Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wasanii 10 wenye 'maokoto' zaidi Afrika Mashariki 2023

-Diamond, Harmonize, Kiba watajwa

-Profesa Jay, Lady Jay Dee waibuka, Tanzania ikizoa nafasi tano,

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waswahili husema, biashara asubuhi, jioni ni mahesabu. Usemi huu unaweza kuulinganisha na matokeo ya kufunga mwaka ya viwango vya maokoto kwa wasanii wa muziki Afrika Mashariki katika mwaka 2023 unaoishia, yakibainisha wasanii kumi bora, huku Mtanzania Diamond Platnumz, akitajwa kushika nafasi ya pili.

Katika matokeo hayo yaliyotolewa na Jarida maarufu la Forbes, leo Novemba 27, mwaka 2023, pamoja na Diamond Plutnumz, wametajwa pia wengine wanne, wakiwemo wakongwe Professor Jay  na Lady Jay Dee kuwa miongoni mwa wasanii wanaoongoza kwa utajiri Afrika Mashariki kwa mwaka 2023.

Msanii Diamond Platnumz (Picha zote kwa hisani ya Mtandao)

Diamond ametajwa na jarida hilo kushika nafasi ya pili kwa utajiri Afrika Mashariki katika mwaka 2023, kwa kumiliki ukwasi unaofikia Dola za Marekani milioni 9.1. Fedha hizo ni sawa na takriban shilingi bilioni 21.84, akiongoza pia kwa utajiri mbele ya Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa kwenye orodha hiyo.

Matokeo hayo yaliyotajwa kuhusisha pia mtandao wa Ugwire.com, yamemtaja  Diamond Plutnumz kuwa ndiye msanii anayetafutwa na kufuatiliwa zaidi kupitia mtandao wa Google, kuwa na wafuasi wengi zaidi, akiwa pia maarufu zaidi kwenye ukanda huo.

Diamond anatanguliwa na Msanii Bobi Wine wa Uganda, ambaye pia ni mwanasiasa na kiongozi wa upinzani nchini Uganda, aliyewahi kumtikisa Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni wakati alipowania urais nchini humo uchaguzi uliopita mwaka 2021.

Msanii Bobi Wine

Wine anamiliki utajiri unaofikia Dola 9.2 (shilingi bilioni 22.08), akimzidi Diamond kwa takriban shilini milioni 240 pekee.

Katika orodha hiyo, anayeshika nafasi ya tatu ni Mwimbaji Akothee wa Kenya anayetajwa kuwa na utajiri unaofikia Dola milioni 9, sawa na wastani wa shilingi bilioni 21.60, huku wa nne akiwa Jose Chameleon wa Uganda ambaye kwa mwaka 2023 ametajwa kumiliki utajiri wa Dola milioni 8 (shilingi bilioni 19.2).

Msanii Professor Jay

Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa na Forbes ni pamoja na Profesa Jay anayeelezwa kusika nafasi ya tano, ambapo anamiliki utajiri unaofikia Dola milioni 7.5 kwa mwaka huu, ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 18.

Profesa Jay, amefuatiwa na  Msanii Ali Kiba aliyeshika nafasi ya sita, ambaye kwa mujibu wa Forbes, hadi leo Novemba 27, mwaka 2023 ana utajiri wenye thamani ya Dola milioni 7.2, sawa na takriban shilingi bilioni 17.28.

Msanii Ali Kiba

Nafasi ya saba katika orodha hiyo amewekwa Msanii Jaguar kutoka Kenya, anayetajwa kuwa na ukwasi wenye thamani  ya Dola milioni 6.9, takriban shilingi bilioni 16.56 na nafasi ya nane pia imeshikwa na Saut Sol wa nchini humo, wenye umiliki wa Dola milioni 6.8(shilingi bilioni 16.32)

Jarida hilo la Forbes, limemtaja Mtanzania mwingine, Harmonize kushika nafasi ya tisa kwa utajiri Afrika Mashariki katika mwaka huu wa 2023, akimiliki ukwasi wenye thamani ya Dola milioni 6.6 ambazo zikibadilishwa kwa fedha za kitanzania, zitakuwa sawa na takriban shilingi bilioni 15.84.

Msanii Harmonize

Msanii Lady Jay Dee, maarufu kama Binti Machozi  au Komando ndiye aliyefunga ndimba la wasanii 10 matajiri zaidi Afrika Masharikikwa mwaka 2023, akielezwa kumiliki utajiri unaofikia Dola 6.5 ambazo ni sawa na takriban shilingi bilioni 15.60.

Lady Jay Dee ndiye msanii pekee wa kike aliyeingia kwenye orodha hiyo, akiwa pia miongoni mwa wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

Msanii Lady Jay Dee


 

 

 

Chapisha Maoni

0 Maoni