Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Msajili Hazina kuwa Mfuko wa Uwekezaji

 -Lengo kuongeza tija

-Yasiyo faida kuchukuliwa hatua 

 Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Msajili wa Hazina (TR),  Nehemiah Mchechu amesema, Ofisi yake ipo mbioni kufanyiwa marekebisho kisheria na kuwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (PIA), lengo likiwa kuongeza tija kwenye  Taasisi za Umma inazozisimamia.

Amesema kutokana na mabadiliko hayo, taasisi hizo zinapaswa kuzalisha kwa ajili kugharamia mipango binafsi iliyonayo na ile ya Serikali, akionya kwamba mashirika yasiyofanya vizuri itabidi yachukuliwe hatua.

 Mchechu amebainisha hayo leo Novemba 28, 2023, katika Kikao Kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Msajili huyo wa Hazina, matarajio ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuona taasisi hasa za kibiashara, zinazalisha faida na kuingizwa Serikalini au kujiendesha bila kutegemea Serikali Kuu.

"Kwa hali hiyo ni lazima kuwepo mabadiliko, ili kuziongezea tija na ufanisi taasisi hizo" amesema Mchechu na kufafanua:

"Katika mabadiliko hayo, tutaangalia kwa nini haya yanafanya vizuri. Yale yasiyofanya vizuri itabidi tuchukue hatua." 

Msajili huyo wa Hazina ameeleza kwamba yapo mashirika ya kimkakati yasiyofanya vizuri na kwamba pamoja na hali hiyo, Serikali haitayaacha, bali itaendelea kuyasimamia na kufanyia kazi mapungufu husika.

“Tutaanzisha Mfuko wa Uwekezaji wa Umma, kazi yake itakuwa kuzisaidia taasisi kuimarisha mtaji,lengo ni kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi  duniani," amesema Mchechu.

Ameeleza kwamba kwa sasa Msajili wa Hazina anawajibika kusimamia utendaji wa taasisi zote za umma, pia amepewa mamlaka ya kuwekeza na kusimamia uwekezaji katika taasisi, lakini wigo uliopo ni finyu.

Mchechu amesema, kuna mambo manne ambayo lazima yazingatiwe ili kuongeza ufanisi katika taasisi hizo.

"Mambo hayo ni pamoja na taasisi kuwa na uongozi bora, kuwa na rasilimali za kutosha, kutoingiliwa mambo yake na nne ni kupima utendaji," amesema.

Akitoa mfano Mchechu amesema: "Sasa tuna vigezo vipya, zamani kulikuwa na vigezo ambavyo havikuzingatia sekta. Sasa unapoisimamia Tanesco au Muhimbili, kazi zao ni tofauti hata vigezo, lazima vigezo na asili ya taasisi inayofanya kazi viendane na sekta husika.” 

Amesema mabadiliko ya kimfumo tayari yameanza ndani ya ofisi yake na kuwataka watendaji wa taasisi zilicho chini ya ofisi hiyo kujiweka tayari kwa kujipanga.

Amedokeza kuwa kutokana na mabadiliko hayo yaliyokwishaanza, yatawagusa watendaji wakuu wa taasisi na bodi, ambapo si ajabu mtendaji wa taasisi binafsi akahamishiwa taasisi ya umma.

Ofisi ya Msajili wa Hazina ina taasisi za umma 298, zilizo chini yake, ambapo kwa mujibu wa Mchechu 248 ni taasisi, wakala wa Serikali, mashirika ya umma, huku 50 zikiwa kampuni zenye hisa chache za Serikali ndani na nje ya Tanzania.

Msajili wa Hazina,  Nehemiah Mchechu, akizungumza wakati wa Kikao Kazi na Wahariri wa Vyombo vya Habari, jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2023.


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza kwenye mkutano wa Msajili wa Hazina,  Nehemiah Mchechu na Wahariri wa Vyombo vya Habari, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wakifuatilia mkutano na wahariri

Baadhi ya Wahariri wa Vyombo vya Habari, wakifuatilia Kikao Kazi kati ya Wahariri na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchecu, jijini Dar es Salaam, Novemba 28, 2023.

Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, wakiwa pamoja na Wahariri wa Vyombo vya Habari, kwenye Kikao Kazi baina ya Wahariri na Msajili wa Hazina,  jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023.


Chapisha Maoni

0 Maoni