Rais Samia afuta sherehe 9 Desemba
-Aagiza fedha zitumike kujenga miundombinu
- Waziri Mkuu aagiza shughuli zirejee ndani ya siku 10
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameelekeza hakutakuwa na maadhimisho ya Sherehe za Uhuru Desemba 09 mwaka huu.
Maelekezo hayo ya Rais Samia, yametolewa kwa niaba yake na Waziri Mkuu, Dk.Mwigulu Nchemba leo Novemba 24,2025 ambaye amesema Rais ameagiza fedha zilizotengwa ili kutumika katika sherehe hizo, zitumike kurekebisha miundombinu iliyoharibika kutokana vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kuiona Tanzania inakuwa moja na kuendeleza umoja wa Watanzania
Akizungumzia ziara yake Dk.Mwigulu amesema: "Nimepitia na kukagua uharibifu wa mali na miundombinu ya umma, huwezi kuamini kama tukio hili limetokea Tanzania."
Amesema Watanzania wanapaswa kujua miundombinu hiyo ni mali ya umma.
"Tunaijenga kwa fedha zetu sisi watanzania, si pesa za Serikali," amesema.
Waziri Mkuu ametoa maagizo kwa Wizara ya Ujenzi, TANROADS, DART, UDART, OWM-TAMISEMI na wadau wengine kuhakikisha ndani ya siku 10 kuhakikisha shughuli katika jiji la Dar es Salaam kanarejea kama kawaida.
"Wekeni mpango wa haraka wa kurejesha, wakati tunasubiri mpango mkubwa, baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, Watanzania tuilinde miundombinu hii, " ameagiza.
Kuhusu miradi, Waziri Mkuu pia ameagiza wizara na taasisi za Serikali kuwapa kandarasi wakandarasi wazawa kwani wana uwezo.
"Wapatieni kazi wakandarasi wazawa, wana uwezo, hata kazi wanazopewa wageni, wakandarasi wazawa ndio wanafanya hizi kazi," amesema.
Amesisitiza kwamba maeneo ambayo kazi inaweza kufanywa na mtanzania ifanywe na Mtanzania, hata maeneo ambayo biashara inaweza kufanywa na mtanzania ifanywe na mtanzania, akisema kuwa Tanzania ni ya Watanzania.
Waziri Mkuu Dk.Mwigulu ameagiza taasisi za umma na Serikali kuwatimua kazi watumishi wazembe na wala rushwa.
"Mfanyakazi yoyote mzembe na mlarushwa msimhamishe, mfukuzeni kazi, vijana wakitanzania ambao wanafanya kazi vizuri wako wengi," amesema.
Waziri Mkuu ameungana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa wote walioathirika na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025
Amesema: Tumuunge mkono Rais na wajumbe wa tume iliyoundwa kwa ajili kuchunguza kwenye undani tukio la vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, ili tujue namna lilivyofanyika na hatua stahiki zitakazochukuliwa."
.Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, wanaoshabikia uharibifu wa miundombinu ya umma hawapo hapa nchini, lakini wanawaambia vijana wa kitanzania wakachome mali za umma.
"Mkifanya hivi mtaishije? HUko wanakoishi, haya wanayowaambia mfanye huko kwao hauwezi kuyafanya.
Amesema watu hao wanajipa haki kwamba wao wanaipenda Tanzania, lakini ukweli ni kwamba mpenda Tanzania hawezi kumwambia mtu aichome Tanzania.
"Miwasikilize, mkiichoma zaidi Tanzania wao ndio wanalipwa zaidi. Wanashawushi tuchome moto vitu, wanaturudisha kwenye umasikini," amesema Mwigulu.
Ametahadharisha kuwa nchi zote zenye rasilimali nyingi ndizo zinasababishiwa vurugu, akieleza kwamba Tanzania ni nchi yenye rasilimali adhimu ikiwemo gesi na madini na kwamba zitalindwa kwa nguvu zote.
"Watanzania amekeni hawa wanaotushawishi kufanya vurugu hawatupendi, nawaomba vijana wa Tanzania, Mungu ametupa nchi nzuri, tuilinde pamoja na miundombinu yake," amesisitiza Waziri Mkuu Dk.Mwigulu.
Aliwageukia viongozi wa dini akiwataka kuwa makini ya namna watu wanavyotaka kuwagonganisha akawaambia: "Kaeni kwenye vikao vyenu, tuifanye Tanzania yetu iwe pamoja."




Maoni
Chapisha Maoni