-Wakandarasi ' watemeshwa bungo'
Mwandishi Wetu,Kigoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kigoma (TAKUKURU) imebaini upungufu mkubwa katika miradi 33 yenye thamani ya shiligi bilioni 12.5, iliyoifuatilia, ikionyesha kuwa chini ya kiwango.
Kufuatia uchunguzi huo, wazabuni wawili waliobanwa na Takukuru, mmoja amerudisha fedha zadi ya shilingi milioni 125 na mwingine kuwasilisha mabati mapya kwenye mradi.
Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa Kigoma, Leonida Mushama amesema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji ya taasisi Takukuru mkoani humo kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba mwaka huu.
![]() |
Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma Mkoa Kigoma, Leonida Mushama akiwasilisha taarifa ya Takukuru mkoani humo. |
Mushama amesema kuwa katika miradi hiyo pia ipo miradi ya ujenzi wa madarasa inayotekelezwa kwa mpango wa BOOST, yenye thamani ya takriban shilingi bilioni tatu.
Amesema Takukuru imebaini upungufu kwenye ununuzi wa mabati yenye thamani ya shilingi milioni 241.3 katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Halmashauri ya Wilaya Kasulu.
Tayari Takukuru imeanzisha uchunguzi kwa ajili ya kuchukua hatua kwa watumishi wa halmashauri hizo waliotajwa kuhusika na tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Mushama, katika hatua za awali, Mzabuni wa Kampuni ya Kiboko katika Halmashauri ya Wilaya Kasulu aliwasilisha mabati mengine yenye viwango yenye thamani ya shilingi milioni 129 wakati yule wa Kampuni ya HERICON katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu alirudisha fedha.
Amesema Mushama kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na wataalam wa halmashauri kuwa na watu wao kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi ambao huelekeza kamati za ujenzi na usimamizi wa miradi kwenda kununua vifaa kwa watu hao kwa ajili ya maslahi binafsi ya wataalam hao wa halmashauri.
Miradi mingine iliyochunguzwa na TAKUKURU ni pamoja na ujenzi wa madarasa saba yenye thamani ya shilingi milioni 195.2 wilayani Kakonko, ujenzi wa shule mpya ya Msingi Kazilamihunda wilaya ya Kakonko wenye thamani ya shilingi milioni 361.5 na.
Aidha miradi mingine iliyochunguzwa na kukutwa na mapungufu ni ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na matundu 22 ya vyoo shule ya msingi Mahembe na ukarabati wa nyumba tano za walimu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 180.
0 Maoni