MAKAMU WA RAIS ATOA SIKU 14 ATAKA VIJANA 10,000 'WAFUNDWE' TAASISI ZA UMMA

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, (pichani chini)ametoa wiki mbili kwa Wizara ya Mipango, Kilimo na Fedha akizitaka ziandae mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa vijana 10,000 katika taasisi na mashirika ya umma ili wafanye mafunzo kwa vitendo huku, ambao baadae watasaidia kuongeza uzalishaji na tija kwenye maeneo hayo kusaidia kufikia lengo la Dira ya taifa 2050.

Makamu wa Rais pia ameagiza vijana wengine 20,000 wakapatiwe mafunzo kama hayo katika sekta binafsi, akieleza ndiyo nia itakayolisaidia taifa kufikia malengo yake.

Akizungumza katika ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma C-CEOs Forum 2026 jijini Arusha leo Septemba28,2026 ambapo alimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,  Makamu wa Rais amesema; "Mpango huo utawajengea vijana uzoefu wa kuajirika na kujiajiri, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050."

Katika hotuba yake iliyojaa mifano ya matumizi ya fedha katika mashirika yanayoweza kupunguzwa na kutumika katika kuwajengea uwezo vijana, Ndijembi ameyataka mashirika ya umma kubana matumizi yasiyo ya lazima, kuongeza tija, kuwa injini ya mageuzi ya uchumi na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.

 
" Kila mwaka kwa takribani vijana 62,570 wanahitimu elimu ya juu na hii ni takwimu ya mwaka jana 2025 toka TCU, idadi hiyo haihusishi wale wanaomaliza VETA na vyuo vya kati. Ukiangalia TAESA takwimu zao zinaonesha vijana  3,200 pekee walikuwa wamepitia programu za mafunzo internship, idadi hii ni ndogo sana kwa kulinganishwa na wahitimu  62,570 kutoka vyuo mbalimbali nchini. 
Mlitazame hili kama uwekezaji wa kimkakati katika nguvu kazi ya Taifa kwa kubana matumizi ya kawaida, hapa mtakuwa mmetekeza kwa vitendo nguzo ya pili ya Dira 2050," amesisitiza
 
Ndejembi, amesema dhamana ya Watendaji, Wakuu wa Mashirika na Wenyeviti wa Bodi ni kubwa, hivyo wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na umakini mkubwa na kwa wakati sahihi ili kujenga uchumi, kuibua fursa mpya na kuinua maisha ya watanzania.

 "Mashirika ya Umma yana nafasi ya kipekee katika kufikia malengo ya Dira 2050 kutokana na dhamana yake ya kusimamia mali za umma, kuendesha miundombinu ya kimkakati, kutoa huduma muhimu za nishati, usafirishaji, mawasiliano, fedha, afya, maji na nyingine zinazobeba uchumi wetu. Lazima tuyaangalie mashirika hayo kama injini ya mageuzi makubwa ya kiuchumi tunayoyalenga katika Dira 2050,” amesisitiza Makamu wa Rais.
 
Makamu wa Rais pia amezitaka taasisi na mashirika ya umma kubuni vyanzo endelevu vya mapato na kuhakikisha kila shilingi ya umma inaleta thamani inayostahili.  
 
Ndejembi ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha mfumo wa tathmini ya utendaji wa mashirika ya umma na kutambua kwenye tuzo za mwaka ujao Taasisi zitakazotekeleza agizo la kuchukua vijana na kuwapa mafunzo.
 
Amezitaka taasisi na mashirika ya umma  kujiandaa mapema kukabiliana na athari za mvua za El Niño ili kulinda miundombinu na uwekezaji wa umma na kuhakikisha huduma muhimu kwa wananchi haziathiriki.

 Kikao hicho cha nne cha C-CEOs Forum 2026 kimewakutanisha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, pamoja na Mawaziri, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Makatibu Wakuu na viongozi wengine wa Serikali.  
 
Kikao hicho cha siku tatu kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kutoa mwelekeo wa kimkakati kuhusu mustakabali wa Mashirika ya Umma, kutathmini yalipotoka na kujadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuongeza mchango wake katika uchumi na maendeleo ya Taifa, hususan wakati Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi