SERIKALI YAKAZIA MACHO UJENZI BARABARA ZA HARAKA KWA MPANGO WA PPP
-Waziri Mkuu awaongoza mawaziri, PPP Center kusonga mbele
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Serikali imeongeza kasi ya kutafuta suluhu ya msongamano wa magari katika barabara kuu kwa kukazia macho ujenzi wa Barabara za Haraka kwa mpango wa ubia, hatua itakayoongeza kasi ya huduma za usafiri na usafirishaji hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Katika kusukuma mbele ajenda hiyo, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba ameongoza kikao cha kazi kuhusu ujenzi wa miradi hiyo ya Barabara haraka (Express Ways), kupitia mfumo wa Ubia Kati ya Umma na Sekta Binafsi nchini (PPP).
Kikao hicho kilichofanyika Januari 17, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kimewajumuisha pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. James Kilabuko, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara pamoja na watendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, David Kafulila.
Kikao hicho kimefanyika wakati tayari Kituo cha Ubia Kati ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), kimeshatangaza zabuni za baadhi ya miradi ya barabara hizo inayosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini, TANROADS, zikiwa katika hatua mbalimbali. Baadhi ya Barabara za Haraka ambazo zabuni zake zimetangazwa ni pamoja na Barabara ya Kasi (Expressway) ya Kibaha – Mlandizi – Chalinze (Lot 1) yenye urefu wa km 78.9
Kwa mujibu wa Mtandao Rasmi wa PPPC, mradi uko katika hatua ya manunuzi (Procurement). Katika maelezo kuhusu mradi huo, PPPC imesema kuwa Barabara ya Kibaha–Morogoro kwa sasa inakabiliwa na msongamano mkubwa wa magari na huduma duni, hali inayohitaji hatua za haraka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.
Imeeleza kwamba Barabara ya Kasi (expressway) inapendekezwa ili kupunguza muda wa safari kutoka Kibaha hadi Chalinze kutoka saa 2 hadi saa 1.
"Mradi utatekelezwa kupitia mpangilio wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambapo watumiaji wa barabara watatozwa ada ya matumizi (tozo). Barabara ya kasi ya kulipia itajengwa sambamba na barabara ya sasa ya Morogoro, hivyo watumiaji wasiotaka kulipa wataendelea kutumia barabara iliyopo," imeeleza PPPC.
Kwa mujibu wa Mtandao huo, utekelezaji wa ujenzi wa Barabara ya Kasi ya Chalinze – Morogoro (Lot 2), uko katika hatua ya utafiti wa upembuzi yakinifu (feasibility study), ambapo mradi husika unahusisha ujenzi wa kipande cha kilomita 128 cha barabara ya kisasa ya kasi kubwa kinachounganisha Chalinze na Morogoro.
Mradi huo umetajwa kuwa ni sehemu ya mpango mpana wa kuendeleza korido ya barabara yenye uwezo mkubwa ili kuboresha ufanisi wa usafiri, kuongeza usalama na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.
Mtandao huo wa PPPC umeeleza kuwa barabara ya kasi imebuniwa kupunguza muda wa safari, kupunguza msongamano kwenye barabara zilizopo na kutoa njia ya moja kwa moja na ya kuaminika kwa usafirishaji wa bidhaa na watu kati ya ukanda wa pwani na maeneo ya ndani ya nchi.
Kituo hichi cha Ubia kati ya Umma na Sekta Binafsi kimeutaja mradi wa tatu wa Barabara za Haraka kuwa ni Korido ya Dar es Salaam iliyoelezewa kuwa ni njia muhimu kwa kurahisisha shughuli za uingizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, na kuchangia ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) la nchi jirani zisizo na bandari.
Korido hiyo inaanzia Bandari ya Dar es Salaam. Barabara ya mzunguko (Bypass) ya Uyole–Songwe inalenga kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Mbeya unaosababishwa na magari mazito ya mizigo, hali inayosababisha muda mrefu wa safari, gharama kubwa za uendeshaji wa magari, na kuongezeka kwa ajali.
PPPC imeeleza kuwa mradi huo utanufaisha mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya
kwa kutoa njia yenye ufanisi zaidi kuelekea Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), na Malawi.





Maoni
Chapisha Maoni