-Yumo kati ya 10 matajiri zadi Afrika
-Awaacha mbali King Mswati, Ramaphosa
-Kagame amfuatia
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Wakati zimesalia takriban siku 34 kuumaliza mwaka 2023, sawa
na mwezi mmoja na siku tatu, orodha ya marais 10 wanaoongoza kwa utajiri barani
Afrika imewekwa hadharani, ikimtaja Rais William Ruto wa Kenya kuwa kinara wa
utajiri ukanda wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2023.
Orodha hiyo imechapwa na Jarida la Forbes mtandaoni leo tarehe
27 Novemba 2023, likimtaja Ruto kumiliki utajiri unaofikia Dola za
Marekani milioni 510, sawa na takriban
shilingi trilioni 1.22.
![]() |
Rais William Ruto wa Kenya (Kushoto), akisalimiana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Nairobi wakati Dk Samia alipofanya ziara nchini Kenya mapema Juni mwaka huu 2023. |
Kutokana na utajiri huo, jarida hilo limemtaja Ruto kushika nafasi ya nne kati ya marais kumi matajiri zaidi Afrika katika mwaka 2023.
Katika orodha hiyo, Rais Paul Kagame wa Rwanda anatajwa kushika nafasi ya sita kwa utajiri barani Afrika kwa kumiliki Dola milioni 460(Sh. Trilioni 1.10), akiwa pia wa pili ukanda wa Afrika Mashariki, huku yeye na Ruto wakiwa pekee walioingia katika orodha hiyo ya marais 10 wanaoongoza kwa utajiri Afrika.
![]() |
Rais Paul Kagame(Kulia) na Cyril Ramaphosa. Wawili hao walikutana katika mkutano wa Russia na viongozi wa nchi za Afrika. |
Kwa mujibu wa orodha hiyo ya marais matajiri zaidi Afrika kwa mwaka 2023, Ruto amemzidi Mfalme Mswati III, anayetajwa kushika nafasi ya tano, akitajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 500 sawa na takriban shilingi trilioni 1.2.
Orodha hiyo inaonyesha kuwa Mfalme Mswati III, ndiye anayeongoza kwa utajiri ukanda wa Kusini mwa Afrika, akifuatiwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrikakusini, anayemiliki ukwasi unaofikia Dola milioni 450, sawa na takriban shilingi trilioni 1.08.
![]() |
Mfalme Mswati III |
Jarida hilo maarufu Afrika, limemtaja Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco kushika nafasi ya kwanza kwa utajiri barani humo akimiliki utajiri unaofikia Dola za Marekani bilioni 5.9 (Sh. trilioni 1,416), akiongoza pia kwa utajiri ukanda wa Afrika Kaskazini.
Hata hivyo, Forbes limeeleza kuwa orodha hiyo iliyoitoa haijumuishi marais wote tajiri Afrika kwa mwaka 2023 badla yake ni viashiria vya udhaifu na nguvu ya uzalishaji ndani ya nchi husika.
Anayemfuatia Mfalme Mohammed wa Sita ni Rais Ali Bongo wa Gabon anayemiliki utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni mbili (Sh. Trilioni 4.8), huku wa tatu akitajwa kuwa ni Rais Teodoro Nguema wa Guinea ya Ikweta akishikilia utajiri wa Dola za Marekani Milioni 700 (Sh. Trilioni 1.68).
![]() |
Mfalme Mohammed wa Sita |
Kwa kiwango hicho cha ukwasi, Nguema pia anaongoza miongoni mwa marais tajiri ukanda wa Afrika Magharibi, akifuatiwa na Rais Paul Biya wa Cameron aliye na utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 210 (Sh. Bilioni 504).
Forbes,limemtaja Rais Biya kushika nafasi ya nane katika orodha ya marais tajiri zaidi Afrika mwaka 2023, huku nafasi ya tisa ikishikiliwa na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ambaye ametajwa kumiliki ukwasi unafikia Dola za Marekani milioni 200 (Sh.bilioni 480).
Katika orodha hiyo inayofunga mwaka huu wa 2023,kiongozi wa Eritrea, Isaias Afwerki anatajwa kushika nafasi ya kumi, akitajwa kumiliki utajiri unaothaminishwa kuwa sawa na Dola za Marekani milioni 120 (Sh.bilioni 288).
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes katika miongo kadhaa, Afrika imekuwa ikijulikana kuwa bara tajiri kutokana na kujaliwa wingi wa maliasili duniani, lakini mara nyingi wanufaika wakubwa wa rasilimali hizo ni viongozi wake.
IFUATAO NI MTIRIRIKO WA MARAIS 10 MATAJIRI
ZAIDI AFRIKA KWA MUJIBU WA FORBES
1. Mfalme Mohammed VI, Morocco- Dola bilioni 5.9
2. Rais Ali Bongo, Gabon- Dola bilioni 2
3. Rais Teodoro Nguema, Guinea ya Ikweta- Dola Milioni 700
4. Rais William Ruto, Kenya- Dola milioni 510
5. Mfalme Mswati, Swaziland-Dola milioni 500
6. Rais Paul Kagame, Rwanda- Dola milioni 460
7. Rais Cyril Ramaphosa, Afrikakusini-Dola milioni 450
8. Rais Paul Biya, Cameron-Dola milioni 210
9. Rais Abdel Fattah el-Sisi, Misri- Dola milioni 200
10. Isaias Afwerki, Eritrea-Dola milioni 120
0 Maoni