WAZIRI MKUU AIPA RAMANI TEF KUTEKELEZA DIRA 2050

-Asema bila sekta binafsi imara uchumi imara hautafikiwa

-Ataka vyombo vya habari visaidie wananchi waelewe umuhimu wa sekta binafsi

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba ametoa rai kwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Vyombo vyote vya nchini kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha wananchi watambue na kuelewa umuhimu wa sekta binafsi nchini katika kujenga uchumi imara wa taifa akieleza kuwa bila sekta binafsi imara Tanzania haitaweza kuwa na uchumi imara.

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Novemba 26, 2026 mkoani Morogoro.

Amesema Wahariri wa Vyombo vya habari wana jukumu kubwa la kusaidiana na Serikali kujenga mtazamo sahihi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga uchumi imara, akiwahimiza pia wahariri kutumia vyombo vyao vya habari kuimarisha umoja wa kitaifa, kupambana na rushwa na kuhimiza uwajibikaji katika jamii.

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jukwaa la Wahariri (TEF), mkoani Morogoro Novemba 26,2026 ambapo amesema pia vyombo vya habari nchini vina nafasi muhimu katika kuelimisha watanzania kuhusu umuhimu wa sekta binafsi.

"Hatuwezi kujenga uchumi imara katika mazingira ya sasa bila sekta binafsi imara. Lazima tuibebe sekta binafsi, hatuwezi kuiacha. Tusaidiane kuueleza umma jambo hili. Tuunganishe nguvu tulifanye hilo," amesema Waziri Mkuu Dk. Nchemba.

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Dk. Deodatus Balile alipowasili Hoteli ya Morena mkoani Morogoro wa ajili ya kufungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Novemba 26, 2026 mkoani Morogoro.

Amefafanua kwamba bado kuna kazi kubwa ya kujenga mtazamo sahihi kuhusu sekta binafsi nchini kutokana na ukweli mkwamba bado kuna watu wanaoamini jambo likifanywa na sekta ya umma linaonekana kuwa la kizalendo, lakini likifanywa na sekta binafsi linatiliwa shaka likibebeshwa mtazamo wa kuwepo udanganyifu au wizi.

“Mtazamo huo upo ndani ya Serikali, ndani ya sekta binafsi yenyewe na hata katika vyombo vya habari. Tunapaswa kuubadili. Hatutaweza kujenga uchumi wa nchi yetu kwa majira ya sasa bila kuwa na sekta binafsi imara.”

Mkutano Mkuu wa Tisa wa Mwaka wa TEF, unafanyika ukiongozwa na kaulimbiu isemayo; “Taaluma ya Habari Kujenga Umoja wa Kitaifa na Uchumi wa Vijana Kupitia Dira 2050,” Waziri Mkuu amesema hiuo ni kaulimbiu muafaka katika wakati muafaka.

Akizungumzia kauli mbiu hiyo Waziri Mkuu amesema inagusa maeneo muhimu ya Taifa letu, ikiwemo taaluma ya habari, umoja wa kitaifa, uchumi wa vijana na utekelezaji wa Dira 2050.

"Ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta binafsi ni ya umuhimu sana katika uzalishaji, uwekezaji na kuongeza ajira. Kila mwaka kuna wahitimu wa ngazi mbalimbali kati ya milioni 1.5 na milioni 2, wote hawawezi kuajiriwa na Serikali. Zamani wahitimu walikuwa wachache kiasi kwamba Serikali iliweza kuwaajiri karibu wote, lakini sasa hali ni tofauti," amesema Dk. Nchemba na kuongeza:

 “Lazima tujenge sekta binafsi itakayozalisha ajira, inayoongeza uzalishaji pia kuchangia pato la taifa, laikini pia tunapaswa kuwa na wakandarasi wazawa wenye uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa, ili fedha zinazotumika kwenye miradi hiyo ziendelee kuwepo kwenye mzunguko wa uchumi wetu ndani ya nchi yetu.”

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa TEF, Dk. Deodatus Balile alisema kuwekeza kwenye vyombo vya habari ni kuwekeza kwenye amani, utulivu na maendeleo na kwamba TEF inaweza kuisaidia Serikalikatika eneo hilo kutokana na ukweli kwamba Taifa lenye vyombo vya habari imara linaweza kupunguza gharama za kusimamia sheria, kukusanya kodi, kupambana na rushwa na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Dk.Balile amesema habari sahihi pia zinaweza kuzuia migogoro kabla haijatokea na kusababisha madhara makubwa kwa maisha na rasilimali za Taifa na kwamba mwananchi anapoelimishwa vizuri kuhusu wajibu wake wa kulipa kodi, hahitaji kulazimishwa kila wakati. 

"Vyombo vya habari vinapochapisha habari za uchunguzi, vinaweza kusaidia kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kutokana na ubadhirifu na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za umma,” amesema Dk. Balile.

Kuhusu mikakati ya TEF Dk. Balile ameeleza kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha programu atamizi ya kuwalea waandishi wa habari vijana ikitumia wahariri wakongwe na wastaafu kwani wanataka kujenga kizazi cha wanahabari kinachoweza kutofautisha habari zilizothibitishwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni.

Kwa mujibu wa Dk.Balile, TEF inatambua mchango wa mitandao ya kijamii katika kusambaza taarifa kwa haraka, hata hivyo taifa lisipowekeza kwenye matumizi sahihi ya teknolojia, mitandao inaweza kutumiwa kuchochea chuki na migawanyiko, badala ya kujenga umoja wa kitaifa. 


Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi