NHC yavunja rekodi miradi mikubwa ya makazi inayoibadili Tanzania
- Sh400 bilioni zawekezwa na NHC ikiongoza safari ya makazi bora
-Ni kupitia Samia
Housing Kijichi, Kariakoo PPP na Kawe 711
-Mabilioni
yazalishwa kwenye miradi kabla muda kusudiwa
- Wananchi
waongeza kasi kununua nyumba
-Miradi ya
kimkakati yainua uchumi, yabadili mandhari ya mijini
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limeendelea kujidhihirisha kama nguzo muhimu ya maendeleo ya makazi nchini, likiendelea kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati inayolenga kuwawezesha Watanzania kumiliki nyumba za kisasa kwa gharama nafuu na katika mazingira salama.
| Mradi wa Samia Housing Scheme utakavyoonekana baada ya kukamilika. |
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, NHC
limewekeza nguvu kubwa katika miradi ya ubunifu, teknolojia ya gharama nafuu na
ushirikiano mpana na sekta binafsi, hatua ambayo imeongeza kasi ya upatikanaji
wa makazi ya kudumu na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hali halisi katika maeneo mbalimbali nchini inathibitisha mageuzi haya, ambapo miradi mipya ya makazi, biashara na ofisi inakua kwa kasi, ikijibu mahitaji ya wananchi na kuongeza thamani ya ardhi na uchumi wa maeneo jirani. Miongoni mwa miradi hiyo ni Samia Housing Scheme Kijichi, mradi wa ubia wa Kariakoo, na Kawe 711, yote ikiwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam ikibeba thamani ya pamoja inayofikia takriban Sh 441.5 bilioni.
| Mafundi wakiendelea na kazi katika Mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi Dar es Salaam. |
Miradi hii
imekuwa mfano halisi wa utekelezaji wa Dira ya Serikali ya kuhakikisha
Watanzania wanapata makazi bora, salama na endelevu—ikiendana na mabadiliko
yanayoendelea ya ukuaji wa miji, ongezeko la watu na mahitaji mapya ya
miundombinu ya kisasa.
Miradi inayobadilisha
taswira ya Dar
Katika Jiji la
Dar es Salaam, NHC inaongoza kwa kasi utekelezaji wa miradi yenye athari pana
kijamii na kiuchumi. Kwa upande mmoja, miradi hii inawapa Watanzania makazi
bora, na kwa upande mwingine, inaongeza mapato ya Serikali kupitia kodi, gawio
na ada mbalimbali zinazotokana na shughuli za biashara na uuzaji wa nyumba.
Samia
Housing Scheme Kijichi: Mradi mpya wa makazi bora yaliyopangwa kitaalam
Mhandisi Julieth Prosper, anayesimamia Mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi, anabainisha kuwa mradi huu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya NHC yenye malengo mapana ya kuboresha mandhari ya eneo la Kijichi na kufungua fursa za kiuchumi huku ukitoa makazi ya kisasa kwa wananchi.
| Mhandisi Julieth Prosper wa Mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi, akitoa maelezo kuhusu mradi huo |
Mradi
unatarajiwa kuwa na majengo 12 yenye jumla ya nyumba 260, zilizogawanywa katika
makundi matatu: Nyumba za vyumba vitatu – majengo 5, nyumba za vyumba viwili –
majengo 5 na nyumba za chumba kimoja – majengo 2.
Nyumba zote
zitakuwa na sebule pana, jiko la kisasa na miundombinu ya msingi ambayo
inakidhi mahitaji ya familia za kitanzania.
Kwa mujibu wa Mhandisi Elias John, mradi pia unajumuisha maegesho ya magari 300, sambamba na nafasi za ziada 40 kwa matumizi ya dharura au wageni. Aidha, kutakuwa na jengo la huduma za kijamii lenye maduka, sehemu za huduma za kifedha kama ATM na huduma nyingine muhimu.
| Mhandisi Elias John msimamizi wa Mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi akifafanua jambo kuhusu mradi huo. |
Mauzo ya nyumba, mwitikio wa wananchi
Ofisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa NHC, Daniel Kure, anasema kuwa mwitikio wa wananchi ni wa kuridhisha, ambapo ndani ya muda mfupi tangu uzinduzi, asilimia 15 hadi 20 ya nyumba tayari zimeuzwa. Uwepo wa fursa za malipo kwa awamu na mikopo ya benki kupitia mifumo ya Mortgage umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi ya wanunuzi.
![]() |
| Daniel Kure |
Kure anafafanua kuwa kuna njia tatu za kufanya malipo: Malipo ya fedha taslimu kwa awamu kuanzia asilimia 10 ya thamani ya nyumba, malipo ya awamu kwa kipindi cha miezi 6 hadi miaka miwili na mkopo wa benki (Mortgage) kupitia zaidi ya taasisi 20 za fedha ambazo tayari zimeingia makubaliano na NHC.
Kwa mfano, mteja anayehitaji nyumba ya Sh milioni 220, anachohitaji kuanza nacho ni Sh milioni 22 tu kama malipo ya awali, kisha taasisi za fedha zikachukua jukumu la kukopesha salio.
Kuhusu bei za nyumba, NHC imeweka wazi kiwango cha ununuzi kama ifuatavyo: Chumba kimoja cha kulala– Sh 112 milioni, vyumba viwili – Sh 220 milioni na vyumba vitatu vya kulala– Sh 335 milioni
Kure anahimiza
wananchi kuchangamkia fursa hii, akisema kuwa licha ya wengi kuamini kuwa
Kijichi ni mbali, kiuhalisia mradi uko karibu na jiji. Ni takriban kilomita 15
kutoka katikati ya Dar es Salaam kupitia Barabara ya Kilwa hadi Mbagala
Misheni, au kupitia Daraja la Kigamboni–Kibada.
Anasisitiza kuwa mradi huu utabadilisha sura ya Kijichi kwa kuongeza shughuli za biashara, uwekezaji na makazi ya kisasa na hivyo kuwa moja ya miradi yenye thamani kubwa kwa mustakabali wa eneo hilo.
Mradi wa
ubia Kariakoo unavyoonesha nguvu ya ushirikiano
Meneja wa
Miradi ya Ubia wa NHC, Elizabeth Maro, anaeleza kuwa mradi wa Kariakoo ni
ushahidi tosha kwamba ubia kati ya NHC na sekta binafsi una uwezo mkubwa wa
kuharakisha maendeleo.
Mradi huu
ulioanza mwaka 2024, una thamani ya Sh271 bilioni, ukitekelezwa kwenye ardhi
yenye thamani ya Sh59 bilioni, unahusisha mikataba 21, ambapo kati ya hiyo miradi
5 ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji na mingine mitano ikiwa tayari
imepata kibali cha matumizi.
Cha kuvutia zaidi ni kwamba, ingawa makadirio ya awali yalikuwa kwamba miradi itaongeza mapato ndani ya miaka miwili, tayari mapato yameanza kupatikana ndani ya mwaka mmoja tu, jambo linalodhihirisha ufanisi wa ubia huu.
![]() |
| Sehemu ya majengo ya miradi ya ubia |
Elizabeth
anaeleza kuwa NHC inaendelea kupokea maombi mengi ya ubia, zaidi ya 100
hadi sasa, hali inayoonyesha imani kubwa ya wawekezaji na watumiaji wa mali
katika Shirika hilo.
Anaeleza kuwa tathmini ya
awali ilionyesha kuwa miradi 21 ingeweza kuingiza Sh bilioni 2 kwa mwaka,
lakini kwa utekelezaji wa sasa ambao umefikia asilimia 25 pekee, mapato
yanatarajiwa kufikia Sh bilioni 6 kwa mwaka.
"Hii ina maana kuwa Serikali itanufaika zaidi kupitia kodi, gawio, na uchochezi wa uchumi katika eneo la Kariakoo ni kitovu kikuu cha biashara Tanzania," amesema Elizabeth.
| Meneja Miradi ya Ubia NHC, Elizabeth Maro |
KAWE 711: Majengo
ya kisasa, viwango vya kimataifa
Kwa upande wa
mradi wa Kawe 711, Kure anaeleza kuwa ni moja ya miradi mikubwa zaidi
inayotekelezwa na NHC kwa sasa ukiwa na thamani ya shilingi 169 bilioni. Mradi huo unajumuisha nyumba 400 katika majengo ya ghorofa
17, ukiwa umbali wa takriban mita 300 kutoka baharini.
Hadi sasa,
ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 60, na kazi za umaliziaji zinaendelea
kwa kasi. Mauzo ya nyumba yanaendelea vyema, huku wananchi wengi wakijitokeza
kuona na kununua nyumba baada ya kushuhudia maendeleo ya ujenzi.
Mradi huo unajumuisha
nyumba za vyumba viwili, vitatu na vine, eneo kubwa la maegesho, maduka, maeneo
ya michezo, mabwawa makubwa ya kuogelea, maeneo ya mazoezi, na huduma za
kibenki.
NHC inapanga
kukabidhi nyumba kwa wanunuzi walio kamilisha malipo kufikia Aprili 2026.
Faida za
kiuchumi
Miradi
inayotekelezwa na NHC inatoa mchango mkubwa katika kuongeza ajira kwa vijana, uibua
biashara ndogo na za kati katika maeneo yanayozunguka miradi, kuongeza thamani
ya ardhi, kuongeza usalama, ustaarabu na thamani ya kijamii kwa kuwapatia
wananchi makazi bora, pia kuchangia pato la taifa kupitia kodi na gawio la
Serikali
Hakuna wa kupinga kwamba NHC inasonga mbele kama mhimili wa mageuzi ya sekta ya makazi nchini, ikiweka misingi imara ya maendeleo ya miji na kupunguza changamoto ya uhaba wa nyumba bora hapa Tanzania.
![]() |
| Mradi wa Nyumba wa Kawe 711 |



Maoni
Chapisha Maoni