-Amwaga mabilioni ya fedha
Mwandishi
Wetu, daimatz@gmail.com
Bilionea Mtanzania, Rostam Aziz ametangaza kutanua uwekezaji
wake kwa kufanya uwekezaji mpya, safari hii akiwekeza nchini Zambia kiasi cha
Dola za Marekani milioni 100 katika sekta ya nishati na madini.
Rostam ambaye pia ni Mwenyekiti wa kampuni za Taifa Group inayofanya
kazi ukanda wa Afrika Mashariki amefanya uamuzi wa kuwekeza fedha hizo, sawa na
takriban shilingi bilioni 250, unaoashiria kuwa na mkakati wa kupanua zaidi
wigo wa uwekezaji wake kwenye ukanda wa kusini mwa Afrika.
![]() |
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan(kushoto) akishuhudia Mfanyabiashara Rostam Aziz, akitia saini moja ya mikataba ya kibiashara katika moja ya ziara za Rais nje ya nchi. |
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na Mtandao wa billionaires.africa
za hivi karibuni, Rostam anayetajwa
kumiliki utajiri mkubwa barani Afrika, tayari amekutana na Rais wa Zambia, Hakainde
Hichilema, Oktoba 20 mwaka huu 2023, ambapo walijadili kuhusu maeneo yenye
fursa na vivutio vya uwekezaji kwenye sekta ya nishati na madini nchini humo.
Mkutano huo unatajwa kuchagiza hatua zaidi katika kukuza
ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.
Taarifa
hizo mpya za uwekezaji nchini Zambia zinafuatia taarifa za takriban miezi
mitano iliyopita, zilizoitaja Kampuni ya Taifa Gas, kueleza mkakati wake wa
kutaka kuwekeza katika uzalishaji umeme nchini Zambia, mradi uliotajwa pia
kugharimu Dola za Marekani milioni 100 (sh bilioni 250).
Mradi
huo wa umeme unaelezwa utaimarisha uwepo wa kampuni ya Taifa Gas kusini mwa
Afrika ukiimarisha pia mtandao wa biashara na kuongeza fursa kibiashara baina
na Tanzania na Zambia.
Akizungumzia uwekezaji huo, Rostam alikaririwa akieleza kuwa
Zambia ni eneo linalovutia kwa uwekezaji zaidi na kwamba Taifa Gas itahakikisha
uhusiano kati ya Zambia na Tanzania unazidi kukua na kuendeleza fursa za
uwekezaji katika nishati na madini.
“Tutahakikisha Tanzania na Zambia zinakuza uhusiano na moyo wa ushirikiano
kwa maendeleo endelevu ya nchi hizo jirani, ninafurahi kwamba tayari tuna
mshirika ndani ya Zambia, nasi kama Taifa Gas tutatumia vizuri fursa hii ya
uwekezaji kwa maslahi ya nchi zetu mbili za Afrika,” amesema Rostam.
Bilionea huyo mwenye umri wa miaka 58,
amesema anaheshimu mwaliko wa Rais wa Zambia, akitoa wito kwa wawekezaji
wengine barani Afrika kuwekeza mitaji Zambia, huku akiahidi kuongeza wigo wa
uwekezaji nchini humo na kwamba uwekezaji wake ni wa ushirikiano na mwekezaji raia
wa nchi hiiyo.
Rostam
alitambuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kumiliki utajiri unaofikia Dola bilioni na
mtandao wa Forbes, mwaka 2013, kutokana na biashara na uwekezaji mbalimbali
ikiwamo katika kampuni za simu, usafiri wa anga, nishati, madini, gesi na sekta
ya nyumba.
0 Maoni