Majaliwa amwakilisha Rais Samia Mkutano wa ACTIF 2025 Grenada

Mwandishi Wetu,daimatzanews@gmail.com

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yupo mjini St. George’s, nchini Grenada ambapo anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum - ACTIF 2025) unaofanyika kuanzia leo Julai 28 hadi 30, 2025 katika kituo cha mikutano cha Radisson.

Lengo la mkutano huo mkubwa ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Afrika na Visiwa vya Karibiani, ukiongozwa na kaulimbiu isemayo “Uhimilivu na Mabadiliko: Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Afrika na Karibiani katika Kipindi cha Changamoto za Kidunia.”

Taarifa zinasema, Waziri Mkuu atashiriki mjadala wa Mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali, kukutana na viongozi wa mataifa mengine, pamoja na kushiriki katika mikutano ya uwili na wawekezaji wakubwa, dhamira ya Tanzania ikiwa ni kuendeleza juhudi zake za kuvutia wawekezaji wa kimataifa, ili kusaidia kujenga uchumi wa kisasa na shindani duniani.

Ushiriki wa Waziri Mkuu Majaliwa katika mkutano huo akimwakilisha Rais Samia ni mwendelezo wa dhamira ya dhati ya kuimarisha Diplomasia ya Uchumi kwa kuifungua nchi kimataifa na kuimarisha ushirikiano, ili kuchochea maendeleo jumuishi kwa Watanzania wote. 

Baadhi ya maeneo muhimu yanayotajwa kujadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na kuanzishwa kwa eneo la Biashara Huria kati ya Afrika na Karibiani, kuimarisha Baraza la Biashara la Afrika na Karibiani, kuchochea uchumi na ubunifu pamoja na kukuza uhusiano wa usafiri wa anga na baharini kati ya Afrika na Karibiani.

Mkutano huo umeratibiwa na Granada pamoja na taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye lengo la kukuza biashara ya bidhaa na huduma ndani na nje ya Afrika (Afreximbank).

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi