Hot Posts

6/recent/ticker-posts

JOWUTA yawasilisha maoni Kamati ya Nape

-Wataka waandishi waungane kudai na kulinda maslahi

Mwandishi Wetu, daimatz@gmail.com

Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimekabidhi maoni yake kuhusu hali ya uchumi kwa vyombo vya habari na wanahabari mbele ya Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi wa Vyombo vya Habari Tanzania.

Ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Suleiman Msuya, aliyeongozana na Naibu wake, Said Mmanga na Mjumbe wa Bodi ya chama hicho, Careen Tausi Mbowe, JOWUTA ilikabidhi maoni yake leo Novemba 7, 2023 kwa Mjumbe wa Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi kwa Vyombo vya Habari na Waandishi, Sebastian Maganga.  

Katibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Suleiman Msuya akikabidhi maoni ya chama hicho kwa Mjumbe wa Kamati ya Kupokea Maoni Kuhusu Hali ya Uchumi kwa Vyombo vya Habari na Waandishi, Sebastian Maganga. Wengine pichani ni Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga(Kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya JOWUTA, Careen Tausi Mbowe.Kulia ni Mtaalam wa Kamati, Dk. Abdallah Katunzi.


Akizungumza baada ya kukabidhi maoni hayo, Msuya amesema: "Tunashukuru kupata fursa, sisi JOWUTA kwa mujibu wa sheria, ndiyo tunawajibika moja kwa moja kwa waandhishi wa habari kisekta. Katika mukhtadha huo, tumeona mambo matatu hayajazingatiwa. Sheria ya Ajira kazini inataka kila mtu akifanya kazi miezi mitatu apewe mkataba, lakini haipo hivyo wa waandishi wengi."

Alifafanua: "Pili, pia sheria ya uwekezaji tumeona haikuzingatiwa, mtu anapowekeza kwenye vyombo vya habari hicho ni kiwanda, kinakuwa na wafanyakazi wa vitengo mbalimbali, ambavyo baadae vitaiwezesha Serikali kupata kodi ya asilimia 10, (pay as you earn), hivyo kuchangia maendeleo ya Taifa, lakini kwa kuwa wanahabari wengi hawana mikataba ya ajira, hilo la kuchangia halipo. Wanahabari hawachangii pato la taifa, kwani hawana mishahara. Tunaomba Serikali isaidie kusimamia eneo la uwekezaji kwenye sekta ya habari ili nao wachangie uchumi moja kwa moja."

Katibu Mkuu huyo wa JOWUTA, amewataka wanahabari kutojirahisisha wanapotafuta ajira, badala yake kushikamana kwa nguvu moja katika kudai na kulinda maslahi yao.

"Lakini jingine muhimu wanahabari tusiwe rahisi, lazima tushikamane tuwe na nguvu moja katika kusimamia maslahi na haki zetu," amesema Msuya.

Januari 24, mwaka huu 2023, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nauye alitangaza kuunda tume ya watu tisa, ambao  wataofanya kazi ya Kutathimini hali ya uchumi katika vyombo vya habari nchini.

Mbele ya waandishi wa habari, Waziri Nape alitangaza kamati hiyo  Jijini Dodoma, akieleza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alimuagiza kushughulikia suala la uchumi kwenye vyombo vya habari.

Aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni pamoja na Mtendaji Mkuu Azam Media Group, Tido Mhando ambaye ni Mwenyekiti, huku katibu wa kamati hiyo akiwa Gerson Msigwa, aliyekuwa Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Wajumbe wa kamati hiyo ni pamoja na Bakari Machumu( Mkurugenzi Mtendaji MCL), Joyce Mhavile (Mkurugenzi Mtendaji ITV na Redio One), Dk. Rose Reuben (Mkurugenzi Mkuu TAMWA) na  Keneth Simbaya (Mkurugenzi Mtendaji UTPC).

Wengine ni Sebastian Maganga (Mkuu wa Maudhui Clouds Media), Jacqueline Woiso (Mkurugenzi Mtendaji Multichoice Tanzania) na Richard Mwaikenda Mwandishi wa kujitegemea.

Awali, katika maelezo yake kuhusu kamati hiyo Waziri Nape alisema: "Baada ya majadiliano, tumefikia uamuzi wa kuunda timu ambayo itakwenda kufanya kazi ya kutathmini hali ya uchumi wa vyombo vya habari,wanahabari na kuleta mapendekezo." 



Chapisha Maoni

0 Maoni