-Wasema wamezungumza wanayajenga
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu imetoa ufafanuzi kuhusu malalamiko yaliyojitokeza kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa mkandarasi, Frank Mwakajumba kuhusiana na malipo ya deni lake.
Mkandarasi huyo alitekeleza kazi ya kutengeneza milango 147 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkapa kwa gharama ya jumla ya Shilingi 45,900,000, ambapo hadi sasa amelipwa Shilingi 15,000,000 na kubakiwa na deni la Shilingi 30,900,000.
Kwa upande wake, Afisa Mipango wa Halmashauri, Rudrick Charles, alisema kuwa amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na mkandarasi huyo, ikiwemo miezi ya Januari na Februari 2026, ambapo alimhakikishia kuwa malipo yake yatatekelezwa mwezi Julai, na mkandarasi alikubaliana na utaratibu huo.
“Nimekuwa nikizungumza naye mara kadhaa kuhusu suala hili na tumekuwa tukikubaliana. Hivyo, tumeshangazwa kuona malalamiko yakitolewa kupitia mitandao ya kijamii ilhali tayari tulishafikia makubaliano,” alisema Charles.
Naye mkandarasi Frank Mwakajumba alikiri kuwepo kwa mazungumzo hayo na kwamba alishakubaliana na Halmashauri kulipwa mwezi Julai mwaka huu.
Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto za kifamilia na madeni zinazomkabili ndizo zilizomsukuma kueleza malalamiko yake hadharani, huku akisisitiza kuwa ana imani Halmashauri itatekeleza ahadi yake ya malipo kwa wakati uliokubaliwa.

Chapisha Maoni