaidi, chanzo kikuu kikiwa mtindo mbaya wa maisha hasa ulaji na kutofanya mazoezi.
 Hali hii husababisha mwili kushindwa kudhibiti na kuitumia sukari kama nishati hivyo kusababisha sukari nyingi kuzunguka kwenye damu. 
Matokeo ya hali hiyo, viwango vya juu vya sukari kwenye damu inaweza kusababisha matatizo ya mfumo wa mzunguko, wa neva na wa kinga.
Kimsingi kisukari aina ya pili kina shida mbili, moja ni  kongosho kushindwa kuzalisha insulini ya kutosha kuzalisha insulin na pili kuzalisha kimeng'enyo hicho kwa kiasi kikubwa.
Kisukari kwa Wajawazito
Hii ni aina ya tatu ya kisukari, ambapo wanawake hupatwa na kisukari, ambayo huwa juu kwenye damu. 
Dalili za tatizo hili ni mjamzito kupatwa na kiu ya kupita kiasi, kukojoa mara kwa mara na kutokwa na jasho jingi.

Jumatatu, 13 Novemba 2023

Papa Fransisko amuweka kando askofu

-Ni Joseph Strickland wa Marekani

Vatican,

Baba Mtakatifu Francisko, amemsimamisha Askofu Joseph Strickland(65), kutoa huduma ya Kichungaji ndani ya Kanisa Katoliki.

Kufuatia uamuzi huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Joe Vásquez, wa Austin, kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo hilo. 

Papa Fransisko(kushoto), Askofu Strickland (kulia)

Kwa mujibu wa Vatican, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani ametangaza uamuzi huo baada ya ziara ya kitume ya maaskofu, Juni 2023 katika Jimbo la Tyler.

Kadinali Daniel Nicholas Di Nardo, Askofu Mkuu wa Mji Mkuu wa Galveston-Houston, alitoa barua yake, iliyobainisha kwamba maaskofu waliofanya ziara hiyo, walikuwa ni Askofu Dennis Sullivan, wa Camden, na askofu mstaafu Gerald Kicanas, wa Tucson.

Amesema maaskofu hao walifanya uchunguzi wa kina katika nyanja zote za utawala na uongozi wa Jimbo la Tyler pamoja na Askofu Joseph Strickland.

"Baada ya miezi kadhaa, uamuzi umetolewa," amesema Kardinali Di Nardo.

Sehemu ya ripoti hiyo inaendelea kusomeka: “Kutokana na ziara hiyo, pendekezo lilitolewa kwa Baba Mtakatifu kwamba haiwezekani Askofu Strickland kuendelea tena na huduma ndani ya Kanisa Katoliki."

Ripoti ya ziara hiyo inaelezwa ilitoa miezi kadhaa ya tafakari kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Baba Mtakatifu, ambapo amuzi ulifikiwa kumwomba Askofu Strickland ajiuzulu.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Novemba 9, 2023 Askofu Strickland alitoa tamko akikataa kujiuzulu.

"Kwa hiyo ni uamuzi wa Papa  kumwondolea majukumu askofu huyo. Wakati tukingojea masharti maalum  zaidi kwa Jimbo la Tyler, tunamkumbuka Askofu Strickland katika sala zetu, pia tunawaombea mapadre na waamini wa Jimbo la Tyler na Askofu Vásquez," amesema Kardinali DiNardo.


Jumapili, 12 Novemba 2023

Hatari yako, majibu ya kisukari

 Mwandishi Wetu

Novemba 14 kila mwaka kama kesho, ulimwengu wa wadau wa afya huadhimisha Siku ya Ugonjwa wa Kisukari Duniani, ambao ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza unaosumbua watu wengi zaidi duniani.

Kutokana na ukweli huo, kila binadamu yupo katika hatari ya kupatwa na ugonjwa huo, lakini pengine kuwa na maswali kuhusu kisukari.

Kwa mwaka huu 2023,  maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa mkoani Dar es Salaam, huku katika mikoa yote nchini ikiadhimishwa kwa wananchi kupata fursa ya kupima na kujua hali zao kuhusu kisukari.

Mkoani Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja pia wananchi wanapewa fursa ya kupima bure baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza kuanzia tarehe 14  hadi 18/11/2023.

Maadhimisho hayo yanafanyika yakiongozwa na kauli mbiu isemayo: "IJUE HATARI YAKO, FAHAMU MAJIBU YAKO".

Wakati hayo yakiendelea, kwa niaba ya Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza nchini (TANCDA), ifuatayo ni makala fupi inayoeleza hatari na majibu kuhusu kisukari, ambao wataalam wanaeleza upo katika makundi matatu, ambayo ni: Kisukari aina ya Kwanza, Kisukari aina na Pili na Kisukari kwa Wajawazito.

Ni kweli kwamba huenda ni mimi au wewe au ndugu na jamaa zetu wapo kwenye dalili za kupata ugonjwa wa kisukari au tuunaishi au wanaishi na ugonjwa wa kisukari. 

Ni jukumu la kila mmoja wetu kujua hatari ya ugonjwa huu wa kisukari na kuchukua taadhari.

Baadhi ya visababishi vya ugonjwa wa kisukari ni pamoja na ukosefu wa mazoezi na ushugulishaji mwili, matumizi ya sukari nyingi kwenye vyakula na vyinjwaji na unjwaji wa pombe uliopitiliza na uvutaji wa tumbaku na bidhaa zake.

Dalili za Ugonjwa wa Kisukari.

Kukojoa mara kwa mara, kuhisi kiu mara kwa mara, kuhisi njaa kila wakati, kupoteza uzito. Uoni hafifu, uchovu, na uponyaji wa polepole wa jeraha. 

Jinsi ya Kujikinga na Ugonjwa wa Kisukari.

Fanya mazoezi angalau dakika 30 kwa siku mara 5 kwa wiki.

Epuka matumizi ya sukari iliyopitiliza kwenye chakula na vinjwaji.

Epuka unjwaji wa pombe uliopitiliza.

Epuka uvutaji wa tumbaku na bidhaa zake.

Mtindo bora wa maisha huu hapa

 -TANCDA yataka watu wajifunze kubadilik-

-Magonjwa yasiyoambukiza huchangia asilimia 33 ya vifo 

Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani, kuadhimisha Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza,(WMY), ambayo hufanyika Novemba ya kila mwaka, kuanzia tarehe 11 hadi 17.

Kwa mwaka huu kitaifa wiki hiyo inafanyika mkoani Dar es Salaam, huku magonjwa hayo yasiyoambukiza yakitajwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya vifo vya mapema duniani.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), katika kila vifo vitatu, kimoja kinasababishwa na Magonywa Yasiyoambukiza (MY), huku yakitajwa kusababisha asilimia 33 ya vifo hapa nchini.

Hata hivyo, wataalam wa afya wanaeleza kuwa Mtindo Bora wa Maisha ndiyo suluhu ya kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Mwenyekiti wa TANCDA, Profesa Andrew Swai, pichani juu, ameeleza kuwa sababu kubwa za magonjwa hayo ni mtindo mbaya wa maisha katika ulaji na kutofanya mazoezi, zikiwamo pia vinasaba vya kurithi.

Profesa Swai amesema kuwa kutokana na hali hiyo TANCDA wameandaa kitabu cha elimu kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza kinachotolewa bure pia kupatikana mtandaoni.

"Tunataka watu wapate elimu hii bure, wajifunze na kubadilika ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza, madhara yake na vifo," amesema Profesa Swai.

Ili kupata elimu zaidi fuatilia ukurasa huu, utapata bure nakala mtandao ya kitabu hicho au bofya:

 

https://shorturl.at/yCEHM





Ijumaa, 10 Novemba 2023

Takukuru yakunjua makucha Kigoma

-Wakandarasi ' watemeshwa bungo' 

Mwandishi Wetu,Kigoma

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa Mkoa wa Kigoma (TAKUKURU) imebaini upungufu mkubwa katika miradi 33 yenye thamani ya shiligi bilioni 12.5, iliyoifuatilia, ikionyesha kuwa chini ya kiwango.

Kufuatia uchunguzi huo, wazabuni wawili waliobanwa na Takukuru, mmoja amerudisha fedha zadi ya shilingi milioni 125 na mwingine kuwasilisha mabati mapya kwenye mradi.

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa Kigoma, Leonida Mushama amesema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji ya taasisi Takukuru mkoani humo kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba mwaka huu.

Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa Kigoma, Leonida Mushama akiwasilisha taarifa ya Takukuru mkoani humo.
Alitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, Stephen Mafipa.

Mushama amesema kuwa katika miradi hiyo pia ipo miradi ya ujenzi wa madarasa inayotekelezwa kwa mpango wa BOOST, yenye thamani ya takriban shilingi bilioni tatu.

Amesema Takukuru imebaini upungufu  kwenye ununuzi wa mabati yenye thamani ya shilingi milioni 241.3 katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Halmashauri ya Wilaya Kasulu.

Tayari Takukuru  imeanzisha uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua kwa  watumishi wa halmashauri hizo waliotajwa kuhusika na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Mushama, katika hatua za awali,  Mzabuni wa Kampuni ya Kiboko katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu aliwasilisha mabati mengine yenye viwango yenye thamani ya shilingi milioni 129  wakati yule wa Kampuni ya HERICON katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu alirudisha fedha.

Amesema Mushama kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na wataalam wa halmashauri kuwa na watu wao kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi ambao huelekeza kamati za ujenzi na usimamizi wa miradi kwenda kununua vifaa kwa watu hao kwa ajili ya maslahi binafsi ya wataalam hao wa halmashauri.

Miradi mingine iliyochunguzwa na TAKUKURU ni pamoja na ujenzi wa madarasa saba yenye thamani ya shilingi milioni 195.2 wilayani Kakonko, ujenzi wa shule mpya ya Msingi Kazilamihunda wilaya ya Kakonko wenye thamani ya shilingi milioni 361.5 na.

Aidha miradi mingine iliyochunguzwa na kukutwa na mapungufu ni ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na matundu 22 ya vyoo shule ya msingi Mahembe na ukarabati wa nyumba tano za walimu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 180.


Wafanyabiashara Kisarawe 'walilia' TRA

Mwandishi Wetu, Kisarawe 

WAFANYABISHARA wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani, wameiomba Mamlaka ya Mapato (TRA), kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi kwa hiari na matumizi ya mashine za EFD.

Ombi hilo limetolewa na wafanyabishara wilayani humo, wakati wa mkutano wao na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara (JWT), wakiongozwa na Mwenyekiti wake Hamis Livembe, wakiwa kwenye ziara ya kikazi ya kusikiliza kero mkoani humo.

Mfanyabishara Christina Mulu, amesema TRA wanatakiwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi badala ya kukazania kukusanya bila kuwasikiliza wafanyabishara kwanza.

"Wafanyabiashara wengi hatuna elimu ya kodi, matumizi ya EFD hatujui wakati mwingine risiti zinagoma kutoka na mashine kusumbua sasa TRA wakija wao ni kutaka tu kutoza faini badala ya kutupa elimu kwanza," amesema Mulu.

Mfanyabishara John Masine, amewataka TRA kuwasaidia wafanyabishara urahisi wa kupata kodi na kuwalinda kwa kuondoa wamachinga mbele ya fremu za biashara.

"Mfanyabishara amekodi nyumba analipa kodi TRA, lakini anakuja mmachinga anaweka kibanda mbele yake na anauza bidhaa zinazofanana kwa bei ya chini zaidi na wala halipi kodi yoyote TRA zaidi ya ushuru wa serikali ya mtaa na hakuna anayejali zaidi ya kutaka kukamua kodi bila kujua tunauza au laa," amesema Masine.

Naye Mfanyabishara Ester Moshi, ametaka wafanyabishara kutofunga biashara siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambayo ni siku ya usafi kwasababu wanakwamisha shughuli za kiuchumi.

"Siyo kwamba siku hiyo biashara hazifanyiki hapana, zinafanyika lakini kwa kujificha na kukimbizana wakati serikali inaweza kupunguza muda ikawa muda wa kufungua ni saa 2 badala ya 4  asubuhi," amesema Moshi.

Naye Ofisa wa TRA wilayani humo, Mohamed Chifu, ameushukuru uongozi wa JWT, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusikiliza kero za wafanyabishara lakini pia kutoa majibu ya kina kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu.

Amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo TRA wilayani humo ni wafanyabishara wengi kuwa wa hali ya kati ambapo wanalipa kodi ndogo.

"Wengi wao wanalipa kodi ya ndogo kwa sababu ya halihalisi ya biashara, haujawa mji wa biashara kubwa. Kero ambazo zinatuhusu nimezibeba na naahidi nitaziwasilisha na kuzifanyia kazi," amesema.


Mwisho

Waziri Mkuu akemea wathamini wababaishaji

 -Awataka kushirikiana na wathaminj binafsi kuchochea maendeleo


Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea tabia ya baadhi ya wathamini wanaokiuka miiko ya kazi hiyo akiwataka kuwa waadilifu, weledi na wazingatie miiko ya taaluma kwenye kazi zao za kila siku.

Majaliwa ametoa karipio hilo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wathamini unaofanyika kwa siku mbili, jijini Dodoma ambapo ameeleza kuwa wathamini ni watu muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua mkutano mkuu wa Watahamini, jijini Dodoma, Novemba 10, 2023.

 “Kazi ya uthamini si ya wababaishaji au vishoka, kila mthamini hana budi kuthamini na kuheshimu taaluma yake, ninyi mnapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia thamani halisi ya ardhi, jengo au chochote kinachofanyiwa uthamini,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza: 

“Kuna baadhi ya wathamini  si waadilifu na kwa kushirikiana na watendaji wengine, hutoa makadirio yasiyowiana na thamani halisi, hivyo kusababisha kupoteza mapato ya Serikali, lakini pia kuwanyima haki wanaostahili kupata haki." 

Amewataka pia wathamini hao kutumia mkutano huo kufanya majadiliano ya kina kuhusu masuala ya taratibu za utwaaji ardhi na sheria zake, ukokotozi wa fidia katika maeneo ya madini, viwango vya thamani ya ardhi na mazao, changamoto za kisera za utwaaji ardhi pamoja na kupata suluhu ya malalamiko ya wananchi.

Badhi ya Watahamini, wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wao mkuu, jijini Dodoma, Novemba 10,2023


Waziri Mkuu Majaliwa, pia amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hasa wathamini kushirikiana na sekta binafsi katika kufanya kazi zao za uthamini.

 “Tumieni fursa ya uwepo wa wathamini binafsi ili kutoa huduma bora na kwa haraka, mkifanya hivyo mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya ushirikishaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Majaliwa. 


Rais Dk.Samia atimua Bodi, afanya uteuzi



Jumatano, 8 Novemba 2023

Bilionea Rostam Aziz aigeukia Zambia

 -Amwaga mabilioni ya fedha


Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com


Bilionea Mtanzania, Rostam Aziz ametangaza kutanua uwekezaji wake kwa kufanya uwekezaji mpya, safari hii akiwekeza nchini Zambia kiasi cha Dola za Marekani milioni 100 katika sekta ya nishati na madini.

Rostam ambaye pia ni Mwenyekiti wa kampuni za Taifa Group inayofanya kazi ukanda wa Afrika Mashariki amefanya uamuzi wa kuwekeza fedha hizo, sawa na takriban shilingi bilioni 250, unaoashiria kuwa na mkakati wa kupanua zaidi wigo wa uwekezaji wake kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan(kushoto) akishuhudia Mfanyabiashara Rostam Aziz, akitia saini moja ya mikataba ya kibiashara katika moja ya ziara za Rais nje ya nchi.


Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na Mtandao wa billionaires.africa za hivi karibuni, Rostam  anayetajwa kumiliki utajiri mkubwa barani Afrika, tayari amekutana na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Oktoba 20 mwaka huu 2023, ambapo walijadili kuhusu maeneo yenye fursa na vivutio vya uwekezaji kwenye sekta ya nishati na madini nchini humo.

Mkutano huo unatajwa kuchagiza hatua zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.

Taarifa hizo mpya za uwekezaji nchini Zambia zinafuatia taarifa za takriban miezi mitano iliyopita, zilizoitaja Kampuni ya Taifa Gas, kueleza mkakati wake wa kutaka kuwekeza katika uzalishaji umeme nchini Zambia, mradi uliotajwa pia kugharimu Dola za Marekani milioni 100 (sh bilioni 250).

 

Mradi huo wa umeme unaelezwa utaimarisha uwepo wa kampuni ya Taifa Gas kusini mwa Afrika ukiimarisha pia mtandao wa biashara na kuongeza fursa kibiashara baina na Tanzania na Zambia.


Akizungumzia uwekezaji huo, Rostam alikaririwa akieleza kuwa Zambia ni eneo linalovutia kwa uwekezaji zaidi na kwamba Taifa Gas itahakikisha uhusiano kati ya Zambia na Tanzania unazidi kukua na kuendeleza fursa za uwekezaji katika nishati na madini.

“Tutahakikisha Tanzania na  Zambia zinakuza uhusiano na moyo wa ushirikiano kwa maendeleo endelevu ya nchi hizo jirani, ninafurahi kwamba tayari tuna mshirika ndani ya Zambia, nasi kama Taifa Gas tutatumia vizuri fursa hii ya uwekezaji kwa maslahi ya nchi zetu mbili za Afrika,” amesema Rostam.

Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 58, amesema anaheshimu mwaliko wa Rais wa Zambia, akitoa wito kwa wawekezaji wengine barani Afrika kuwekeza mitaji Zambia, huku akiahidi kuongeza wigo wa uwekezaji nchini humo na kwamba uwekezaji wake ni wa ushirikiano na mwekezaji raia wa nchi hiiyo.

Rostam alitambuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kumiliki utajiri unaofikia Dola bilioni na mtandao wa Forbes, mwaka 2013, kutokana na biashara na uwekezaji mbalimbali ikiwamo katika kampuni za simu, usafiri wa anga, nishati, madini, gesi na sekta ya nyumba.

 

 

Jumanne, 7 Novemba 2023

JOWUTA yawasilisha maoni Kamati ya Nape

-Wataka waandishi waungane kudai na kulinda maslahi

Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimekabidhi maoni yake kuhusu hali ya uchumi kwa vyombo vya habari na wanahabari mbele ya Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi wa Vyombo vya Habari Tanzania.

Ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Suleiman Msuya, aliyeongozana na Naibu wake, Said Mmanga na Mjumbe wa Bodi ya chama hicho, Careen Tausi Mbowe, JOWUTA ilikabidhi maoni yake leo Novemba 7, 2023 kwa Mjumbe wa Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi kwa Vyombo vya Habari na Waandishi, Sebastian Maganga.  

Katibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Suleiman Msuya akikabidhi maoni ya chama hicho kwa Mjumbe wa Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi kwa Vyombo vya Habari na Waandishi, Sebastian Maganga. Wengine pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga(Kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya JOWUTA, Careen Tausi Mbowe.Kulia ni Mtaalam wa Kamati, Dk. Abdallah Katunzi.


Akizungumza baada ya kukabidhi maoni hayo, Msuya amesema: "Tunashukuru kupata fursa, sisi JOWUTA kwa mujibu wa sheria, ndiyo tunawajibika moja kwa moja kwa waandhishi wa habari kisekta. Katika mukhtadha huo, tumeona mambo matatu hayajazingatiwa. Sheria ya Ajira kazini inataka kila mtu akifanya kazi miezi mitatu apewe mkataba, lakini haipo hivyo wa waandishi wengi."

Alifafanua: "Pili, pia sheria ya uwekezaji tumeona haikuzingatiwa, mtu anapowekeza kwenye vyombo vya habari hicho ni kiwanda, kinakuwa na wafanyakazi wa vitengo mbalimbali, ambavyo baadae vitaiwezesha Serikali kupata kodi ya asilimia 10, (pay as you earn), hivyo kuchangia maendeleo ya Taifa, lakini kwa kuwa wanahabari wengi hawana mikataba ya ajira, hilo la kuchangia halipo. Wanahabari hawachangii pato la taifa, kwani hawana mishahara. Tunaomba Serikali isaidie kusimamia eneo la uwekezaji kwenye sekta ya habari ili nao wachangie uchumi moja kwa moja."

Katibu Mkuu huyo wa JOWUTA, amewataka wanahabari kutojirahisisha wanapotafuta ajira, badala yake kushikamana kwa nguvu moja katika kudai na kulinda maslahi yao.

"Lakini jingine muhimu wanahabari tusiwe rahisi, lazima tushikamane tuwe na nguvu moja katika kusimamia maslahi na haki zetu," amesema Msuya.

Januari 24, mwaka huu 2023, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye alitangaza kuunda tume ya watu tisa, ambao  wataofanya kazi ya Kutathimini hali ya uchumi katika vyombo vya habari nchini.

Mbele ya waandishi wa habari, Waziri Nape alitangaza kamati hiyo  Jijini Dodoma, akieleza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alimuagiza kushughulikia suala la uchumi kwenye vyombo vya habari.

Aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu Azam Media Group, Tido Mhando ambaye ni Mwenyekiti, huku katibu wa kamati hiyo akiwa Gerson Msigwa, aliyekuwa Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Bakari Machumu( Mkurugenzi Mtendaji MCL), Joyce Mhavile (Mkurugenzi Mtendaji ITV na Redio One), Dk. Rose Reuben (Mkurugenzi Mkuu TAMWA) na  Keneth Simbaya (Mkurugenzi Mtendaji UTPC).

Wengine ni Sebastian Maganga (Mkuu wa Maudhui Clouds Media), Jacqueline Woiso (Mkurugenzi Mtendaji Multichoice Tanzania) na Richard Mwaikenda Mwandishi wa kujitegemea.

Awali, katika maelezo yake kuhusu kamati hiyo Waziri Nape alisema: "Baada ya majadiliano, tumefikia uamuzi wa kuunda timu ambayo itakwenda kufanya kazi ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari,wanahabari na kuleta mapendekezo." 



Mazingira: Serikali kujenga ukuta fukwe za Nungwi



Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni Dodoma kuhusu wizara yake.




 
.



Jumatatu, 6 Novemba 2023

JWT yaanza ziara kusikiliza kero za wafanyabishara Pwani

Mwandishi Wetu, Pwani

JUMUIYA ya Wafanyabiasha nchini (JWT) imeanza ziara ya kikazi ya kusikiliza kero za wafanyabishara katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani.

Lengo la ziara hiyo ni kusikiliza kero za wafanyabishara, wenye viwanda na kampuni ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kuepuka changamoto ikiwamo migomo ya mara kwa mara.

Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe, akiongozana na viongozi wengine mapema leo wamewasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kufanya mazunguzo na Katibu Tawala, Rashid Mchatta kabla ya kuanza mikutano yao.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, (katikati)akizungumza na ujumbe wa JWT walipomtembelea ofisini kwake, kabla ya ziara yao mkoani humo.

Livembe amesema, Rais Samia anawapenda wafanyabishara ndio sababu amewaagiza wasikilize kero zao ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema wafanyabishara wakiungana wanaweza kujisemea na kumaliza kero zao bila kufunga biashara wala kufanya vurugu hivyo ni muhimu kujitokeza kwenye mikutano hiyo.

Naye Mchatta ameipongeza jumuiya hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuisaidia serikali kusikiliza kero hizo nchi nzima na kuzifilisha kwenye mamlaka husika.

"Niwasihi tu viongozi wa JWT msiache kuwaelimisha wafanyabishara umuhimu wa kulipa kodi pamoja hayo wazingatie tahadhari za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini," amesema.